Uasi wa Boko Haram, na maenezi yake hadi katika mataifa ya Kameruni, Chadi na Nijeri, ndio tishio kubwa la usalama lililotajwa nchini Nijeria. Ila, kulingana na International Crisis Group, mzozo wa mwaka wa 2018 kati ya wakulima na wafugaji nchini Nijeria ulikuwa hatari mara sita zaidi kuliko tishio la Boko Haram.
Mizozo isiyopata kuangaziwa zaidi ni ile ya chini kwa chini kama ya wizi wa mifugo au kushindania raslimali kati ya wakulima na wafugaji. Mizozo hii inaendelezwa na maenezi ya silaha ndogondogo katika maeneo ya mashambani na yaliyotengwa katika bara la Afrika ambako athari ya serikali ni haba.
Mwaka wa 2019, kwa mfano, watu 160 waliuliwa na watu waliojihami katika kijiji kimoja nchini Mali karibu na mpaka wa Bukinafaso katika kile kilichotajwa na vyombo vya habari nchini kama “mauaji mabaya zaidi ya kijamii katika kumbukizi.”
Watekelezaji wa mauaji hayo walisemwa kutoka kwa jamii ya wasasi na wafugaji ya Dogon, ilhali wahasiriwa walichukuliwa kuwa Wafulani, jamii ya wafugaji wa kuhamahama. Jamii hizo zimekuwa zikizozania maji na malisho tangu jadi.
Huu ni mfano mmoja wa mizozo ya kijamii inayotokea katika mataifa mengi barani Afrika, ambako ongezeko la silaha ndogondogo limegeuza mizozo ya maeneo ya mashambani kuwa makabiliano hatari na kuzidisha uhalifu mashambani na mijini
Taasisi ya Masomo ya Usalama, iliyoko jijini Pretoria, Afrika Kusini inaeleza kuwa, “Tangu miaka ya 1990, silaha ndogondogo—haswa bunduki aina ya AK-47—zimekuwa silaha zinazopendelewa na wezi wa mifugo, na kutwaa nafasi ya silaha za kitamaduni zisio hatari sana.”
Kulingana na Small Arms Survey (SAS), kituo cha utafiti kilicho Jeneva kinacholenga kupunguza maenezi haramu na athari ya silaha ndogondogo na nyepesi, zaidi ya 80% ya silaha ndogondogo barani Afrika zi mikononi mwa raia.
Uchunguzi wa 2019 wa SAS na ule wa Umoja wa Afrika, Weapons Compass: Mapping Illicit Small Arms Flows in Africa, ulikadiria kwamba raia, pamoja na vikundi vya waasi na wanamgambo, wanamiliki zaidi ya milioni 40 ya bunduki na silaha. Vikundi vya kiserikali vinamiliki chini ya milioni 11.
Mbali na Nijeria, mizozo ya kijamii ni tishio katika mataifa ya Uhabeshi, Kenya, Somalia, Sudan na Uganda, miongoni mwa mengine. Aghalabu tatizo hili linazidishwa na uchache au ukosefu wa vikosi vya usalama katika maeneo ya mizozo. Hata vinapokuwepo, vikosi hivi hulemewa na kuuliwa.
Baada ya “mauaji ya kijamii” nchini Mali, kikundi cha wanajeshi kilifukuzwa na raia kilipojaribu kumtia mbaroni mshukiwa mmoja wa shambulio aliyetekwa nyara na wenyeji. Baadaye video ya tukio hilo iliwekwa katika mitandao ya kijamii kuviaibisha vikosi vya usalama.
Uhusika wa jamii katika amani
Mara nyingi serikali hupeleka maafisa zaidi wa usalama katika maeneo yaliyoathiriwa na wakati mwingine kufanya oparesheni za kijeshi kwa nia ya kuwatia mbaroni wanamgambo na kukomboa silaha zao. Mipango ya kuwanyang’anya wananchi silaha na kuzinunua tena imetekelezwa katika mataifa kadhaa, ila amani ipatikanayo aghalabu haidumu kwa muda mrefu.
Nchini Nijeria, mbali na kutumia askari na wanajeshi, serikali inawahusisha wanajamii wenyewe katika kusuluhisha mizozo. Mwaka huu serikali ilizindua Mpango wa Kitaifa wa Mageuzi ya Mifugo unaolenga miaka 10 kusaidia kumaliza mizozo ya kijamii inayohusisha mashamba na malisho kwa kuifanya sekta hiyo iwe zalishi zaidi na endelevu pamoja na kuupa usasa uzazi wa mifugo na mbinu za kuzalisha.
Katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mali, ambako mizozo ya kijamii inaendelea kutokea licha ya juhudi za serikali na kuwepo kwa maelfu ya walinda usalama, Umoja wa Mataifa unashirikiana na jamii kusaidia kupunguza taharuki kupitia mipango ya Kupunguza Mizozo ya Jamii (CVR) na kukuomboa silaha kutoka kwa raia, kuwatoa waasi hamasa na kuwajumuisha katika jamii tena (DDR).
CVR na DDR zina malengo sawa: kumaliza mizozo na kujenga amani. Idara ya Oparesheni na Amani ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa mpango wa Kupunguza Mizozo ya Jamii unatofautiana na juhudi nyinginezo “kwa kuwa inashirikiana moja kwa moja na jamii husika kupata masuluhisho kwa vyanzo vya mizozo iendelezwayo kwa silaha ndani ya jamii, na huwalenga makusudi vijana walio katika hatari ya kusajiliwa na makundi yaliyojihami mbali na wapiganaji wa awali.
Mpango huu unaelekea kuzaa matunda katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, japo kidogo. “Ingawaje ni mapema, kuna dalili za awali kwamba CVR inachangia kupunguza uhasama tangu ilipoanzishwa mwaka 2017,” ilisema maakala moja katika jarida la mtandaoni Small Wars Journal, na kutambua kupunguka kwa viwango vya jumla vya mizozo ya vurugu ambako mipango ya CVR inatekelezwa.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa uliripoti mwezi Novemba kwamba jamii mbili za Jamhuri ya Afrika ya Kati zilizokuwa zikizozana, Nièm na Yéléwa, zinaishi kwa amani sasa. Kama sehemu ya mpango wa CVR, wahusiska wa jamii hizo mbili walipewa ng’ombe na mafundisho kuhusu mbinu bora za ufugaji. Jamii hizo mbili sasa zinaweza kujipatia mapato, kupanua shughuli zao na kujenga upya vijiji vyao miaka miwili baada ya uzinduzi wa mpango huo.
Mipango hii imesaidia kurejesha amani kati ya jamii za Nièm na Yéléwa, kulingana na Bachirou Amadou, meya wa huko. Alisema, “Muhimu zaidi ni kwamba jamii hizo mbili hazikuwacha silaha na kuja pamoja tu, bali pia zinashirikiana kibiashara bila uoga wa mizozo.”