Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wazuru Côte d'Ivoire na Guinea-Bissau.
Get monthly
e-newsletter
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wazuru Côte d'Ivoire na Guinea-Bissau.
Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wako ziarani Afrika magharibi ambako wanatathmini hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa amani nchini Côte d'Ivoire na Guinea-Bissau.
Wajumbe hao wamewasili Alhamisi wiki hii katika mji mkuu wa Côte d'Ivoire, Abidjan ambako Balozi Anatolio Ndong Mba wa Equatorial Guinea, rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Februari na mkuumwenza wa ujumbe na wajumbe wa Baraza la Usalama wamekutana na waziri wa mambo ya nje, Marcel Amon-Tanoh na makamu wa rais, Daniel Kablan Duncan.
Wajumbe wa Baraza la Usalama wameshiriki katika mazungumzo ya mezani kuhusu mabadiliko kutoka kwa ulinzi wa amani hadi ujenzi wa amani na wawakilishi wakazi wa Umoja wa Mataifa nchini Côte d'Ivoire na Liberia.
Côte d'Ivoire imekuwa mwanachama asiyewa kudumu kwa Baraza la Usalama tangu kuanza kwa mwaka 2018. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Côte d'Ivoire (UNOCI)ulifunga shughuli zake mwezi Juni mwaka 2017 baada ya miaka 13 tangu kuanzishwa wakati nchi hiyo ikikumbwa na mgogoro kuanzia mwaka 1999 hadi mwkaa 2011. Kumalizika kwa kazi ya UNOCI kukitajwa kama ushindi mkubwa katika ulinzi wa amani wa Umoja wa Matafia.
Akihutubia waandishi wa habari Ijumaa, mwakilishi wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa na kiongozi mwenza wa ujumbe ziarani Leon Kacou Adom, amesema ziara imetoa fursa ya kubadilishana uzoefu na taarifa ikiwemo njia mujarabu za kuondokana kutoka ulinzi wa amani hadi ujenzi wa amani miongoni mwa wawakilishi wan chi wanachama, wawakilishi wa mamlaka wa Côte d'Ivoire na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa kutoka Côte d'Ivoire na Liberia.
Ameongeza kuwa, “wakati operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa ziko njia panda, katika mazingira ya mabadiliko yaliyozinduliwa na Katibu Mkuu António Guterres, ni dhahiri kuwa baraza la usalama ambalo linasimamia ulinzi wa amani na usalama kimataifa, unapaswa kuangazia uzoefu chanya kwa mantiki hiyo, mfano ukiwa ni Côte d'Ivoire na Liberia.
Uchaguzi wa wabunge Machi 10 Guinea Bissau
Wajumbe wa Baraza la Usalama waliwasili Guinea Bissau Ijumaa katika awamu ya pili ya zaira yao Afrika magharibi. Lengo kuu la ziara na kufuatilia hali na kutathmini mchakato wa maazimio ya kutatua mzozo nchini humo
Uchaguzi unatarajiwa kufanyika ,Machi 10, 2019 nchini Guinea Bissau na kufuatiwa na uchaguzi wa rais ambapo tarehe itapangwa hapo baadaye.
Wakati wa ziara yao, wajumbe wamekutana na waziri mkuu Aristides Gomes, na naibu mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa David McLachlan-Karr, pamoja na mashirika yanayohusika na ujenzi wa amani nchini Guinea Bissau, kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa kitengo cha Umoja wa Mataifa kuhusu maswala ya kisiasa na ujenzi wa amani.
Aidha ujumbe huo umekutana na spika wa bunge, wakuu wa vyama vya kisiasa, rais wa kamisheni ya kitaifa ya kusimamia uchaguzi na rais wa mahakama kuu na wawakilishi wa mashirika ya kiraia. Halikadhalika wamekutana na rais José Mario Vaz.
Baada ya mikutano mingine Guinea-Bissau, wajumbe wa baraza hilo watarejea jijini New York Jumapili Februari 17 mwa ka huu.