Licha ya juhudi za washikadau kuleta amani barani Afrika, mizozo inayoendelezwa kwa silaha bado inaendelea katika maeneo mbalimbali ya bara hili. Hali ya mizozo ya vurugu ni tofauti na ile ya kabla ya uhuru ambayo aghalabu iliongozwa na itikadi na mielekeo ya wapiganaji. Mizozo mingi ya sasa inaongozwa na tamaa ya mamlaka ya kisiasa au mapato ya kifedha, huku vikundi vilivyojihami vikipigana kumiliki raslimali za madini yenye thamani, kulazimisha itikadi zao au kueleza malalamishi yao.
Umoja wa Afrika katika juhudi zake za “Kuzima Bunduki barani Afrika kufikia 2020” (ambayo ndiyo kaulimbiu yake mwaka huu) pamoja na washirika wengine wanastahili kutilia maanani maeneo yenye migogoro sasa: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Somalia, Sudan Kusini, Nijeria, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na Libya, ambako makumi ya maelfu ya watu wameuliwa na wengine mamilioni kulazimika kuhama makwao.
Haya ndiyo maeneo hatari ya Afrika:
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Vita katika DRC ni moja kati ya vile hatari zaidi barani Afrika. Zaidi ya watu milioni tano wameuliwa katika vita vya Kongo, kulingana shirika la habari la Reuters. Vilianza mnamo 1998 kwa uhusika wa takribani vikundi 20 tofauti vilivyojihami na vinavyozunguka misitu mipana ya taifa hilo. Vikundi hivi vinakabiliana, ilhali vingine kutoka mataifa jirani vinatumia nchi hii kuanzisha mashabulizi kwa mataifa yavyo. Vingine vinatumia raslimali za madini za taifa hili, ikiwa ni pamoja na dhahabu, platini na koltani na kuendeleza zaidi mizozo iliyopo.
Miongoni mwa vikundi hivyo vilivyojihami ni pamoja na Democratic Forces for the Liberation of Rwanda; Allied Democratic Forces, kikundi cha waasi kutoka Uganda kilicho katika Mlima Ruwenzori, mashariki mwa Kongo, Lord’s Resistance Army, kikundi kingine cha waasi kutoka Uganda kilichoko katika mpaka wa kaskazini; National Forces of Liberation, kikundi cha waasi wa Burundi kinachofanyia shughuli zake Kusini mwa Kivu; na wanamgambo wa Mai-Mai walioko Kivu.
Katika miezi sita ya kwanza ya 2019, takribani watu 732,000 walisemwa walilazimika kuhama kwao. Kati yao, 718,000 walihama kutokana na mizozo ilhali 14,000 wakihama kutokana na majanga.
Sudan Kusini
Baada ya vita hatari vya wenyewe kwa wenyewe vilivyohusishwa na athari za ukoloni wa Mwingereza, Sudan Kusini ilitangaza kuwa huru kutoka kwa Sudan mnamo 2011. Hata hivyo, taharuki iliendelea kutokana na raslimali asilia, haswa viwanja vya mafuta katika Sudan Kusini. Hali imeharibiwa zaidi na uhasama kati ya mgao mmoja wa vuguvugu la Sudan People’s Liberation Movement linaloongozwa na Rais Salva Kiir, na mgao wa pili ulio katika upinzani unaoongozwa na aliyekuwa naibu wa Bw. Kiir, Riek Machar.
Tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipozuka Sudan Kusini mnamo 2013, takriban watu 380,000 wameripotiwa kuuliwa na zaidi ya milioni mbili kushurutika kutoroka makwao. Mkataba wa Amani wa 2015 ulivunjika baada ya vita kati ya waasi na vikosi vya serikali kuzuka. Mkataba mpya ‘ulioimarishwa’ ulitiwa sahihi mwaka 2018, hata hivyo kasi yake ni ya polepole. Makataa ya pili ya kuunda serikali ya muungano yamepita huku Machar akieleza wasiwasi wake kuhusu masuala fulani ambayo hayajasuluhishwa.
Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR)
Kumekuwa na mizozo katika CAR kwa zaidi ya miaka sita. Mizozo hiyo ilianzishwa awali na upinzani uliojihami wa Séléka kujitoma katika jiji kuu la Bangui mnamo Machi 2013 kumpinga aliyekuwa Rais, François Bozizé na ukafaulu kunyakua udhibiti wa taifa hilo.
Hali ya usalama ilizorota zaidi mwezi wa Disemba vita vilipozuka kati ya makundi mbalimbali yaliyojihami. Vita hivyo vinaendelea na vimekuwa changamano zaidi kutokana na kusambaratika kwa muungano na kuunda kwa miungano mingine.
Manamo Februari 2014, serikali na vikundi 14 vilivyojihami vilitia sahihi Mkataba wa Amani ambao umepunguza makabiliano ya moja kwa moja. Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na wengine wanashirikiana kuunga mkono mkataba huo ili kumaliza vurugu dhidi ya raia, kuimarisha upanuzi wa mamlaka ya serikali na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika taifa hilo.
Libya
Mzozo unaoendelea Libya ulianza mwaka wa 2011 baada ya kuporomoka kwa utawala wa Muammar Gaddafi, Mgogoro huo unahusu udhibiti wa nchi na viwanja vya mafuta haswa.
Vita vimekuwa kati ya Baraza la Wawakilishi lililoanza kazi kirasmi mnamo 2014 na linalodhibiti maeneo ya mashariki na kusini mwa Libya na wapinzani wake Bunge la Kitaifa (GNC) lililoko Tripoli. Mwezi wa Disemba 2015, makundi haya hasimu yalitia sahihi Mkataba wa Makubaliano ya Kisiasa wa Libya (LPA), yakiahidi kuunga mkono Serikali ya Muungano wa Kitaifa (GNA). Hata hivyo, GNA, ambayo inatambuliwa na Umoja wa Mataifa, inaendelea kukabiliwa na upinzani kutoka ndani ya Bunge la Kitaifa na Baraza la Wawakiishi.
Mnanmo Aprili 2019, Khalifa Haftar, kiongozi wa kikundi kinachojiita Libyan National Army, ambacho kinadhibiti sehemu kubwa ya mashambani, alishambulia Tripoli. Takriban watu 1,000 waliripotiwa kuuliwa katika shambulio hilo na zaidi ya watu 128,000 kulazimika kuhama kwao tangu awamu ya hivi karibuni ya mzozo ilioanza Aprili. Marufuku iliyowekwa kwa silaha na Umoja wa Mataifa inaendelea kukiukwa huku pande mbili husika zikitegemea msaada wa kimataifa kwa silaha.
Nijeria
Uasi wa Boko Haram ulioanza Nijeria mnamo 2009 umeenea hadi kwa mataifa jirani, kama vile Cameroon, Chad na Nijeri. Lengo la awali la kikundi hiki cha jihadi lilikuwa kukabili kile kilichoonekana kama ukengeushwaji wa utamaduni wa Nijeria na ule wa kigeni. Kikundi hicho kiliahidi utiifu kwa Islamic State of Iraq na Levant au ISIS na kulipa shirika lake sura mpya kama Taifa la Kiislamu kwenye kanda la Afrika Magharibi (Islamic State in West Africa).
Zaidi ya watu 30,000 wameuliwa katika mzozo wa muda mrefu kati ya serikali ya Nijeria na Boko Haram. Takriban watu milioni mbili wametoroka nyumbani kwao na wengine 22,000 hawajulikani waliko, wanaaminika kuwa wamelazimishwa kusajiliwa katika jeshi la Boko Haram. Mnamo Aprili 2014, kundi hili liliwateka nyara wasichana 276 kutoka shule moja katika kijiji cha Chibok, jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nijeria. Wachache walifaulu kutoroka au kuokolewa. Zaidi ya wasichana 112 hawajulikani waliko.
Mali
Mwaka wa 2012, waasi waliojitenga kutoka kwa National Movement for Liberation of Azawa (MZLA) wa Tuareg walitwaa eneo la kaskazini ya Mali. Kabla ya hili, idadi kubwa ya waasi wa Tuareg walikuwa wameingia Libya kujiunga na jeshi la kivita la Muammar Gaddafi. Walirejea na silaha bora zaidi kujiunga na shambulio la 2012 la kaskazini ya Mali baada ya kuporomoka kwa serikali ya Gaddafi.
Tangu wakati huo vikundi vingine vilivyojihami viliibuka au vikachomoza kutoka kwa vilivyokuwepo vikiwa na nia ya kujitawala na malalamishi ya kisiasa pamoja na ya kijamii na kiuchumi. Serikali ya Mali na miungano miwili ya vikundi hivi viwili - Plateforme na Coordination – ilitia sahihi mkataba kuhusu amani na Maridhiano nchini Mali Mei 2015. Hata hivyo, mapigano yanaendelea huku vikundi vya kiislamu vilivyojihami vikishambulia raia, mipango ya serikali ya kuukabili ukaidi, na kusababisha rabsha katika jamii.
Somalia
Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia vilianza mwaka wa 1991 wakati serikali ya Rais Siad Barre ilipopinduliwa. Vikundi vilivyojihami vilianza kupigania mamlaka. Somali iligeuka na kuwa taifa lililofeli kwa kukosa utawala madhubuti. Mabwana kinzani wa kivita na vikundi mbalimbali vilidhibiti sehemu tofautitofauti za jiji kuu Mogadishu na maeneo mengine ya kusini mwa Somalia.
Kikundi cha wanamgambo cha AL-Shabaab kilichipuka kama tawi la Muungano wa Mahakama za Uislamu (Islamic Court) ambao ulidhibiti Mogadishu mnamo 2006, wakati serikali ya mpito ikiwa ukimbizoni nchini Kenya. Majeshi ya Uhabeshi yaling’oa muungano huo na kutoa nafasi kwa serikali iliyokuwa ukimbizoni kurejea nyumbani. Al-Shabaab waliishambulia serikali, na kusababisha haja ya kuyapeleka majeshi ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) mwaka wa 2007.
Serikali mpya ya majimbo iliundwa mwaka wa 2012. Mwaka huo, Al-Shabaab ilitangaza utiifu kwa Al-Qaeda. Vita kati ya vikundi haramu vilivyojihami na majeshi ya serikali vimesababisha vifo vya maelfu ya raia na kuhama kwa watu zaidi ya milioni mbili kutoka kwao. Licha ya ufanisi dhidi ya kundi hili, waasi wa Al-Shabaab wanaendelea kufanya mashambulizi ya kutisha dhidi ya raia na serikali.