Katibu wa Umoja wa Mataifa Zainab Hawa Bangura ni Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Nairobi (UNON), wadhifa ambao ameushikilia tangu tarehe 30 Desemba 2019. Kabla ya kutwazwa kwake, alikuwa Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Unyanyasaji wa Kijinsia katika Migogoro. Katika mahojiano haya na Kingsley Ighobor wa AfrikaUpya, Bi Bangura anajadili uwezeshwaji wa kijinsia na vijana, mkakati wa Umoja wa Afrika wa "Kukomesha vita ifikapo 2020", miongoni mwa masuala mengine. Hizi hapa dondoo.
Acha tuanze kwa suala nzito—COVID-19. Kwa kuzingatia hali ya sasa ya janga barani Afrika, una ujumbe gani kwa Waafrika wakati huu?
Ujumbe wangu ni kwamba Afrika inaweza kushinda virusi hivi, kupona na kuwa bora zaidi. Waafrika huwa imara. Hata hivyo, vifo ni vingi, njia zetu za maisha zimevurugwa na kuna uharibifu mkubwa wa uchumi.
Ripoti nyingi zilizotolewa hadi sasa, pamoja na sera ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu athari ya COVID-19 barani Afrika, zinaonyesha kwamba makumi ya maelfu ya maisha ya watu yanaweza kupotea pamoja na mabilioni ya dola ya shughuli za kiuchumi. Katibu Mkuu ametoa wito wa kusimamisha deni na kutolewa kwa msaada wa dola bilioni 200 kusaidia nchi maskini kukuza uchumi wao. Ninaamini pia kuwa kipindi cha baada ya janga hili ni fursa ya Afrika kupona kwa njia bora.
Kwa hivyo, lazima tuzingatie miradi endelevu ya maendeleo, yakiwemo yanayolinda mazingira, na tumakinike zaidi kwa uwezeshaji wa wanawake, vijana na watu walioko hatarini.
Kama Mkurugenzi Mkuu wa UNON, maeneo yako ya kipaumbele ni yapi?
Kama unavyojua, kabla ya kutwazwa kwangu UNON haikuwa na kiongozi kwa zaidi ya mwaka mmoja, kwa hivyo kazi yangu ya kwanza ilikuwa kusawazisha vitengo na idara ili ziwe kitengo kimoja kinachoruhusu mikakati ya pamoja kufikia malengo ya shirika.
Pili, tunaendeleza kazi za Makatibu wa awali ili kuwezesha kutambuliwa kwa UNON, ambayo ni makao makuu ya Umoja wa Mataifa barani Afrika. Utambuzi kama huu bila shaka utavutia vyombo vya habari, makongamano ya kimataifa na matukio mengine. Tunayo maono wazi na tumeweka vipaumbele ikiwa ni pamoja na kusaidia kutekeleza mikakati ya Katibu Mkuku ya mageuzi ya shirika. Pia inajumuisha kuhamasisha umma kuhusu kazi ya Umoja wa Mataifa nchini Kenya na Afrika Mashariki, kusaidia taasisi nyingine za Umoja wa Mataifa na kuimarisha ushirikiano na mashirika mengine ya kikanda.
Kama Mkurugenzi Mkuu, nipo pia kusaidia kuendeleza ofisi nzuri za Katibu Mkuu katika kanda hii na diplomasia ya kuzuia, ambayo ni kupatanisha watu kabla ya mizozo kutokea.
Je, tajriba yako ya awali na kazi katika Umoja wa Mataifa imekuandaa vipi kwa kazi yako ya sasa?
Nilikuwa mwanaharakati katika asasi za kiraia na nilikuwa waziri wa serikali katika nchi yangu Sierra Leone [Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kisha Waziri wa Afya].
Nilikuwa pia nimefanya kazi na Umoja wa Mataifa katika kulinda amani na baadaye kama Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Unyanyasaji wa Kijinsia katika Migogoro. Tajriba hii inathibitisha zaidi mapenzi yangu na kujitolea kwangu kwa masuala ya wanawake, utawala bora na maendeleo endelevu. Kwa wanawake haswa, hatuwezi kupiga hatua yoyote katika masuala ya haki za binadamu, amani na usalama na maendeleo, bila michango yao.
Najikumbusha na kuwakumbusha wenzangu kila wakati kwamba vipaumbele vyetu na kazi yetu lazima zizingatie kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambao kwa msingi wake unazingatia watu, sio tu michakato mingine ya bure, isiyo ya watu.
Je, kuwa na makao makuu ya Umoja wa Mataifa barani Afrika kuna umuhimu gani wa kimkakati?
Huduma ambazo Umoja wa Mataifa hutoa katika masuala ya amani, usalama, miitikio ya kibinadamu, haki za binadamu na maendeleo zinaletwa karibu na wale wanaofaidika ambao wengi wanaishi barani Afrika.
UNON ni makao ya kipekee kwa maana kwamba ina mchanganyiko wa makao makuu ya kidunia, ofisi za nchi na kanda, Misheni Maalum ya Siasa na shughuli za kusaidia amani. Ni makao makuu ya Umoja wa Mataifa barani Afrika na pia makao makuu ya ulimwengu kwa Shirika la Makazi na Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa. Kazi za Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyoko Nairobi huchangia sana katika kuendeleza malengo na maadili ya Umoja wa Mataifa—nchini Kenya, katika kanda na kote duniani.
Moja ya vipaumbele vya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ni usawa wa kijinsia katika mfumo wa Umoja wa Mataifa. Je, unatarajia kufikia lengo hili namna gani UNON?
Tunayo hati ya sera ya kijinsia ambayo imesambazwa sana miongoni mwa wafanyakazi kwa hivyo kila mtu anaelewa kanuni hizi. Wasimamizi wakuu hupata mafunzo kila mara, yakijumuisha yale yanayotolewa na UN Women, kuhusu kushughulika na upendeleo usiokusudiwa katika kuajiri wafanyakazi. Wasimamizi wa juu zaidi pia wameombwa kujumuisha katika mipango yao ya kazi wanayotarajia kutekeleza kufanikisha usawa wa kijinsia. Utafiti umeonyesha kuwa kueleza tajriba ya miaka kadhaa kama "inavyotakikana" badala ya "inavyohitajika" katika fursa za kazi ni mwaliko zaidi kwa wanawake.
Isitoshe, fursa zetu za kazi zinaandikwa kwa lugha inayohimiza sana wanawake kuomba kazi hizo. Tunajaribu pia kuwahimiza wanawake waliohitimu na kuendeleza hatua za kupanda cheo ambazo zinasaidia maamuzi ya wanawake kuja Nairobi. Kwa hivyo, kuhusu masuala ya kijinsia, tunapiga hatua kwa njia nyingi.
Kama mwanaharakati wa zamani wa asasi za kiraia, unaonaje wajibu wa wanawake katika maendeleo ya Afrika?
Kama nilivyotaja hapo awali, wanawake wana wajibu muhimu sana, wa kutekeleza katika maendeleo ya nchi. Wakati wanawake hawapo kwenye meza ya mazungumzo, kunakuwa na ubishi mwingi. Lakini wakati wanawake wanakuwepo, nafasi za makubaliano ni kubwa. Na tukumbuke wajibu wa wanawake katika ajenda za kimataifa.
Katibu Mkuu [António Guterres] alisema wakati wa uzinduzi wa kitabu “She Stands for Peace” mnamo Februari kuwa utetezi wa walinda amani wanawake, haswa barani Afrika, ulisaidia kuzidisha kasi miaka 20 na kuishia kwenye Azimio la Baraza la Usalama 1325 kuhusu Wanawake, Amani na Usalama (WPS).
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa wanawake kutambuliwa sio tu kama waathirika wa vita lakini pia kama watu walio na utaalamu ambao wanaweza kusaidia kupata suluhisho la amani katika migogoro.Tangu wakati huo, kumekuwa na maazimio mengine tisa ya Baraza la Usalama kuhusu WPS, pamoja na sheria za Umoja wa Afrika. Usawa wa kijinsia, kama tunavyojua, ni suala wa mamlaka.
Ni muhimu sana kwamba wanawake zaidi wako katika nafasi za uwajibikaji, katika sekta za umma na za kibinafsi, ili kufungua uwezo kubwa wa kijamii na kiuchumi ambao utasababisha maendeleo ya Afrika.
Umoja wa Mataifa unaunga mkono kampeni ya Umoja wa Afrika ya kukomesha vita kufikia 2020. Kwa kuzingatia tajriba yako kutoka nchi iliyoshuhudia migogoro, unafikiria ni kwa nini vita lazima vikome barani Afrika?
Hakuwezi kuwa na maendeleo bila amani na usalama, ndiyo sababu Umoja wa Afrika ulizindua mkakati wa "Kukomesha Vita ifikapo 2020". Kwa hakika, hatua kubwa zimefikiwa katika kukomesha vita katika sehemu nyingi barani Afrika, lakini wakati huohuo tumeshuhudia jinsi kazi hiyo ilivyo ngumu kwa sababu bado tunayo migogoro mingi tata.
Umoja wa Mataifa unaunga mkono mkakati wa Umoja wa Afrika—kuna juhudi za pamoja zinazoendelea kati ya Umoja wa Mataifa na Muundo wa Amani na Usalama wa Afrika wa Umoja wa Afrika ili kuimarisha uwezo wa kuzuia migogoro ya nchi wanachama.
Ili kumomesha vita kabisa kutahitaji kushughulikia sababu za migogoro na haya yanajumuisha masuala kama kuongezeka kwa silaha barani, athari za mabadiliko ya tabianchi, usimamizi mbovu wa mali asili za nchi, ukosefu wa usawa wa kijamii na kiuchumi na masuala mengine ya utawala kama kutengwa kwa wanawake na vijana katika mchakato wa uchaguzi.
Je, vijana wanaweza kutekeleza wajibu gani katika kuimarisha amani na maendeleo ya Afrika?
Nitarudia kile Katibu Mkuu alichosema mwaka jana katika Mkutano wa Umoja wa Afrika, ambacho ni kwamba vijana wa Afrika wanahitaji kuhusishwa na kuwezeshwa kwa sababu ndio mawakala wa mageuzi. Hatuwezi kufikia maendeleo endelevu bila kushirikiana na vijana. Ninaamini sana, kwamba vijana wana wajibu muhimu kutekeleza katika kufikia amani, usalama, utulivu na utawala bora barani Afrika. Tunahitaji mawazo na nguvu yao. Tumeona kile vijana wanaweza kufanya katika, kwa mfano, matumizi ya teknolojia kutatua matatizo. Uwezo wao wa kuhamasisha k wa kutumia teknolojia, kuimarisha uhamasishaji miongoni mwa watu wengi kuhusu masuala muhimu ya kijamii, ni ajabu.
Mataifa mengi ya Afrika ni ya mapato ya chini na dhaifu, na kuna vitisho vinavyoendelea kwa amani na usalama, ikiwemo migogoro ya kikabila. Kwa hivyo, lazima pia tugundue kuwa vikundi vingi ambavyo vinataka kuchochea shida katika nchi huanza kwa kuwasajilisha vijana. Mataifa na taasisi zinazozingatia maendeleo kama Benki ya Maendeleo ya Afrika na Benki ya Dunia kwa hivyo lazima ziwekeze kwa vijana katika suala la elimu bora na kuwapa ujuzi.
Lazima tugundue haja ya kuunda mazingira ya kiuchumi yanayowezesha, yakiwemo kutoa fursa za ajira na huduma kama vile nishati, huduma ya afya, miundombinu ya kisasa ya uchukuzi ambayo vijana wanahitaji kustawi. Bora ni kuwa, mkakati wa Umoja wa Afrika wa kukomesha vita unazingatia zaidi vijana. Nina imani katika uwezo wa vijana wa Afrika kubadilisha simulizi ya maendeleo ya bara hili.