51³Ô¹Ï

Chuki hufunzwa: tunaweza kupambana nayo

Get monthly
e-newsletter

Chuki hufunzwa: tunaweza kupambana nayo

Mkakati mpya, 'Mpango wa Michezo' wa Umoja wa Mataifa na washirika utasaidia kupambana na Matamshi ya chuki kupitia ushirikiano na Michezo.
Afrika Upya: 
6 June 2023
Alice Wairimu Nderitu.
Ikiwa huwezi kusoma sasa, sikiliza tu toleo la sauti: 
Sauti iko kwa Kiingereza.

Kutangulia Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Matamshi ya Chuki inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 18 Juni, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mshauri Maalum wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari, Alice Wairimu Nderitu, anaangazia matamshi ya chuki katika michezo na kwa nini tunapaswa kupambana nayo:

Matukio ambayo yalikuwa ya kufurahisha na kuhuzunisha vilevile yalijiri huko Madrid Jumatano Mei 24, 2023. Ndani ya uwanja mkubwa zaidi nchini Uhispania, Santiago Bernabéu, timu ya nyumbani Real Madrid ilisimama pamoja na mwenzao, Vinícius Jr, ambaye siku zilizopita alikuwa mwathirika wa matamshi ya chuki.

Nyota huyo wa Brazili mwenye umri wa miaka 23 alivumilia semi za kiubaguzi wa rangi wakati wa mechi ambayo ilimfanya achukizwe na hivyo kueleza nia yake ya kuondoka Uhispania na kuachana na ligi yake ya soka, La Liga.

Siku hiyo ya Jumatano usiku, hata hivyo, Vinícius Jr alipoingia uwanjani kabla ya mechi ya Real Madrid na Rayo, huenda alihisi tofauti kidogo. Wachezaji wote walikuwa wakivalia jezi za ‘Vini Jr. 20’ kuonyesha mshikamano naye. Wachezaji wa timu mbili zinazoshindana waliinua bendera pamoja iliyotangaza: "Wabaguzi wa rangi, wasishiriki soka".

Tumekuja kuelewa kuwa hii ni kauli mbiu ya kampeni mpya iliyoanzishwa na mamlaka za michezo nchini Uhisipania kupiga vita ubaguzi wa rangi katika soka - doa ambalo si la kipekee kwa mchezo mmoja au nchi moja.

Karibu na Santiago Bernabéu, timu ya wanawake ya Madrid na timu za mpira wa vikapu pia zilivaa mashati ya 'Vini Jr' kabla ya michezo yao - onyesho lingine la mshikamano na nyota huyo wa Brazil.

Usiku huo wa Jumatano, tofauti na Jumapili iliyotangulia huko Valencia, kulikuwa na mshikamano. Kulikuwa na utu. Kulikuwa na ahadi, na tumaini.

Tangu wakati huo, nyota wengi wa michezo wamejitokeza kumuunga mkono Vini Jr. kufuatia tukio hilo baya na la kudharauliwa huko Valencia, kama vile wasimamizi wa michezo na wanasiasa.

Kuna ongezeko la utambuzi kwamba matamshi haya yasipopigwa vita, mchezo huu mzuri utaendelea kukumbwa na doa baya.

Ni utambuzi kwamba, kwa kuwa matamshi ya chuki yanafundishwa, yanaweza kupigwa vita. Ni lazima tufanye yote tuwezayo ili kupambana na matamshi ya chuki katika aina zake zote, ikijumuisha zile zinazowasilishwa katika masimulizi na nyimbo za ubaguzi wa rangi. Utambuzi huu upya unaleta matumaini.

Kwa hakika, sisi sote tuko sawa, katika utofauti wetu kama wanadamu. Hata hivyo, hisia hii ya umoja inaweza kuangamizwa haraka na matamshi ya chuki yenye misingi ya rangi, kabila, dini, utaifa, jinsia, ukimbizi na hali ya uhamiaji, ulemavu, au aina nyingine yoyote ya utambulisho.

Ofisi yangu inafanya kazi usiku na mchana kushughulikia na kupambana na matamshi ya chuki, ambayo yalikuwa wazi sana katika semi za ubaguzi wa rangi dhidi ya Vini Jr.

Hali ilivyo Brazili

Kisadfa, nilikuwa nimerejea kutoka nchi yake Vini Jr., Brazili, ambako watu wa asili ya Kiafrika kama yeye, na watu wa kiasili, wanaendelea kukabiliana na changamoto zinazohitaji kushughulikiwa haraka.

Michezo, hasa kandanda, huvutia mamilioni ya watazamaji duniani kote, na kwa sababu hiyo, matamshi ya chuki yanayotolewa wakati wa mchezo, kama tulivyoshuhudia huko Valencia, yanaweza kusikika kote ulimwenguni. Lakini wachezaji walipoungana kupambana na matamshi ya chuki yaliyoelekezewa Vini Jr. ulimwengu mzima pia ulisikia kuhusu mapambano hayo, na yalionekana kupata mvuto zaidi kuliko matamshi ya chuki yenyewe.

Ndani ya muktadha huu, sisi pamoja na washirika wengine, tumeandaa Mpango wa Utekelezaji wa Kupambana na Matamshi ya Chuki kwa Kujihusisha na Michezo: MPANGO WA MCHEZO, uliozinduliwa Disemba mwaka jana, ambao tulianza kuupanua kwa 'Mkutano Mkuu wa Kukomesha Chuki Michezoni'Ìý nchini Uingereza, iliyoandaliwa na Klabu ya Kandanda ya Liverpool mwezi Aprili mwaka huu.

MPANGO WA MCHEZO unatokana na Mkakati na Mpango wa Utekelezaji wa Umoja wa Mataifa kuhusu Matamshi ya Chuki na unawiana kikamilifu na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, hasa, haki ya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni - haki ambayo inapaswa kulindwa, na si kutumiwa vibaya.

MPANGO WA MCHEZO ulitokana na ufahamu kwamba mhalifu wa matamshi ya chuki mara nyingi huwa amekumbana na matamshi ya chuki yaliyomdunisha mtu mwingine. Pia inatokana na ukweli kwamba wahalifu wengi ni kama watu wengi wa kawaida ambao ni mashabiki wa michezo kama wewe na mimi.

Kwa kuidhinisha Julai 2021, Juni 18 kama Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Matamshi ya Chuki, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulitambua haja ya kukabiliana na ubaguzi, chuki dhidi ya wageni na matamshi ya chuki, na kutoa wito kwa wahusika wote muhimu, ikiwemo nchi, kuongeza juhudi zao kushughulikia suala hili, kwa kuzingatia sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Katika historia, matamshi ya chuki yamejulikana kusababisha unyanyapaa, kuwatenga watu, na hatimaye kuchochea uhalifu wa chuki na mizozo mikubwa, ikiwemo mauaji ya kimbari.

Matamshi ya chuki ni sumu, lakini yanaweza kukomeshwa.


Bi. Nderituni Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Kuzuia Mauaji ya Kimbari.Ìý

More from this author