Ofisi ya Mshauri Maalum Kuhusu Afrika (OSAA) iliundwa mwaka wa 2003 kuimarisha usaidizi wa kimataifa kwa maendeleo na usalama wa bara Afrika kupitia kazi zake za utetezi na uchanganuzi, na kumsaidia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuboresha upatanifu na ushirikiano wa mfumo wa usaidizi wa Umoja wa Mataifa kwa Afrika. Bi. Bience Gawanas aliteuliwa Msaidizi wa Katibu Mkuu na mshauri maalum kuhusu Afrika mwaka jana. Alizungumza na Zipporah Musau wa AfrikaUpya kujadili jukumu lake na mambo anayoyapa kipaumbele mwaka 2020. Hizi hapa sehemu za mazungumzo hayo:
Jukumu lako kama mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Afrika ni lipi?
Najiona kama sauti ya Afrika katika Umoja wa Mataifa. Ofisi yangu, ofisi ya Mshauri Maalum kuhusu Afrika, humsaidia Katibu Mkuu kuleta upatanifu mkuu kupitia kwa msaada wa Umoja wa Mataifa kwa maendeleo ya Afrika. Tunasaidia pia mpango wa Ushirikiano Mpya kwa Maendeleo ya Afrika (NEPAD), ambao unageuzwa kuwa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika (AUDA).
Kwa maoni yako, ni changamoto zipi tatu kuu zinakabili Afrika leo?
Ninastahabu kuzungumza kuhusu nafasi katika bara la Afrika. Ninapenda kufanya usimulizi chanya kuhusu Afrika. Hata hivyo, tunajua kwamba bado tunakabiliwa na changamoto za mizozo, magonjwa, umaskini na njaa. Hii ndiyo sababu ni lazima tutekeleze mpango wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na Ajenda 2063 ya Afrika (ruwaza na mpango kabambe wa Umoja wa Afrika kugeuza Afrika).
Ni nafasi zipi tatu kuu unazoziona katika bara hili mwaka wa 2020?
Kuna nafasi kadhaa zinazoweza kuiweka Afrika katika njia tofauti. Kwangu mimi nafasi kuu zaidi sasa ni Mpango wa Bara Afrika wa Biashara Huru (the African Continental Free Trade Area) (AfCFTA) iliyotekelezwa miezi michche iiyopita. Afrika ina uwezo wa kuwa moja kati ya masoko makuu kabisa ulimwenguni. Ila tunahitaji kushirikiana wenyewe kibiashara kama Waafrika.
Nafasi ya pili ni mpango wa “Kuzima Bunduki”, moja kati ya miradi muhimu ya Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika. Kaulimbiu ya 2020 ya Umoja wa Afrika itakuwa “Kuzima Bunduki,” na kutakuwa na juhudi mpya kwa kampeni za kuongeza kasi ya mpango huo.
Nafasi nyingine kulingana nami ni mbadiliko ya tabianchi. Kwa mara ya kwanza watu wengi zaidi wanajihusisha na kujadili mabadiliko ya tabianchi kuliko walivyowahi kufanya awali.
Kama mshauri kuhusu Afrika, ni mambo yapi matatu unayoyapa kipaumbele?
Niliteuliwa katika ofisi mwaka mmoja uliopita wakati Umoja wa Mataifa ulikuwa unapitia mageuzi makubwa katika nguzo ya amani na usalama, nguzo ya maendeleo, na usimamizi. Aidha Umoja wa Afrika ulikuwa unapitia mageuzi ya kitaasisi. Ni bayana kwamba tulistahili kujipa sura mpya. Jambo ninalolipa kipaumbele ni kuhakikisha kuwa ofisi hii inasalia muhimu, faafu, stadi na yenye mguso katika dhima na majukumu yetu. Mimi ni mwanamke wa kwanza katika nafasi ya mshauri maalum kuhusu Afrika, ninajiona kama mwanzilishi katika mfumo wa Umoja wa Mataifa, kwa hivyo ninastahili kuyapa mahitaji ya wanawake na watoto kipaumbele.Ěý
Utaipa mipango ipi kipaumbele mwaka wa 2020?
Tunaongozwa zaidi na mambo ambayo bara la Afrika linayapa kipaumbele, ushirikiano kati ya hizo ajenda mbili—Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika na Ajenda ya kimataifa ya 2030. Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa zimetia sahihi mikataba miwili ya kimfumo: kuhusu ushirikiano katika amani na usalama pamoja na katika ushirikiano katika kutekeleza hizo ajenda mbili. Hayo mawili yatasalia kupewa kipaumbele kwetu sisi.
Aidha tutatangaza mambo yanayofanywa na mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika, hiyo ndiyo sababu Mfululizo wa Mazungumzo ya Afrika mwezi wa Mei umesalia ukumbi muhimu kwetu. Kwa mfano, mwaka huu, kaulimbiu ya Umoja wa Afrika ilikuwaĚý “Kuelekea kwa Masuluhisho ya Kudumu kwa Watu Waliohamishwa kwao kwa Lazima barani Afrika” na kwa kuitilia mkazo wakati wa Mfululizo wa Mazungumzo ya Afrika, ni dhahiri tuliiweka katika ajenda ya Umoja wa Mataifa. Hiyo ndiyo sababu mwaka huu kulikuwa na majadiliano kadhaa kuihusu mada hii katika Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na katika Baraza la Usalama na kwingineko. Tunatumai kupata ufanisi kama huo katika kaulimbiu ya “Kuzima Bunduki” mwaka wa 2020.
Unahisi vipi kuwa mwanamke Mwafrika kiongozi katika kiwango cha kimataifa?
Nina bahati kubwa sana. Mara nyingi ninakumbuka, nilipokuwa mwanamke mchanga, nilipokuwa katika mstari wa kwanza kupigania uhuru wa Namibia. Ninajiambia kwamba kama tuliweza kupigania uhuru, kwa hakika tunaweza kuongoza. Hili halijawahi kuwa tatizo kwangu kwa kuwa niliihudumia nchi yangu katika nafasi nyingi kama mwanamke wa kwanza. Nilitoka Namibia hadi kwa kiwango cha bara, ambako nilihudumu kama kamishina wa kwanza mwanamke katika Tume ya Umoja wa Afrika. Sasa niko hapa katika kiwango cha kimataifa. Kwa hakika ni heshima kuu.
Je, kuna matatizo yoyote?
Changamoto zinazowakabili wanawake zinafanana kote wanapoingia katika mifumo iliyotawaliwa na wanaume na isiyowahi kuwa na wanawake. Tunahitaji kubuni mwanzo mpya na kuanza usimulizi mpya ambao unatuzingatia sisi kama wanawake. Nimesema mara nyingi kuwa dhana kwamba wanawake wamo katika nafasi za uongozi haiwageuzi kuwa wanaume. Ninaleta sifa na mitazamo yangu kama mwanamke kuboresha eneo la kazi. Tunastahili kuwa razini kila wakati. Ninawaambia wanawake wasiiangushe ngazi pindi wapandapo juu. Ishikilie ngazi hiyo ili wanawake wengine waipande kama ulivyofanya. Ěý
Ni jukumu lipi linaloweza kutekelezwa na wanawake barani Afrika ili kuchangia kuwepo kwa bara bora kwa wote?
Tunastahili kuuliza jukumu ambalo wanawake wanatekeleza tayari na walilotekeleza awali. Kwa hakika hatungekuwa hapa bila mchango wa wanawake. Je, ni kitu gani ambacho wanawake wanatakia Afrika? Tunataka ulimwengu unaomtambua kila mmoja kama binadamu kwanza. Ninaamini kwamba tunapouliza maswali sahihi na kuchangia katika nyanja tofautitofauti tunamopatikana, tunaijenga jamii tofauti. Tumetoka mbali. Uthabiti na nguvu za wanawake zitaleta tofauti.
Afrika ndilo bara changa zaidi ulimwenguni huku 70% ya watu wake wakiwa chini ya miaka 35. Unampa Katibu Mkuu ushauri upi kuhusu vijana wa Afrika?
Ushauri wa kwanza ni kwamba ni sharti tusikilize wanachokisema vijana wa Afrika. Wanataka nini, na matumaini na matarajio yao ni yapi kuhusu bara hili? Zungumza nao na ubuni nafasi nyingi kuwahusisha. Kijana mmoja aliwahi kutuambia: “Kama unataka kuharakisha utendaji, wape vijana nafasi ya kutekeleza kwa kuwa tunakimbia upesi.” Ni muhimu pia kuzungumza kuhusu amani na uthabiti na namna unavyohusiana na maendeleo na ufanisi. Vijana wanasema, “Wekeza katika sisi—wekeza katika matumaini na matamanio yetu, katika ubunifu wetu na katika michango tunayoweza kutoa.”
Ni mambo yapi matatu mazuri uliyoyaona barani Afrika mwaka wa 2019?
Bila shaka, mkataba wa Amani kati ya Eritrea na Uhabeshi uliomfanya Waziri Mkuu wa Uhabeshi, Abiy Ahmed, kupata Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka huu. Aidha juhudi za kuleta Amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini na Sudan pia ni jambo nzuri. Tuzo ya Amani ya Nobel ilikuwa ishara muhimu katika kutambua uwezo wa Afrika kusuluhisha mizozo yake binafsi. Lakini pia nilipenda namna tulivyotia fora katika michezo na utamaduni—Timu Springboks ya Afrika Kusini ilishinda Kombe la Dunia la Raga na Eliud Kipchoge wa Kenya akakivunja kizuizi cha saa mbili katika mbio za masafa marefu. Hizi ndizo hadithi nzuri ninazotaka kusimulia.
Unatarajia nini katika mwaka wa 2020?
Kufanikisha baadhi ya programu na mipango tuliyoweka. Kuipa Ofisi ya Mshauri Maalum Kuhusu Afrika sura mpya (OSAA), kufanya kazi kwa karibu na mataifa wanachama ili kuleta tofauti. Kuendelea kutetea ajenda ya Afrika ya maendeleo, amani na usalama.
Ěý