Shirika la Afya Duniani na UNFPA, shirika la Umoja wa Mataifa la afya ya uzazi, wanatoa tahadhari kwamba kuendelea kwa mashambulizi dhidi ya vituo vya afya, majengo na wafanyakazi nchini Sudan kunawanyima wanawake na wasichana huduma za afya za kuokoa maisha, huku wanawake wajawazito wakiathirika zaidi.
Asilimia 67 ya hospitali katika maeneo yaliyoathiriwa na vita zimefungwa, na hospitali kadhaa za kuzalishi3a watoto hazifanyi kazi, ikiwemo Hospitali ya Omdurman, hospitali kubwa ya rufaa nchini Sudan.
Miongoni mwa watu milioni 11 nchini Sudan wanaohitaji msaada wa dharura wa afya ni wanawake na wasichana wapatao milioni 2.64 walio katika umri wa uzazi. Baadhi yao, wanawake 262,880 ni wajawazito na zaidi ya 90,000 watajifungua katika muda wa miezi mitatu ijayo. Wote hawa wanahitaji kupata huduma muhimu za afya ya uzazi.
Tangu Aprili 2023, vita vilipoanza, Shirika la Afya Duniani limethibitisha mashambulizi 46 dhidi ya wahudumu wa afya na vituo, mashambulizi yaliyoua watu wanane na kujeruhi wengine 18. Vifaa na mali za kiafya pia zimeporwa, na wafanyakazi wa afya wamekumbwa na vita. Idadi ya vituo vya afya vinatumiwa na vikosi vya kijeshi.
Kuna ripoti za uvamizi wa kijeshi wa mahifadhi ya Hazina ya Kitaifa ya Dawa na Bidhaa za Kimatibabu (NMSF) katika mji mkuu, Khartoum, ambapo dawa za nchi nzima, ikiwa ni pamoja na dawa za malaria, zinahifadhiwa, na pia ndiko hifadhi ya dawa za kitaifa za magonjwa sugu.
Hifadhi ya Shirika la Afya Duniani ya vifaa vya matibabu ya dharura na bidhaa za maendeleo huhifadhiwa kwenye mahifadhi kwenye majengo yake.
Akiba ya UNFPA ya dawa na vifaa kwa ajili ya huduma za uzazi, matibabu ya baada ya ubakaji, pamoja na aina mbalimbali za dawa za kupanga uzazi, ambazo zimehifadhiwa kwenye mahifadhi huko Khartoum, Darfur Kusini, Darfur Magharibi na kwingineko pia hazipatikani.
Vituo vya afya katika majimbo kadhaa, ikiwemo Darfur, vimeonya kwamba vinakumbwa na uhaba mkubwa wa vifaa vya kimatibabu.
Katika hali inayojiri, hospitali zinakosa mafuta ya jenereta zinazoleta umeme. Watoto sita wachanga walifariki katika hospitali moja katika jiji la Eld'aeen Mashariki mwa Darfur katika muda wa wiki moja kutokana na matatizo mengi yakiwemo ukosefu wa oksijeni huku kukiwa na kukatika kwa umeme na madaktari wa eneo hilo wakikadiria kuwa zaidi ya watoto 30 waliozaliwa wamefariki katika hospitali hiyo tangu kuanza kwa vita.
Mwezi Mei, UNFPA na mshirika wa nchini, Shirika la Maendeleo la CAFA, walitoa mafuta kwa hospitali saba za kuzalia watoto mjini Khartoum ili kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa wanawake na watoto wachanga.
Katika wiki moja tu, zaidi ya wanawake 1,000 walijifungua salama ama kikawaida au kupitia upasuaji. Lakini msaada zaidi unahitajika kupata mafuta na vifaa kwa ajili ya hospitali muhimu ili kuendeleza huduma muhimu.
Asilimia 15 ya wanawake wajawazito hupata matatizo yanayohusiana na ujauzito na kujifungua na wanahitaji kupata huduma ya dharura ya uzazi na watoto wachanga.
Shirika la UNFPA linatoa huduma ya afya ya kingono na uzazi kupitia vituo vya afya na hospitali kote nchini Sudan.
Wakunga waliopatiwa mafunzo na shirika la UNFPA wanaendelea kusaidia wanawake kujifungua salama nyumbani na katika vituo vya afya vinavyofanya kazi. Kuna takriban wakunga 27,000 wanaofanya kazi kote Sudan; karibu 2,330 katika mji mkuu. Wengi wao huzalisha watoto wapatao watatu au wanne kwa siku, kulingana na mkuu wa muungano wa wakunga unaoufadhiliwa na UNFPA.
UNFPA pia linaunda maeneo salama kwa wanawake na kutoa huduma za kuzuia na kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia (GBV), ikijumuisha matibabu ya baada ya ubakaji, ushauri nasaha na kudhibiti visa hivyo; pamoja na kutoa huduma za mbali. UNFPA pia inatoa mafunzo kwa wahudumu na mashirika ya kijamii yanayotoa ulinzi, kuzuia na kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia.
Shirika la Afya Duniani linafanya kazi kwa karibu na Wizara ya Afya na washirika wengine ili kuhakikisha utoaji wa huduma muhimu za ngono, uzazi, watoto wachanga pamoja na huduma za dharura za uzazi na watoto wachanga mjini Khartoum na Gezira, na katika majimbo yanayohifadhi wakimbizi wa ndani.
Shirika la Afya Duniani linatoa dawa na vifaa vya kuokoa maisha na kugharamia uendeshaji wa vituo vya afya vinavyotoa huduma hizi. Shirika la Afya Duniani pia linatoa mafunzo kwa wafanyakazi wa afya walio kwenye usaidizi wa kwanza, kutoa matibabu baada ya ubakaji na afya ya akili kwa waathirika wa unyanyasaji wa kingono na linasaidia Mashirika mengine yasiyo ya kiserikali yanayotoa huduma kwa waathiriwa wa unyanyasaji wa kingono.
"Wahudumu wa afya wanahatarisha maisha yao ili kutoa huduma za dharura, uzazi, matibabu ya watoto wachanga na magonjwa sugu na tunawasaidia," Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus. "Tunatoa wito kwa pande zinazozozana kuheshimu ahadi walizofanya huko Jeddah mwezi Mei, ikiwemo kurejesha huduma muhimu na kuondolewa kwa wanajeshi hospitalini na kwenye vituo muhimu vya umma."
“Mizozo lazima ikome, vituo vya afya, wahudumu wa afya na wagonjwa lazima walindwe, misaadwa ya kibinadamu na kimatibabu lazime iendelee kutolewa,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt. Natalia Kanem. "Watu wanaohitaji huduma ya afya ya dharura hawapaswi kuogopa kuondoka majumbani mwao kwa kuhofia usalama wao, na haki ya wanawake ya kupata huduma ya afya ya uzazi lazima ilindwe, iwe kuna mzozo au hakuna mzozo wowote," aliongeza.