51³Ô¹Ï

'Lengo letu ni chanjo ya haraka kwa Waafrika milioni 800'

Get monthly
e-newsletter

'Lengo letu ni chanjo ya haraka kwa Waafrika milioni 800'

—Benedict Okey Oramah, Rais wa Afreximbank na Mwenyekiti, Bodi ya Wadhamini wa Hazina ya Kukabili ya Umoja wa Afrika ya COVID-19.
Kingsley Ighobor
Afrika Upya: 
11 August 2021
Profesa Benedict Oramah
Benedict Okey Oramah, Rais wa Afreximbank na Mwenyekiti, Bodi ya Wadhamini wa Hazina ya Kukabili ya Umoja wa Afrika ya COVID-19.
Ikiwa huwezi kusoma sasa, sikiliza tu toleo la sauti: 
Sauti ya Kiingereza

Profesa Benedict Oramah huvaa kofia nyingi. Yeye ndiye Rais wa Benki ya Export and Import Africa (Afreximbank), Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hazina ya Umoja wa Afrika ya kukabili COVID-19 na mwanachama wa Kikosi cha Upataji Chanjo kwa Afrika (AVAT), mkakati wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) na washirika wake kuwapa Waafrika chanjo za COVID-19. Mwanzoni mwa usambazaji wa chanjo milioni 400 kwa nchi za Afrika, Kingsley Ighobor wa Afrika Upya alimhoji Prof. Okey Oramah kuhusu mahitaji ya chanjo barani Afrika na changamoto za ununuzi; na kutekeleza lengo la utengenezaji wa bidhaa za dawa barani. Hizi hapa dondoo za mahojiano hayo:Ìý

Huku Afrika ikipambana na janga la COVID-19, ni wajibu gani ambao programu fanifu ya chanjo inachakua katika kurejesha bara katika hali yake ya awali?Ìý

Kiini cha urejesho wa kiuchumi ni chanjo. Huwezi kuzungumzia urejesho bila kuchanja watu wetu. Haijalishi umeweka sera au vifaa vipi, bila kushughulikia tatizo la kimsingi, vitaharibika kwa sababu unaweza kuipatia nchi fedha leo, na kesho watafunga uchumi. Tayari, bodi yetu ya [Afreximbank] iliidhinisha dola bilioni 2 ambazo ziliiwezesha Kikosi cha Upataji Chanjo kwa Afrika [AVATT], kupitia Hazina ya Upataji Chanjo kwa Afrika, kununua dozi milioni 400 za chanjo za Johnson & Johnson.Ìý

Kama unavyojua, hata leo, huwezi kuzungumza na watengenezaji wa chanjo bila kuwa na pesa. Tulichofanya kama Afreximbank kilikuwa kuwezesha wanachama wa AU kununua chanjo kupitia AVATT. Tunaamini kuwa chanjo hizo zitasafirishwa kuanzia wiki hii.Ìý

Ndio, chanjo yenye mafanikio itasababisha urejesho baada la janga katika miezi ijayo.Ìý

Kuhusu chanjo milioni 400 ambazo umetaja muda mfupi uliopita, chanjo hizo zilinunuliwa kwa usaidizi wa Benki ya Dunia. Je, ni kweli?Ìý

Sisi [AVATT] tuliunda mfumo ambao uliwezesha wengine kuja kutuunga mkono. Unaona, mtazamo wa Benki ya Dunia ni kushughulikia kila nchi kivyake. Lakini huwezi kuiambia nchi ndogo ijadiliane na watengenezaji wa chanjo, watengenezaji hawatasikiliza. Inahusu hela.Ìý

Na kwa hiyo, kundi la AVATT liliunda mfumo kwa ununuzi wa pamoja. Tulijadili dozi milioni 400, lakini huwezi kujadili dozi milioni 400 zenye thamani ya mabilioni ya dola bila pesa na Benki ya Dunia haitahusika katika ununuzi wa pamoja. Kwa hiyo, ilitulazimu kufadhili na kulipa malipo ya mapema ya dola milioni 330. Kwa msingi huo, Benki ya Dunia ilijitolea kwa kile tulichokuwa tunataka wafanye na hiyo ni kufadhili nchi kivyake kulipia chanjo.Ìý

Kwa hivyo, ufadhili wa Benki ya Dunia, ambao ni mdogo kuliko wetu, unatumika kulipia chanjo hizo.Ìý

Chanjo milioni 400 za J&J, kuongezea kwa dozi zilizo chini ya milioni 100 zilizotolewa katika nchi za Afrika kufikia sasa, hazitatosha hata nusu ya idadi ya Waafrika. Je, mnapanga kununua chanjo zaidi?

Acha nieleze: AU ilisema, kupitia Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Afrika, kwamba ili kufikia kinga thabiti kwa jamii tunahitaji kuchanja asilimia 60 ya idadi ya watu wetu [au watu milioni 800]. Hilo ndilo lilikuwa lengo. Bila shaka, virusi aina ya Delta vimebadilisha hayo.Ìý

Mwanzoni Afrika ilitarajiwa kupokea chanjo kwa asilimia 30 ya idadi ya watu kupitia mpangilio wa . Tulijua tunapaswa kutafuta pesa kwa asilimia nyingine 30. Kwa sababu hiyo, tulinunua dozi milioni 400 kwa Waafrika milioni 400. Ikiwa COVAX itatoa chanjo kwa watu wengine milioni 400, hiyo itakuwa Waafrika milioni 800 ambao wataweza kupatiwa chanjo.

Je,Ìý COVAX inatimiza ahadi yake?

Dozi nyingi zilitakiwa kutoka India, lakini wakati fulani nchi hiyo ilipiga marufuku uuzaji wa nje na kulemaza usambazaji wa chanjo. Kwa hivyo, kumekuwa na hitilafu na matatizo mengine. Mimi sio mtaalam wa haya, lakini sasa kuna utambuzi kwamba kitu fulani lazima kifanyike haraka ili COVAX iweze kutimiza ahadi zilizotolewa, la sivyo, Afrika itaendelea kusalia nyuma kwa jambo hili.Ìý

Je, unaweka shinikizo lolote kwa COVAX kutimiza ahadi ya dozi milioni 400?

Bado tunaendelea kuweka shinikizo zaidi. Kwa kweli,Ìý tunapata majibu. Serikali ya Marekani imetoa misaada, ambayo baadhi yake inasambazwa. Serikali ya Ufaransa pia imetangaza misaada. Tunadhani kwamba kupitia juhudi hizi, pamoja na zetu, tunaweza kufikia asilimia 60 tunayozungumzia. Lazima pia nishukuru Wakfu ya Mastercard ambao umetoa, kupitia AVATT, karibu dozi milioni 67 zenye thamani ya dola milioni 500.Ìý

Baadhi ya nchi zimeshirikiana na nchi nyingine kupata chanjo. Je, munazingatia jambo hili katika mpango wenu wa usambazaji kuhusu idadi ya chanjo inayotolewa kwa nchi tofauti?Ìý

La, hatushughulikii misaada. Ni COVAX inayotoa msaada. Tunasambaza kile nchi za Afrika zinaagiza kupitia kwetu. Kabla ya kuagiza, nadhani tayari huwa wamezingatia kile walichonacho, msaada wanaopata, na mambo mengine yanayohusiana na hayo.Ìý

Je, Afrika ina uwezo wa kutengeneza bidhaa zake za dawa? Je, Afreximbank inasaidia mpango wowote katika suala hili?

Kwa nini isiwe nao? Kwa mfano, kwa chanjo za Johnson & Johnson tunazonunua, utengenezaji na ukamilisho unafanywa na kituo cha Aspen Pharmacare kilicho Afrika Kusini. Hapa Misri [makao makuu ya Afreximbank yako Cairo] Vacsera, [watengenezaji wa chanjo] wanafanya kazi kuanza kutoa chanjo. Makampuni nchini Aljeria, Nijeria, na Senegali yanatarajia kutengeneza chanjo.Ìý

Kuhusu dawa, kuna fursa nzuri kwa Afrika. Shida tuliyonayo ni upatikanaji wa masoko. Moja ya mambo tunayojaribu kubadilisha ni kupata mashirika hayo yanayofanya maagizo makubwa kugeuza mkakati wao, ili kuipatia Afrika fursa ya kuzalisha dawa.Ìý

Tumekuwa na mazungumzo mazuri sana na UNICEF kuhusu suala hili, na Afreximbank iko tayari, na najua benki zingine ziko tayari pia. Tulita saini Makubaliano na Shirika la Fedha la Afrika kushirikiana na kusaidia miradi ya utengenezaji wa chanjo barani Afrika.

Tunahitaji kuunda uwezo huu wa utengenezaji wa bidhaa za dawa kwa sababu kuna soko kwazo. Kwa hakika, sisi ndio soko. Dawa hizi zinatujia; wanunuzi wananunua bidhaa kutoka kwenye masoko mengine na kutuletea. Kwa hiyo, tunataka kubadilisha hali hii. Tumeona hatari ya kuzidi kwa uzalishaji katika maeneo machache.Ìý

Je, utekelezaji bora wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) utasaidia katika suala hili?Ìý

Kwa kweli, hiyo ni mojawapo ya sababu za kuwepo kwa AfCFTA. Soko la pamoja litaunda mifumo ya usambazaji; masoko yataanza kuunganika, na tutakuwa na uwezo wa kununua utakaowezesha uzalishaji zaidi barani.Ìý

Ikiwa watu wanaweza kununua vitu kutoka sehemu yoyote ya Afrika, utaona ongezekoÌý la mahitaji. Leo hii, soko letu limegawanyika. Hatuna habari juu ya kile kinachotokea katika maeneo mengine.Ìý

AfCFTA itasaidia kukabiliana na ukosefu huu wa habari za soko. Na tunaposhughulika nayo na kuimarisha soko, tutaanza kubadilisha simulizi kuhusu bara hili.

Je, Afrika inapataje teknolojia inayotakiwa kutengeneza dawa zake, ikizingatiwa kuwa kampuni katika nchi zilizostawi zinalinda siri za teknolojia?

Teknolojia ni suala la hakimiliki, sivyo? Maarifa ni jumuishi. Wazia miaka 35 au 40 iliyopita. Nchi ya Uchina ilikuwa mahali ilipo leo? Je, walikuwa na teknolojia miaka hiyo kama walivyonayo leo?Ìý

Lazima tutafute njia ya kukuza uhamishaji wa teknolojia, hasa kwa kitu ambacho kitaleta usalama wa afya.

Katika Afreximbank, tuna kituo cha kurahisisha kampuni za kigeni kutoa leseni ya teknolojia zao kwa wazalishaji wa Kiafrika. Tunahakikisha malipo ya mrabaha au ada ya leseni, tunahakikisha kuwa ada ya leseni itatumika kulingana na makubaliano, na tunahakikishia hakuna kitu kitapunjwa. Njia mbadala ni ile ambayo hatutaki, ya watu kuiba teknolojia. Tunataka uhamisho ulio wazi wa teknolojia.

Pia, lazima tuanze kuimarisha uwezo wa taasisi zetu za elimu ili Waafrika waweze kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maarifa ya ulimwengu na hakimiliki. Hivyo ndivyo tunafikiria mambo yanafaa kubadilika. Kwa hivyo, tunasaidia kulipia upatikanaji wa teknolojia, kusaidia kufadhili utengenezaji-hiyo ni kwa muda mfupi. Lakini baada ya muda, lazima tuwasaidie watu wetu kuunda teknolojia yao.Ìý

Mkurugenzi wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Afrika, Dkt. John Nkengasong, anataka kuundwa kwa ushirikiano. Tunaweza kuunda kwa pamoja kwa sababu tuna ujuzi wa ndani na rasilimali. Ukiangalia uhaianuwai yetu, kwa mfano, kile tulichonacho kinachosaidia kujenga sekta ya dawa ni cha kushangaza.