51Թ

Ubaguzi wa kirangi katika kutibu COVID-19 ukome -Bachelet

Get monthly
e-newsletter

Ubaguzi wa kirangi katika kutibu COVID-19 ukome -Bachelet

UN News
4 June 2020
By: 
Mama na mwanawe wakiwa hospitalini nchini Colombia akati huu wa janga la COVID-19
PAHO
Mama na mwanawe wakiwa hospitalini nchini Colombia akati huu wa janga la COVID-19

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu kwenye Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ametaka hatua za dharura zichukuliwe ili kukabiliana na ukosefu wa usawa kwenye jamii unaosababisha ubaguzi katika utoaji wa huduma dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona au

Taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi na ofisi ya Kamishna huyo imetaja nchini Marekani ambako raia wenye asili ya Afrika wanashindwa kupata huduma ilhali huko Uingereza, Ufaransa, Brazil hali inakumba pia watu wa makundi madogo.

Amesema nchini Marekani, kiwango cha vifo kwa wamarekani wenye asili ya Afrika ni maradufu zaidi ya raia wa rangi nyingine, ilihali huko Uingereza, takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha vifo kwa weusi, wapakistani na wabangladesh kutokana na COVID-19, ni mara mbili kuliko vifo vya weupe.

Bi. Bachelet amesema ingawa mjadala ni mkubwa kuhusu athari za COVID-19 kwa makundi madogo, cha kusikitisha, haiko dhahiri ni nini kinafanyika kusaka suluhu.

Ni kwa mantiki hiyo anasema kuwa, “hatua za dharura zinahitajika kuchukuliwa na serikali kama vile kupatia kipaumbele upimaji, ufuatiliaji, upatiaji wa huduma za afya na taarifa kwa jamii hizo za wachache.”

Amesisitiza kuwa pamoja na hatua hizo ni lazima kuwa na upembuzi wa kina na kushughulikia ukosefu wa usawa kwenye sekta ya kiuchumi kwa sababu, “watu hao wa makundi madogo ndio pia wako wengi kwenye ajira zilizo hatari, ikiwemo sekta za usafiri, afya na usafi.”

Ameongeza kuwa,virusi hivi vinafichua ukosefu wa usawa ambao kwa muda mrefu umepuuzwa. Nchini Marekani, maandamano yaliyochochewa na kuuawa kwa mmarekani mweusi George Floyd, yanaonesha siyo tu ghasia dhidi ya watu weusi, bali pia ukosefu wa usawa kwenye afya, elimu, ajira na ubaguzi wa rangi ulioota mizizi.”

Ametamatisha akisema kuwa, “vita dhidi ya COVID-19, haiwezi kufanikiwa iwapo serikali zitapinga kutambua uwepo wa ukosefu wa usawa katika kutokomeza janga hilo. Juhudi za kutokomeza na kupona janga hili zitafanikiwa iwapo kila mtu atakuwa na haki ya uhai na afya yake inalindwa bila kubaguliwa.”