51Թ

Wanawake Weusi wapiga picha wafana katika mtandao mpya wa “wasanii”

Get monthly
e-newsletter

Wanawake Weusi wapiga picha wafana katika mtandao mpya wa “wasanii”

Mpiga picha mwenye asili ya Kenya na mzaliwa wa Kenya azindua jukwaa la ulimwengu kutangaza talanta zao.
Franck Kuwonu
Afrika Upya: 
6 May 2021
Mpiga picha Polly Irungu.
Mpiga picha Polly Irungu.
Mpiga picha Polly Irungu.

Polly Irungu, mpiga picha aliyezaliwa Kenya na kukulia Marekaani amezindua “udada” wa kimataifa wa kitaaluma kuziinua sifa zao na kuzitangaza talanta zao.

Kutoka kwa maisha ya “upweke wa kukirihi” mpiga picha Polly Irungu alikuwa mmoja kati ya wasanii na wapiga picha wanaochipuka ambao walikuwa wakipambana kutambua kusudi lao katika ulimwengu huu unaoenda kwa kasi.

Habari haikupatikana kirahisi na kwa miaka mingi, Bi. Irungu hakujua amwendee nani ili kupata uelekezi na wakati uo huo kujipatia riziki kutokana na upigaji picha, ambao pia anauhusudu kwelikweli.

Angefurahia kupokea ushauri kutoka kwa wanairimu wenzake, au ashukuru kwa fursa ya kupata uanagenzi, au kuwa tu sehemu ya jamii ya wapiga picha wasiojali kujadiliana kuhusu tajriba zao kuhusu namna ya kupambana na changamoto za fani ya uanahabari inayokua kwa kasi. Hata hivyo, Bi. Irungu hakupata msaada wa aina hiyo. Kama mpiga picha mchanga aliyefuzu kwa shahada ya Uanahabari, alitamani sana kupatana na watu ambao angeweza kujitabulisha nao kitamaduni na kitaaluma.

Huku akitafakari kuhusu miaka yake ya mwanzo, Bi. Irungu asema, “Nilifahamu bayana kwamba nilihitaji mwelekeo … Zaidi ya hayo, niliihitaji jamii.”

Kuunda mtandao

Hili ndilo lililomwongoza mpiga picha huyu mchanga katika lengo lake la sasa – kuunda mtaandao wa wanawake Weusi wapiga picha wanaoshiriki na kubadilishana maarifa na raslimali ambazo zitawainua na kuwafanya kutambuliwa katika fani ya usanii.

“Kuna nyakati ambazo nilijiwazia, heri kama ningekuwa na jamii, heri ningekuwa na mtu kielelezo, heri kama ningewajua wapiga picha wengine Weusi, hasa wapiga picha na wanawake wanahabari wapiga picha ambao ningewaendea,” Bi Irungu aliiambia AfrikaUpya.

“Hatimaye nilitambua kwamba nilihitaji kufanya kitu badala ya kusalia pembeni,” alisema. “Upigaji picha umesalia fani iliyotawaaliwa na Wazungu.”

Mpiga picha Polly Irungu.

Bi. Irungu alizaliwa Nairobi na akakulia Marekani ambako alijikuta katika upigaji picha kinasibu tu. Aliinunua kamera ya kwanza na tarakilishi mwishoni mwa mwaka wake wa mwisho wa shule ya upili kwa fedha alizolipwa baada ya kufanya kazi katika mkahawa mmoja wa vyakula.

Aliwapiga picha jamaa zake, marafiki, na karibu kila mtu na kila kitu alichokiona. Alijifundisha ujuzi na akaisakura mitandao ili kupata maarifa kuhusu upigaji picha.

Kuanzia mwanzo, kulikuwa na orodha ya wanawake Weusi wapiga picha ambayo Bi. Irungu alikuwa ameiandaa miaka michache awali. Aliitoa vumbi na akaaandika kwenye twiti kuihusu. Baada ya twiti yake kusambazwa kwa zaidi ya twiti mia mbili, aliamua kuwatafuta waliohusika, kujitambulisha na kuwauliza kuhusu tajriba zao.

“Kazi yako ya mwisho ilikuwa gani? Je, ulilipwa? Wewe hupata ajira mara ngapi? Je, umewahi kuhisi nyakati ambazo ulitaka kuiwacha fani hii?” Ni baadhi ya maswali, aliyouliza, na kutambua kwamba tajriba zao zilifanana kwa kila hali.

Takriban miezi mitano baadaye, uamuzi wa Bi Irungu “kufanya kitu” umesababisha kuwepo kwa jamii yenye uanuwai wa wanawake Weusi wapiga picha — mpango wenye nia, unatangaza, “kuchachawiza uelewa kwamba ni vigumu kuwatambua kuwapa majukumu wasanii Weusi.”

Kwa muda mrefu sasa, mtandao huo wa Wanawake Weusi Wapiga picha uliofikiriwa umekuwa jamii anuwai ya Wanawake Weusi ambao wangechachawiza uelewa kwamba ni vigumu kuwatambua na kuwapa majukumu wasanii weusi.”

Kuipigapiga orodha ya kitambo ili kutoa vumbi

Wakati COVID-19 ilipotukumba, kupata ajira ilikuwa vigumu. Maandamano dhidi ya ukatili wa polisi yalilipuka kote Marekani na kwingineko ulimwenguni kufuatia kifo cha George Floyd.

Kwa wanahabari, matukio ya kihistoria ambayo yalishuhudiwa katika majiji ulimwenguni kote yangetoa fursa murua ya kufanya kazi. Bali fursa hizi zilisalia nadra kwa mtu kama Bi. Irungu.

Leo hii, mtandao wa Wanawake Weusi Wapiga Picha (BWP) umesalia ghala la data ya kidijitali ya washiriki 600 tangu kuzinduliwa kwa mara ya kwanza mwezi wa Julai 2020 kwa msaada kutoka kwa hazina ya msaada ya COVID-19 (#BWPReliefFund) iliyochanga zaidi ya $14,000 kutoa msaada wa kifedha kwa wanawake Weusi na kwa wapiga picha wasio wa jinsia mahususi wakati wa janga la COVID-19.

“Nilipoanza kufanya hili,” alisema, “kwa kweli sikutumia (matukio yaliyochipuka) kuamua mwelekeo wangu. Nilichokitumia kilikuwa tajriba zangu pamoja na zile nilizokuwa nikizisikia kutoka kwa wanawake ili kuamua kuhusu mwelekeo wangu.”

Hata hivyo, haiwezi kupuuzwa kwamba mpango huo uliwavutia watu wengi kutoka janibu zote za ulimwengu, kwa sababu mazungumzo kuhusu rangi ya watu na haki yaliwavutia watu wengi.

Washiriki wa jamii hii wanatoka katika mataifa kama Nijeria, Kenya, Afrika Kusini, Japani na Australia.

Na ukimsikia Bi. Irungu akisema; huu ni mwanzo tu: “Kinachonipa msukumo zaidi ni kuweza kumulika mwangaza kwa visa vilivyopuuzwa kwa muda mrefu.”