Mradi waushirikiano kati ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na Seriali ya Malawi kuboresha hali ya lishe ya wanawake wajawazito, akina mama na watoto wenye umri chini ya miaka mitano umekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi nchini Malawi.
Mradi wa kuboresha hali ya lishe ili kupambana na utapiamlo katika wilaya sita za nchini Malawi, ni msaada mkubwa wa kidunia ambao unazileta pamoja nchi kadhaa katika juhudi za kuweka sera za nchi katika kutekeleza mipango yenye malengo ya pamoja kuhusu lishe.
Kupitia ufadhili wa Wizara ya ushirika wa uchumi na maendeleo ya Ujerumani, BMZ, vikundi vya viongozi wa huduma katika jamii wanaimarishwa katika ujuzi na maarifa ili wanapotembelea nyumba kwa nyuma, watoe ushauri nasaha kwa akina mama na wasaidizi wa nyumbani kuhusu lishe bora.
Mmoja wa akina mama wanufaika ni Elizabeth Chirwa wa Kijiji cha Chatupa kilichoko katika wilaya ya Nkhata Bay. Ana mtoto wa kike mwenye umri wa miezi nane. Elizabeth anasema,
“Nilijifunza kuwa ili mtoto kukua vema, anatakiwa kulishwa chakula kizuri. Nimejifunza kuhusu kuwa na bustani za nyuma ya nyumba ambako nalima mbogamboga kuhakikisha mtoto wangu analishwa kwa mujibu wa makundi sita ya chakula. Ninaongeza mbogamboga katika uji ninaouandaa. Ninampeleka mtoto wangu katika ufuatiliaji wa ukuaji. Nimejifunza kuwa uanatakiwa kumpeleka mtoto wako wa chini ya umri wa miaka mitano katika kiliniki kila mwezi kwa ajili ya ufuatiliaji wa ukuaji, chanjo na kupokea virutubisho vya vitamini C.”
Viongozi wa kikundi cha kutoa huduma, wanawapima watoto ili kufanya utambuzi wa mapema wa utapiamlo na kuwaelekeza mapema kwenda kupata matibabu katika vituo vya afya.
Pia vikundi vinafanya maonesho ya maelekezo kuhusu mapishi. Ili kuboresha chakula, unga wa lishe unaongezwa katika chakula cha watoto wa umri wa miezi 6 hadi 24. Ganizani Mhoni ni kiongozi wa kikundi cha Kaimika Care kutoka Nkhata Bay anasema,Katika vikao vyetu vya kikundi tunawafundisha walezi kuhusu usafi na kujisafi. Tumekuwa tukifanya matembezi majumbani kuwashauri kuhusu aina tofauti za kujisafi. Kuna usafi binafsi, usafi wa nyumba na mazingira. Tunawafundisha pia jinsi ya kuwahudumia watoto wao kwa maana ya jinsi ya kuandaa chakula na jinsi ya kulisha. Pia kuhusu usafi na kujisafi, tumekuwa tukizisihi kaya kuwa na choo cha shimo na vifaa vya kunawa mikono na kwamba katika eneo la kunawa mikono waweke sabuni kuzuia magonjwa ambayo yanaweza kuvuruga ukuaji mzuri wa watoto wao."
Matokeo ya ya programu hii yanaonekana katika hali ya lishe ya wanawake na watoto waliolengwa. Mama mwingine anasema, Tangu mwaka jana 2019, takribani watoto 310,000 na wanawake 400,000 wamenufaika kutokana na mradi huu.