51³Ô¹Ï

Teknolojia ya kidijitali ni muhimu kwa usimamizi wa mali

Get monthly
e-newsletter

Teknolojia ya kidijitali ni muhimu kwa usimamizi wa mali

Teknolojia kama vile droni husaidia kukusanya picha za ardhi kwa ajili ya uchanganuzi wa picha, na katika kuweka mipaka ya viwanja.
Afrika Upya: 
17 Novemba 2021
Na: 
Washiriki wa Mkutano wa 2021 wa Sera ya Ardhi Barani Afrika.
UNECA
Mkutano wa 2021 wa Sera ya Ardhi Barani Afrika.

Teknolojia ya kidijitali inaweza kutekeleza jukumu muhimu katika kusaidia kutatua matatizo ya usimamizi wa ardhi duniani kote, hasa barani Afrika ambako mizozo inayoendelea ya ardhi.

Haya ni kulingana na wataalam wa ardhi waliotoa mawasilisho katika Kongamano la nne la Sera ya Ardhi Barani Afrika (CLPA) lililofanyika katika mji mkuu wa Rwanda Kigali, wiki iliyopita.

Katika kikao kuhusu Jukumu la Data Huru na Teknolojia ya Kigijitali katika usimamizi wa Mali katika Mataifa yanayoendelea: Mfano wa Rwanda, Fredrick Magina wa Idara ya Mipango ya Miji na Mikoa katika Chuo Kikuu cha Ardhi nchini Tanzania, alisema data huru na teknolojia ya kidijitali inaweza kusaidia kuunda usimamizi bora wa mali katika nchi zinazoendelea.

"Kushindwa katika usimamizi bora wa mali kunaweza kusababisha mizozo inayohusiana na ardhi," alisema Dkt. Magina, akiongeza kuwa nchi za Afrika zimekuwa miji kwa kasi na hivyo basi jitihada za usimamizi bora wa mali katika maeneo ya vijijini na mijini zitaendelea kuongezeka.

Kwa kurejelea utafiti uliofanywa katika wilaya ya Nyarugenge nchini Rwanda liliko jiji la Kigali, Dkt. Magina na mtafiti mwenzake David Mihio, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamifu katika Uhandisi wa Habari katika Upimaji, Uhusishaji na Muungio wa Mbali, katika Chuo Kikuu cha WuhanÌýnchini China, walisema teknolojia za kidijitali kama vile droni na Magari ya Angani yasiyo na rubani (UAVs) yamechangia pakubwa katika sekta ya ardhi.

Hasa, teknolojia husaidia kukusanya taarifa zinazohusiana na ardhi kwa njia ya upigaji picha kwa lengo la uchanganuzi bora na wazi wa picha, pamoja na kuweka mipaka ya viwanja wakati wa upimaji wa ardhi na usajili katika mfumo uliopo wa taarifa za ardhi. Pia zinatumika katika sekta nyingine kama vile ujenzi na kilimo.

Rwanda ni mojawapo ya nchi chache barani Afrika ambazo zimefanikiwa kutumia mfumo wa kidijitali wa usajili wa ardhi kwa raia wake. Usajili umekuwa ukifanywa nchini Rwanda tangu 2008 na unahifadhi rekodi zinazohusiana na umiliki wa ardhi, kipindi cha umiliki wake na sasisho za rehani zozote. Hii inasaidia katika kufanya maamuzi kuhusu umiliki wa ardhi.

Kwa hivyo Dkt. Magina alibainisha kuwa data huru na teknolojia ya kidijitali katika usimamizi wa mali ni muhimu kwa maendeleo ya vijijini na mijini ya nchi kwa kuwa inasaidia kupata umiliki wa ardhi wa muda mrefu, na kukuza utulivu kati ya watu wanaoishi katika jamii. Anaongeza kuwa pia imesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha umiliki wa ardhi kwa wanawake.

Changamoto

Miongoni mwa changamoto katika kusimamia mali, kwa mujibu wa utafiti huo, ni uhaba wa fedha, ukosefu wa wataalamu wa teknolojia zinazoibuka na ukosefu wa uwezeshaji wa jamii. Suala hili linahitaji mafunzo zaidi, miongoni mwa juhudi nyingine.

Kwa misingi ya utafiti huo, Dkt. Magina anapendekeza matumizi ya teknolojia zinazoibukia za kidijitali kukusanya na kuhifadhi data ya mali kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya siku zijazo na kwa mipangilio mizuri ya miji; uwezeshaji wa jamii katika masuala ya ujuzi wa teknolojia ya kusimamia matumizi ya teknolojia mpya; na kuanzisha mifumo ya data inayohusiana na ardhi kwa uwazi.Ìý

Katika ufunguzi wa mkutano wa CLPA, Waziri wa Mazingira wa Rwanda, Jeanne D'Arc Mujawamariya, alitoa wito kwa nchi za Afrika kuendeleza sera za ardhi zinazopendelea maskini na haki za umiliki wa ardhi, hasa kwa wanawake na vijana.

"Tunahitaji kujitolea katika ngazi za nchi na kanda ili kuhakikisha usawa," Bw. Mujawamariya alisema, akiongeza kuwa jambo lolote linalohusiana na masuala ya ardhi linahitaji nia njema ya kisiasa, uungwaji mkono na watu, na ushirikiano wa karibu.

Waziri huyo alieleza jinsi mabadiliko ya hali ya hewa yalivyoongeza hatari ya ukataji miti na uharibifu wa ardhi na kutaka kuwepo kwa ubunifu katika utekelezaji wa mageuzi na huduma za ardhi.

Kongamano hilo huandaliwa kila baada ya miaka miwili na Kituo cha Sera ya Ardhi cha Afrika,Ìýmkakati wa pamoja wa Tume ya Kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Afrika (ECA), Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Mada ya mwaka huu ilikuwa:Ìý"Utawala wa ardhi kwa ajili ya kulinda sanaa, utamaduni na urithi kuelekea Afrika Tunayoitaka".Ìý

Mada ya Kongamano hili inalingana na mada ya Umoja wa Afrika ya 2021, "Sanaa, Utamaduni na Urithi: Nguzo za Kujenga Afrika Tunayoitaka.'' Kongamano hili lilenga turathi za Kiafrika na vipimo vya kiasili vya ardhi na uwezekano wa kulinda njia za kutafuta riziki, ukuaji wa uchumi, na maendeleo endelevu kupitia uchumi wa ubunifu katika mazingira ya vijijini na mijini.Ìý

Mada: