51Թ

Wanahabari wa Kiafrika: Mafundisho zaidi na raslimali zitapiga jeki utoaji habari kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Get monthly
e-newsletter

Wanahabari wa Kiafrika: Mafundisho zaidi na raslimali zitapiga jeki utoaji habari kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Taarifa kuhusu mazingira ni ghali; zinahitaji kusafiri kwingi na kujasirisha
Kingsley Ighobor
Afrika Upya: 
22 December 2022
Journalists reporting at COP27 in Sharm El Sheikh, Egypt

Mwishoni mwa taarifa ya habari ya dakika tano kutoka kwa studio ya muda huko Sharm El Sheikh, Misri, ukumbi wa COP27, mwanahabari anayeishi Cotonou Ghyslaine Florida Zossoungbo aliweza kutoa taarifa wakati ikitokea kwa wananchi wenzake wa Jamhuri ya Benin.

Bi. Zossoungbo anaripotia , jukwaa la mtandaoni lililojitolea kukuza Malengo ya Maendeleo Endelevu () (SDGs) nchini mwake.

Siku hii, alikuwa amepata kona ndogo katika moja ya banda huko COP27, alikaa kwenye kiti kirefu nyuma ya tarakilishi huku kamera ikiwa juu ya kiweko chenye miguu mitatu umbali wa futi chache.

Bi. Zossoungbo na wanahabari wengine, hata wale wa mashirika makuu ya vyombo vya habari kama vile CNN au wanablogu waliozishika iPhone lakini wenye wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii, walikimbia kwa kasi kuwafuata watu mashuhuri na viongozi wa dunia au mtu yeyote ambaye alikuwa na jambo muhimu la kusema kuhusu mabadiliko ya tabianchi katika kongamano hilo.

Na mwishoni mwa kila siku, mara moja walizitangazia hadhira zao kimataifa maudhui kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo, licha ya jitihada bora za Bi. Zossoungbo za kuripoti kuhusu mgogoro wa tabianchi, akichochewa na teknolojia mpya ya habari ya umma, anasema kuripoti kuhusu mabadiliko ya tabianchi katika nchi yake—labda pia katika maeneo mengine ya Afrika—kunakabiliwa na changamoto.

"Sisi ndio taasisi pekee ya vyombo vya habari ambayo inaripoti mara kwa mara kuhusu mgogoro wa tabianchi kwa sababu tunaangazia SDGs," Bi. Zossoungbo anasema. "Vyombo vya habari vingine vinazingatia siasa na masuala mengine."

Anaongeza: “Watu wanaweza kuona kwamba kuna kitu kinachotokea kwa hali ya hewa kwa sababu ya mafuriko na ukame, lakini bado hawaelewi ni nini katika muktadha wake kamili. Kwa hivyo tunaendelea kuzungumza na kuzungumza juu yake."

Nchini Kameroon, Killian Chimton Ngala, mwanahabari anayetajika sana, anaeleza, “Mabadiliko ya tabianchi mara nyingi hayatokei katika kurasa za mbele za magazeti au habari za runinga au redio.”

Kuripoti kuhusu tabianchi hukosa muktadha mara nyingi. Wanahabari wanaporipoti kuhusu mafuriko, kwa mfano, hawayahusishi na mabadiliko ya tabianchi haswa. Agahalabu wao wanaangazia tukio na athari zake.

Muktadha wa kuripoti

Tajriba ya Bwana Ngala ni kwamba “Kuripoti kuhusu tabianchi hukosa muktadha mara nyingi. Wanahabari wanaporipoti kuhusu mafuriko, kwa mfano, hawayahusishi na mabadiliko ya tabianchi haswa. Agahalabu wao wanaangazia tukio na athari zake.”

Bila mtazamo, kuripoti kuhusu mabadiliko ya tabianchi kunakuwa dhana changamano kwa wengi, haswa watu mashinani.

Bw. Ngala anatoa mfano wa ripoti kama hiyo: "Si muda mrefu uliopita, mapigano yalizuka kati ya jamii katika Mkoa wa Kaskazini wa Kameroon, kati ya wafugaji wa ng'ombe wa Choa-Arab na wakulima wa Mousgoum, kwa sababu ya kudidimia kwa rasilimali za maji.

Watu wengi walifariki katika mzozo huo, na afisa wa juu wa serikali akaamua kulitembelea eneo hilo.

"Je! unajua jinsi wanahabari walivyoripoti habari hiyo?" Bwana Ngala anauliza kwa kejeli. “Wote waliripoti kwamba waziri alizionya jamii na akazitaka ziwe na amani.

"Ilhali, ukiitazama, ni kwa nini jamii zilikuwa zinapigana? Ni kwa sababu kijito cha kijiji kilikuwa kikikauka, na wakaaji wa jamii na wafugaji ng’ombe walilazimika kupigania maji kidogo, tokeo la mabadiliko ya hali ya hewa.

“Ukiuliza watu wengi baŕani Afŕika ni kwa nini ziwa lao linakauka au ni kwa nini wanakumbwa na ukame wa mara kwa mara, wengine hata hawatajua, achilia mbali kupendekeza suluhu.

"Zingatia kukauka kwa Ziwa Chad, ambako kunawalazimu wafugaji kaskazini mwa Nijeria na Kameroon kuhamia kusini. Wakulima wa kusini wanaamini kuwa wafugaji wanakuja kuzinyakua ardhi zao. Pambano lililotokea limegharimu maisha ya wengi,” analalamika.

Ni kwa nini basi vyombo vya habari havisimulii hadithi ya tabianchi kithabiti inavyopaswa kuwa?

Kuripoti kuhusu mazingira ni ghali; kunahitaji kusafiri sana na kujasirisha. Si nafuu. Mashirika mengi ya habari barani Afrika yanaona kuwa hayawezi kumudu. Kwa mfano, hayana uwezo wa kutumia maelfu ya dola kufadhili wanahabari kuripoti COP27

Haja ya mafundisho

Bw. Ngala analaumu kwa ukosefu wa rasilimali na mafundisho.

“Kuripoti kuhusu mazingira ni ghali; kunahitaji kusafiri sana na kujasirisha. Si nafuu. Mashirika mengi ya habari barani Afrika yanaona kuwa hayawezi kumudu. Kwa mfano, hayana uwezo wa kutumia maelfu ya dola kufadhili wanahabari kuripoti COP27,” anasema Bw. Ngala.

“Kuna waandishi wachache sana wa mazingira katika vyumba vya habari waliopata mafundisho”, anasema. Matokeo ni kuwa kuripoti kuhusu mabadiliko ya tabianchi bado hakupati umuhimu unaostahili.

“Wasimamizi wa vyombo vya habari wanastahabu kutuma wanahabari kuangazia siasa, zinazoendesha mauzo, kuliko kuripoti masuala yanayohusiana na mazingira, isipokuwa kama ni janga kubwa. Wanasstahabu kutuma wanahabari kuangazia safari ya Rais wetu Addis Ababa kuliko COP27,” anasema.

Wadhamini wa nje

Bw. Ngala alikuwa mmoja kati ya wanahabari kadhaa wa Kiafrika waliodhaminiwa kuripoti kuhusu COP27 na mashirika yanayaoangazia tabianchi, haswa katika Uropa na Amerika ya Kaskazini.

Kwa mfano, mpango wa ushirika wa Climate Change Media Partnership (CCMP), mradi wa Earth Journalism Network (EJN) unaosimamiwa na Internews, Kituo cha Amani na Usalama cha Stanley, ulimleta Bw. Ngala na wanahabari wengine watano wa Kiafrika Sharm El Sheikh ili kuripoti kuhusu COP27. Walikuwa kati ya wanahabari 20 (kutoka zaidi ya 500 waliotuma maombi) kutoka kwa mataifa maskini na yenye mapato wastani yaliyodhaminiwa chini ya ushirika huo.

Kifurushi cha ushirika huo kinahusisha mafundisho kuhusu "kuripoti matukio katika COP27 kwa njia bora," kulingana na tangazo la EJN, na kuongeza kuwa Afrika inachangia asilimia 2-3 ya uzalishaji wa hewa hatari duniani lakini inaathiriwa pakubwa na mgogoro wa tabianchi. Kwa hiyo, ni lazima wanahabari wa Kiafrika waendelee kuripoti kuhusu athari za mgogoro huo na kuziwajibisha serikali.

"Ulikuwa ni mchakato mkali wa kutuma maombi," anasema Evelyn Kpadeh Seagbeh wa shirika la Power FM na Televisheni lililoko Liberia, ambalo pia ni mshirika.

"Lakini nisingekuwa hapa bila ushirika, [COP27]. Nilituma maombi ya ushirika kwa sababu kuja hapa kwa wiki mbili kungegharimu maelfu ya dola, ambazo huenda shirika langu lisingeweza kumudu.”

Ninaamini hali inabadilika taratibu. Nchini Nigeria, kuripoti kuhusu mgogoro wa tabianchi kunazidi kupata umaarufu polepole lakini kwa kasi katika vyombo vya habari. Tutafaulu

Maudhui ya Tabianchi

Uhusiano wa kufaana kati ya watayarishaji wa maudhui ya habari na hadhira zao ni changamano.

Haja zinazodhaniwa za hadhira zinaweza kuathiri utayarishaji wa maudhui hata kama jukumu la kuweka ajenda la vyombo vya habari linahusisha kuongoza hadhira kuzingatia masuala mahususi.

Inaelekeza kwa hoja kwamba wanahabari wa Kiafrika bado hawajahusisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi kikamilifu na ustawi wa kijamii na kiuchumi wa raia.

"Hilo ndilo suala," anajibu Bw. Ngala. "Wanahabari wanaripoti kuhusu mazingira kwa kuyatenga na sekta nyingine za maendeleo ya kiuchumi. Unaweza kuona ni kwa nini, katika mataifa mengi, wizara za masuala ya kiuchumi hazizingatii mgogoro wa tabianchi kama sehemu ya uwaziri wao. Mara nyingi ni hifadhi ya wizara za mazingira ambazo hupata ufadhili mdogo.”

"Kuna ukosefu wa kuthamini umuhimu wa mgogoro wa tabianchi," anaelezea Mwika Bennet Simbeye, kaimu Mhariri Mtendaji wa Times of Zambia.

"Wanahabari kisilka huwa na mwelekeo wa kuangazia matatizo ya kila siku—sarakasi zote za kisiasa na masuala ya kawaida," Anasema Bw. Simbeye.

Huku akikubali kwamba mafundisho na ongezeko la rasilimali za ufadhili zitainua viwango vya kuripoti kuhusu mazingira, Paul Omorogbe, Ripota Mkuu wa Tribune of Nijeria, ana matumaini.

“Ninaamini hali inabadilika taratibu. Nchini Nigeria, kuripoti kuhusu mgogoro wa tabianchi kunazidi kupata umaarufu polepole lakini kwa kasi katika vyombo vya habari. Tutafaulu.”