Ikiwa leo ni siku ya udongo duniani , shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO limesisitiza umuhimu wa kuhifadhi udongo ili kuhakikisha unaendelea kuleta tija kwa maisha ya mamilioni ya watu duniani wanaotegemea chakula kutoka kwenye kilimo kwani udongoni ndiko chakula kinakoanzia.
Katika taarifa yake kuhusu siku hii ya udongo duniani ambayo mwaka huu imebeba maudhudhi“Udongoni ndiko chakula kinakoanzia”imesema kwamba “Udongo wenye afya ni msingi wa chakula bora na mazingira bora na licha ya maendeleo yote yaliyopigwa katika teknolojia binadamu bado wanategemea sentimita chache za udongo ili kuishi kwani asilimia 95% ya chakula tunachokula kinazalishwa na wakulima katika udongo wetu.”
Kwa mujibu wa FAO kuna viumbe hai zaidi katika kijiko kimoja cha udongo kuliko watu duniani. Udongo ni ulimwengu unaoundwa na viumbe, madini, na chembechembe ambazo hutoa chakula kwa wanadamu na wanyama kupitia ukuaji wa mimea.
Shirika hilo limesisitiza kuwa“Kama tulivyo sisi binadamu, udongo nao unahitaji mgawanyo sawia na tofauti wa virutubisho katika viwango vinavyofaa ili kuwa na afya. Mifumo ya kilimo hupoteza virutubisho kwa kila mavuno, na ikiwa udongo hautasimamiwa kwa uendelevu, basi rutuba inapotea hatua kwa hatua, na udongo utazalisha mimea isiyo na virutubisho.”
Hivyo FAO imesema“Upotevu wa virutubisho vya udongo ni mchakato mkubwa wa mmomonyoko wa udongo unaotishia lishe. Unatambulika kuwa miongoni mwa matatizo makubwa zaidi katika ngazi ya kimataifa kwa ajili ya uhakika na uendelevu wa chakula kote ulimwenguni.”
Zaidi ya miaka 70 iliyopita, shirika hilo limesena kiwango cha vitamini na virutubisho katika chakula kimepungua sana, na inakadiriwa kuwa watu bilioni 2 duniani kote wanakabiliwa na ukosefu wa virutubisho unayojulikana kama njaa iliyojificha kwa sababu ni vigumu kuitambua.
Pia FAO inasema mmomonyoko wa udongo unasababisha baadhi ya udongo kukosa virutubisho na kupoteza uwezo wake wa kurutubisha mazao, huku udongo mwingine ukiwa na mkusanyiko mkubwa wa virutubisho ambavyo vinaowakilisha mazingira yenye sumu kwa mimea na wanyama, huchafua mazingira na kusababisha mabadiliko ya tabianchi.
Siku ya udongo duniani inayoadhimishwa kila mwaka Desemba 5 mwaka huu 2022kampeni yake ya “Udongo ndiko chakula kinakoanzia”inalenga"kuongeza uelewa wa umuhimu wa kudumisha mfumo wa ikolojia wenye afya na ustawi wa binadamu kwa kushughulikia changamoto zinazoongezeka katika usimamizi wa udongo, kuongeza uelewa wa udongo na kuhimiza jamii kuzingatia kuboresha afya ya udongo."