Katika tukio anzilishi, wanawake katika Wilaya ya Bugiri, Mashariki mwa Uganda, wamekiuka kanuni za kijamii na kuingia katika tasnia ya ufugaji samaki iliyotawaliwa na wanaume.
Kupitia Mpango wa Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi uliozinduliwa na UN Women, wanawake hawa hawajabobea tu katika sanaa ya uvuvi, lakini pia wameleta mapinduzi makubwa katika ustawi wao kiuchumi.
Rose Nakimuli, mkazi wa Bugiri, anakumbuka vyema safari yake katika ufugaji samaki.
"Nilipochaguliwa kupata mafundisho ya ufugaji samaki, niliikumbatia fursa hiyo. Niliichukulia kama ajira," Bi. Nakimuli anasema kwa dhamira.
Kwa msaada wa mradi wa UN Women, alijifunza mambo mengi kuhusu ufugaji samaki, kuogelea, na uvuvi, na kuwa mfugaji mjuzi wa samaki. Leo, yeye huilisha familia yake kwa fahari na kujipatia riziki nzuri kutokana na utaalamu wake mpya.
Bi Nakimuli ni mmoja wa wanawake 1,400 waliopewa mafunzo ya ufugaji samaki.
Mpango huu ulioanzishwa mwaka wa 2019, umeweka malengo kabambe ya kuimarisha usalama wa kipato cha wanawake, kukuza kazi zenye staha, na kuwawezesha kujitegemea kiuchumi ifikapo 2025. Mafanikio yaliyopatikana katika tasnia ya ufugaji samaki katika Wilaya ya Bugiri ni kielelezo cha athari za mpango huo.
Kwa ufadhili wa Serikali ya Sweden na Benki ya Standard, UN Women ilishirikiana na Serikali ya Wilaya ya Bugiri kuwasaidia wanawake wa vijijini kushiriki shughuli za ufugaji samaki kwenye maji ya Ziwa Victoria.
Kama matokeo, vizimba 28 vilivyojaa samaki wa ana ya tilapia sasa vinasimama kama ushahidi wa kujitolea na dhamira isiyoyumba ya wanawake.
Amina Nakiranda, meneja wa uzalishaji wa mradi huo, anaeleza kuwa ulikwenda zaidi ya kuwafundisha wanawake jinsi ya kuvua samaki kwani mpango huo pia uliwapa ujuzi muhimu wa usimamizi wa biashara.
"Kabla ya mpango huu, wengi wetu tulihangaika na biashara ndogondogo za kuuza mboga na matunda au samaki wa fedha katika masoko ya mitaani," Bi. Nakiranda anafichua.
"Hata hivyo, kupitia mafunzo ya kina yaliyotolewa na mradi huu, tulijifunza jinsi ya kuendesha biashara zetu kwa ufanisi, kuanzia mwanzo hadi mwisho."
Mradi huo wa vizimba vya samaki umeimarisha uwezo wa wanawake katika utawala, ujuzi wa kifedha, na mkondo mzima wa thamani ya samaki. Huku wakihamasishwa na mafanikio yao, wanawake hawa walianzisha kampuni ya kibinafsi iitwayo "Women Economic Empowerment Bugiri (WEEB)."
Immaculate Were, Mkurugenzi Mtendaji wa WEEB, anaangazia kwa fahari safari ya kimapinduzi ya wanawake hawa. “Ingawaje asilimia 85 ya wanufaika hawajui kusoma na kuandika, wamekuwa wataalam katika masuala mbalimbali ya ufugaji samaki, ikiwa ni pamoja na ulishaji, uvunaji, uhifadhi, uuzaji na biashara,” asema Bi. Were, huku akiongeza kwamba, “Pindi mwanamke apatapo utajiri, huo ni utajiri kwa taifa zima.”
Mradi huo pia umepiga hatua kubwa katika kuboresha mahusiano ya kijinsia katika ngazi ya familia. Huku wanawake wakichangia katika bajeti ya familia na kupata uhuru wa kifedha, dhuluma za kijinsia zimepungua pakubwa.
Judith, mjumbe wa bodi kuu ya WEEB, anaelezea tajriba yake: “Mradi huu umepunguza dhuluma za kijinsia kwa sababu hatuketi tena nyumbani na kuwaomba waume zetu kila kitu. Sisi si mizigo tena; mradi umetuwezesha.”
Zaidi ya habari za mafanikio ya mtu binafsi, mradi wa ufugaji samaki umetoa mchango mkubwa katika Pato la Kitaifa. Kwa uzalishaji wa kuvutia wa tani 508.5 za samaki, wanawake hawa wamezalisha mauzo yenye thamani ya bilioni 4.3 za UGX (takriban dola milioni 1.15).
Athari za mradi huo zinaenea zaidi, huku UN Women ikitoa msaada muhimu, ikiwa ni pamoja na malazi kwa wanawake wanaofanya kazi, huduma za kulea watoto wao mchana, na rasilimali muhimu kama vile malazi, nyavu za samaki, jaketi za uokozi, na lori la jokofu kwa ufikiaji rahisi katika soko.
"Kwa sababu ya UN Women, leo tunajisikia kama mashujaa," Bi. Nakimuli anaongeza. "Hata wanaume wanatuona kama mashujaa, kwa sababu uvuvi ulikuwa kazi ya wanaume na tunaumudu vyema. Pia hutupa mapato ya kuzikimu famila zetu."
Safari ya wanawake hawa wastahimilivu hutumika kama msukumo, huku ikithibitisha kwamba kwa msaada na dhamira kuu, vikwazo vinaweza kusambaratika, na upeo mpya unaweza kuangaziwa.