51Թ

Kijana rubani wa meli atenda kinyume na matajario

Get monthly
e-newsletter

Kijana rubani wa meli atenda kinyume na matajario

Mfahamu Elizabeth Marami, rubani wa meli wa kike wa kwanza nchini Kenya
Raphael Obonyo
Afrika Upya: 
1 June 2023
Elizabeth Marami, Kenya’s first female marine pilot.
Elizabeth Marami, rubani wa kwanza mwanamke wa baharini nchini Kenya.
Ikiwa huwezi kusoma sasa, sikiliza tu toleo la sauti: 
Sauti iko kwa Kiingereza.

Elizabeth Wakesho Marami analeta mabadiliko katika tasnia ya ubaharia inayotawaliwa na wanaume. Katika Siku ya Kimataifa ya Wanawake wa Baharini iliyoadhimishwa Mei 18, alizungumza na Raphael Obonyo kutoka Afrika Upya, akiwa katika safari yake ya kazi: Haya hapa ni madondoo:

Afrika Upya: Je, wewe ni nani?

Mimi ni rubani wa meli aliye na cheti kutoka Uingereza cha Chief Mate unlimited/Master 3000GT, nina uzoefu mpana wa ubaharia nimefanya kazi kama gwiji, rubani wa pili na kwenye meli za mizigo.

Kwa sasa ninafanya kazi na meli za watalii kama afisa wa 1 katika Kundi la Watu Mashuhuri la Royal Caribbean Cruises.

Mimi pia ni mwanzilishi wa Against the Tide Foundation wakfu ambao unalenga kuwatambulisha mabaharia wanawake kwa kuangazia changamoto zao kupitia hadithi za kidijitali.

Nina umri wa miaka thelathini na tano.

Ulizaliwa na kukulia wapi na historia yako ya elimu ni ipi?

Nilizaliwa na kukulia katika bandari ya Mombasa, pwani ya Kenya. Nilisomea Shule ya Msingi ya Loreto Convent kisha Shule ya Upili ya Wasichana ya Mama Ngina, zote zikiwa Mombasa. Baada ya shule ya upili nilisomea Shahada ya Kwanza ya Sayansi katika Teknolojia ya Usafiri wa Majini katika Chuo cha Kiarabu cha Sayansi, Teknolojia na Usafiri wa Baharini (Arab Academy for Science, Technology & Maritime Transport) huko Alexandria, Misri.

Pia nina Stashahada ya Juu ya Kitaifa (HND) katika Sayansi ya Baharini kutoka Chuo cha Bahari cha Warsash nchini Uingereza.

Kwa sasa ninamalizia Shahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Biashara katika Chuo Kikuu cha Nairobi, nchini Kenya.

Uliingiaje katika sekta ya ubaharia?

Nilikulia Mombasa, ambacho ni kisiwa, kila mara niliona meli zikiingia na kutoka bandarini, lakini sikuwahi kufikiria kabisa kufanya kazi kwenye meli kwani niliona kuwa ni kazi ya wanaume tu.

Kwa hivyo, baada ya shule ya upili nilipopata ufadhili wa masomo mnamo 2009 kusomea Teknolojia ya Ubaharia huko Misri, sikuwa na ufahamu wake kabisa. Lakini siku zote nilijua nataka kuwa tofauti, kuwa wa kwanza katika jambo fulani, na ndivyo ilivyokuwa.

Marafiki na familia walijaribu kuzungumza na familia yangu ili kuniruhusu kuendelea na masomo ya ubaharia lakini ninakumbuka waziwazi siku moja baba yangu aliniambia kuwa lilikuwa chaguo langu kulifanya. Siku iliyofuata nilikuwa kwenye basi pamoja na mama yangu kuelekea Nairobi kughairi usajilishaji wangu katika kitivo cha sheria cha Chuo Kikuu cha Nairobi. Sijawahi kujuta tangu wakati huo.

Rubani wa Meli ni Nani?

  • Rubani wa meli ni mtaalamu aliyefunzwa sana ambaye husafiri na kuendesha meli kupitia njia tata za maji, bandari na ufuoni.

Nahodha wa Meli ni nani?

  • Nahodha wa Meli ni mtu aliyepatiwa leseni na ambaye ana uwezo kudhibiti urambazaji wa meli, mawasiliano na utunzaji salama wa meli.

Kuna tofauti gani kati ya Nahodha na Rubani wa meli?

  • Nahodha wa Meli huendesha meli kwenye kina kirefu cha bahari, Rubani wa Meli husaidia kuendesha meli kupitia njia tata za maji hadi bandarini.
  • Wakati Nahodha wa Meli akiendesha meli majini, hali inapokuwa hatari au kuna hali yoyote inayohitaji ustadi mkubwa katika uendeshaji wa meli, Rubani wa Meli hutoa ushauri kuhusu njia ya kutumia na mabadiliko gani yanapaswa kufanywa wakati wa kuingia au kuondoka bandarini.

Je, ulikuwa na wasiwasi kuhusu sekta ya ubaharia kutawaliwa na wanaume?

Kwa hakika, nilikuwa na wasiwasi, lakini nilikulia katika familia ya wasichana watatu na mvulana mmoja. Kwa hivyo, majukumu ya kijinsia hayakuwa mada tuliyojadili kwa kuwa ilikuwa kawaida kwetu sote kurekebisha kinasa mawimbi cha runinga yetu, kusafisha gari na kufanya kazi nyingine za nyumbani.

Majukumu ya kijinsia hayakuwepo akilini mwangu, na nilibeba mawazo hayo hadi kwenye tasnia hii. Nilichojua ni kwamba nilihitaji kukamilisha kazi hiyo. Na niko hapa leo, ni mimi yuleyule, nikitia bidii kazini kuhakikisha kwamba ninaiacha ikiwa mahali pazuri kwa wasichana wadogo ambao watakuja baada yangu.

Ninapanda mti ambao siwezi kamwe kukaa kwenye kivuli chake - hilo ndilo jambo ambalo kwangu ni kutetea uwakilishi wa jinsia 50:50 katika tasnia ya ubaharia.

Je, unaweza kuelezeaje maendeleo yako ya kikazi kufikia sasa?

Nikipiga darubini nyuma, kule haya yote yalipoanzia hadi chuo kikuu huko Misri mwaka wa 2009, napata furaha. Nimetumia vizuri fursa nilizozipata na ninahisi kwamba maarifa, ujuzi na uzoefu ambao nimepata kwa miaka mingi unaendelea kunisukuma mbele. Kwa ujumla, nimeridhika na maendeleo yangu ya kikazi.

Kazi yako ya kila siku inahusu nini?

Inahusu kile tunachokiita “kukaa macho”, ambako kuna maana kwa urahisi kuwa ninawajibika, kudhibiti na kuelekeza meli kwa usalama wakati wa zamu yangu, ambayo ni kati ya saa mbili asubuhi na saa sita adhuhuri na kati ya saa mbili usiku na sita usiku.

Majukumu na wajibu wangu mwingine unajumuisha kuhakikisha uzingatiaji wa kanuni za usalama, sheria za mazingira; kupiga ripoti matukio muhimu; kufuata sera na taratibu za urambazaji; na kudumisha muda ufaao wa kupumzika.

Pia ninamsaidia Afisa wa Usalama katika kutunzavifaa vya usalama, kuendesha mafunzo ya usalama na kufanya hesabu za uthabiti.

Nafasi hii inahitaji uhitimu maalumu, ikiwemo uidhinishaji unaofaa, uweledi wa lugha na uwezo wa kimwili kwa taratibu za dharura.

Je, meli unayoshughulikia kwa sasa ina ukubwa kiasi gani?

Kwa sasa, ninafanya kazi katika Celebrity Cruises’ Celebrity Beyond - meli kubwa na ya kifahari yenye tani 140,660 za jumla.

Unafanya nini wakati hauko baharini?

Ninatumia muda wangu kuandika hadithi za mabaharia wanawake; kusoma zaidi kuhusu tasnia ya ubaharia; na kutafuta njia au tuseme suluhisho za jinsi ya kuwasaidia vijana wanaotaka kuwa mabaharia.

Vilevile, niko huru kushiriki katika mazungumzo ya kuunda mustakabali wa vijana wa Kiafrika katika ubaharia.

Je, ungependa kuwapa ushauri gani wasichana na wanawake kwa ujumla ambao wangependa kujiunga na sekta ya ubaharia?

Wajiunge. Kuna mabadiliko makubwa, wewe binafsi ndiye mabadiliko hayo. Hakuna kisichowezekana. Jiamini na ujitahidi kuwa bora zaidi.

Kila kitu ni hatua za kujifunza, hakuna mtu aliyezaliwa akifanya chochote ipasavyo, kwa hivyo una uwezo kamili.Chukua hatua ya imani na ujiunge na tasnia hii.

Ukweli kwamba umekuwa mwanzilishi na ukafaulu katika kazi yako unavutia. Je, kumekuwa na changamoto na hukabiliana nazo vipi?

Sitaki kupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa na kusema kwamba safari ilikuwa rahisi. Sivyo kwa kabisa!

Tatizo la kwanza lililonikabili ni kukataliwa kwa nafasi nyingi za kazi, lakini nilijua nilichohitaji ni kukubaliwa, kisha nilete mabadiliko, kwa hivyo, kamwe singekata tamaa.

Hakika sikuwahi kufikiria ningejipata nikifanya kazi kwenye meli za kitalii. Nina picha zangu nilizopigwa nikiwa na meli za kitalii kwa kuwa nilikuwa na hakika kwamba hazingeajiri mtu kama mimi.

Kisha siku moja nikaomba kazi katika Shirika lisilo la faida la Marine Stewardship Council (MSC) na nikaipata.

Nilifikiri ningekuwa nikifanya kazi kwenye meli zao za mizigo kwa kuwa huo ndio ulikuwa uzoefu na tajriba yangu, lakini niliishia kupewa kazi kwenye meli zao za kitalii.

Ndipo nilipojiambia, ‘Huyu ndiye Liz, ni wakati wako wa kung’aa.’