Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema maono ya baba wa taifa la India, Mahatma Gandhi yameendelea kuvuma ulimwenguni kote kupitia kazi za umoja huo za maelewano, usawa, maendeleo endelevu, uwezeshaji vijana na suluhu ya amani ya mizozo.
Guterres amesema hayo leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya kupinga machafuko, ikiwa pia ni kumbukumbu ya miaka 150 tangu kuzaliwa kwa hayati Gandhi.
Amesema,“katika zama za sasa za misukosuko, machafuko yanajitokeza katika njia nyingi, kama vile dharura za uharibifu wa tabianchi, uteketezi uliosababishwa na migogoro ya silaha, umaskini, udhalimu wa ukiukwaji wa haki za binadamu na athari za kikatili za kauli za chuki.”
Bwana Guterres amesema, bila shaka iwe mitandaoni au nje ya mitandao,“kote tunasikia kauli za chuki zinazoelekezwa kwenye makundi madogo au mtu yeyote anayechukuliwa kama tofauti na wengine”
Amesema ni kwa mantiki hiyo,“Umoja wa Mataifa umezindua hatua mbili za haraka ili kushughulikia changamoto hii inayozidi kuchipuka. Hatua ya kwanza ikiwa mpango wa hatua dhidi ya kauli za chuki na ya pili ikihusiana na usalama kwenye maeneo ya kidini. Na wiki iliyopita, nilitoa wito wa kimataifa kwa hatua ya muongo wa kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, tukilenga amani, ustawi na heshima katika sayari yenye afya.”
Katibu Mkuu amesema,“Gandhi alikuwa na mazoea ya kusisitiza pengo kati ya kile tunachofanya, na kile tunachoweza kufanya na kwa mantiki hiyo katika siku hii ya Kimataifa, nawasihi kila mmoja wetu kufanya kila kitu kwa uwezo wetu kuziba pengo hili wakati tunajitahidi kujenga mustakabali bora kwa wote.”