Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, wataalamu wa Umoja wa Mataifa na wale kikanda wamesema ukosefu wa ridhaa katika tendo la ndoa ni lazima iwe ainisho la kitendo cha ubakaji duniani.
Kupitia taarifa yao ya pamoja waliyoitoa hii leo mjini Geneva, Uswisi, wataalamu hao wamesema kuwa kukubalika kwa ainisho hilo kutaziba pengo la sheria za kitaifa na kimataifa kuhusu kitendo cha kubakwa.
Ni kwa mantiki hiyo, wataalamu hao wametaka mataifa duniani kote kukubali ainisho hilo ili kuziba pengo hilo ambalo wamesema ukosefu wake unanyima haki waathirika wa kitendo cha ubakaji.
Wataalamu hao wamesema katika miaka ya hivi karibuni, kupitia kampeni kama vile #MeToo, #TimesUp, #Niunamenos, #NotOneMore, na nyinginezo, manusura wa ubakaji wamepaza sauti zao wakiangazia upungufu huo katika ainisho la kitendo kubakwa.
Wamesisitiza kuwa ubakaji ni kitendo ambacho mara nyingi hakiripotiwi na hata kinaporitiwa, wahusika hawashtakiwi, na hii ni kutokana na masuala kadhaa ikiwemo misimamo iliyopitwa na wakati kuhusu jinsia na mifumo ya haki ambayo ainisho lao la kubakwa ni pale tu nguvu inapotumika.
Halikadhalika wamesema mamlaka na udhibiti vinaendelea kujenga mazingira ya kijamii ambamo kwayo ukatili kama ubakaji unaendelea kuonekana kitu cha kawaida sambamba na kupunguza thamani ya wanawake kwenye jamii.
"Tunapoangazia siku zijazo, na ili kuweza kushughulikia kitendo hiki na madhara yake ya kutisha kwa wanawake na haki zao za kibinadamu hatua za dharura lazima zichukuliwe na serikali, mashirika ya kiraia na yale ya kimataifa na mifumo ya ufuatiliaji,”wamesema wataalamu hao.
Wamehitimisha kwa kutaka jamii iendelee kuhoji mifumo ya kijamii iliyopitwa na wakati ambayo inaendelea kupigia chepuo ubakaji sambamba na kuwapatia msaada wanawake ambao wako tayari kupaza sauti dhidi ya kitendo hicho.