51Թ

Kupambana na COVID-19 ni mchango wangu kwa nchi yangu

Get monthly
e-newsletter

Kupambana na COVID-19 ni mchango wangu kwa nchi yangu

-Dkt. Alison Amarachukwu Karen (Nijeria)
Africa Renewal
21 May 2020
Dr. Alison Amarachukwu Karen (Nigeria)
Dkt. Alison Amarachukwu Karen (Nijeria)

Tufahamishe kidogo kukuhusu?

Jina langu ni Dkt. Allison Amarachukwu Karen, kutoka Jimbo la Imo nchini Nijeria. Nina umri wa miaka 32 nafanya kazi na Shirika la Kimataifa la SOS katika eneo la Jimbo la Ogun. Mimi ni mpenzi wa mazoezi ya kimwili na mfanyabiashara.

Je, umekuwa ukifanya kazi kama mhudumu wa afya kwa muda gani?

Nimekuwa mfanyakazi wa afya kwa miaka saba sasa. Nilifuzu kutoka Chuo Kikuu cha Port Harcourt na kufanya mazoezi ya kazi katika Hospitali ya Mafunzo ya Chuo Kikuu cha Port Harcourt.

Kinachofurahisha ni kuwa sikutaka kuwa daktari nilipokuwa mtoto. Nilitaka kusomea Kiingereza na kukifundisha, lakini wazazi wangu hawakutaka. Nina ndugu pacha na mama yangu alisema mmoja wetu anapaswa kuwa daktari na ndivyo walinielekeza kwa njia hiyo. Mwanzoni, nilijaribu kuasi lakini nashukuru walisimama kidete. Nilipokuwa nikikua, nilikuwa nataka kuwatunza watu, kuwafanya watu wajisikie vizuri na kwa njia hiyo, niligundua kuwa naweza kufanya hivyo katika udaktari vilevile. Kwa hiyo, nilipenda udaktari na ndiyo nikajipata hapa leo.

Je, una hofu au majuto yoyote kufikia sasa?

La. Nitakuwa nadanganya nikikwambia kuwa nina majuto yoyote. Lakini, hata hivyo, nina hofu. Hofu yangu kuu ni kutofikia uwezo wangu kamili. Hiyo ndiyo inanichochea kutia bidii katika kazi yangu.

Je, unasaidiaje nchi yako kupambana na COVID-19?

Sikujua ningegundua kisa cha kwanza cha COVID-19 nchini Nijeria, lakini nadhani hiyo ni moja ya michango yangu kwenye vita hivi.

Kama hatua ya tahadhari baada ya utambuzi, ilinibidi kujitenga na kutoenda kazini kwa muda. Kwa sababu ya hatua za kufungiwa, sijaweza kusafiri kutoka jimbo moja kwenda lingine. Ninajaribu kutoa huduma za matibabu za bure na ushauri kwa watu walio karibu nami na pia natumia mitandao yangu ya kijamii kutoa habari sahihi juu ya hatua za kuzuia na kinga kama ilivyo kwenye miongozo na taratibu zilizowekwa na viongozi wetu wa afya.

Twambie zaidi kuhusu wakati ulipomgundua mgonjwa wa kwanza wa COVID-19 nchini Nijeria. Ni nini kilikufanya kufikia hitimisho hilo?

Naam, siku hiyo Februari 26 2020 ilikuwa kama siku nyingine yoyote kazini. Kwa hakika, hakukuwa na kazi nyingi. Nilitazamia kwenda nyumbani, kula chakula kizuri na kulala. Mambo hayakutokea hivyo. Takriban dakika 28 kabla ya zamu yangu kukamilika na kuondoka, mgonjwa huyo wa kwanza akaingia ofisini mwangu. Alilalamikia joto jingi, maumivu ya kichwa, uchovu na maumivu ya misuli. Kwa kuchukua historia zaidi, nikagundua kuwa alikuwa nchini Nijeria kwa siku mbili tu. Niliwazia kwamba kama hii ilikuwa mara yake ya kwanza nchini Nijeria basi haiwezi kuwa kisa cha ugonjwa wa malaria na haikuwa uchovu wa joto tu, kwa sababu niligundua kuwa hata baada ya kukaa kwa muda katika ofisi yangu iliyo na hewa isiyo na joto, joto mwilini wake lilizidi kuwa mbaya.

Nini lipi lilikuwa likiendelea akilini mwako wakati huo?

Kwa bahati nzuri, timu yangu nami tulipokea mafundisho yaliyosasishwa kuhusu COVID-19 siku mbili zilizotangulia kufika kwa mgonjwa yule kwenye kituo. Kwa ufahamu huu, nilijua kuwa kilichokuwa mbele yangu kinaweza kuwa kisa cha COVID-19, hata ingawa mgonjwa hakuwasilisha dalili za kawaida za ugonjwa huo - hakuwa na kikohozi, hakuumwa na koo na hakuwa na shida kupumua. Hakutoa historia yoyote kuhusu mtagusano wa awali nilipouliza. Nilikuwa na shuku kuu na nikaamua kuwa ni bora kukosea kwa upande wa tahadhari na nikaagiza kuwa atengwa na kupimwa.

Je, ulimwambia kilichokuwa kinaendelea?

Nilimwambia kwa upole: ''Nadhani unaugua ugonjwa huu ...'' Nilimpatia barakoa na kumjulisha kuwa nitamtenga. Alishirikiana vizuri. Kwa haraka nilinawa mikono yangu na kuvaa barakoa kabla ya kuwasilisha kisa hicho kwa Mkurugenzi wa Matibabu wa Shirika la Kimataifa la SOS, ambaye aliwajulisha viongozi wa afya wanaohusika. Mgonjwa alitengwa na kuhamishiwa Kituo cha Magonjwa ya Kuambukiza huko Lagos asubuhi iliyofuata ambapo alithibitishwa kuwa na COVID-19.

Je, wafanyakazi wenza walisemaje?

Nilipowaambia wenzangu kuwa huenda tuna kisa cha COVID-19, walikuwa na wasiwasi sana. Tulisafisha eneo hilo kwa viua vijidudu sote tuliomhudumia mgonjwa huyo tuliingia karantini kwa siku 14 kama hatua ya tahadhari.

Je, COVID-19 inakutisha?

Ndiyo. Inanitisha kwa sababu inaenea kwa haraka sana na hata ingawa ulimwengu mzima unapambana nayo - wanasayansi, makampuni makubwa, watu werevu - bado hakuna tiba inayojulikana na chanjo itachukua muda kupatikana. Lakini bado ninahitaji kufanya kazi yangu kwa sababu, kando na kiapo nilichokula, ninapenda sana kuwatunza wengine.

Je, nini inakufanya kuzidi kuendelea?

Wapendwa wangu – wazazi wangu na kaka zangu. Huu ndio mchango wangu; Sina pesa ya kutoa hivyo hili ndilo naweza kufanya. Najua mwishowe tutalishinda janga hili. Ndio kweli wakati ni mgumu kwa sasa na unaweza kuwa mgumu kwa watu wengine kuliko wengine lakini ni lazima tuzidi kuwa na matumaini! Kuna mwanga mwishowe. Wazazi wangu hunihimiza sana; mama yangu hupiga simu kuniombea na dada yangu hunijali. Haya ndiyo hunifanya kuendelea, hata wakati naogopa.

Je, ulifanikiwa vipi wakati wa karantini?

Nilitumia muda huo kusoma, kufanya kozi mtandaoni, mazoezi na kutazama filamu. Nilikuwa na msaada kutoka kwa familia, marafiki na mwajiri wangu.

Nchi tofauti zimepitisha mikakati tofauti ya kupambana na COVID-19. Kwa mtazamo wako ni mkakati gani uliofanikiwa katika mapambano haya na gani haukufaulu?

Hatua za kuzuia kama kutumia vifaa namavazi ya kujikinga binafsi (PPE), barakoa, kukaa mbali na wengine, kunawa mikono vizuri, adabu ya kupumua na hatua za kufungiwa zimefanya kazi. Kile ambacho hakijafanya kazi ni uvumi, uwongo na taarifa potofu kuhusu gonjwa hili. Nadhani kuchukua hatua iliyogatuliwa kupambana na COVID-19 kutakuwa na athari zaidi. Baadhi ya nchi zinaitekeleza sasa, kuimarisha kutafuta waliotagusana na wagonjwa, udhibiti wa visa, kushirikisha jamii, kuwafundisha vijana na kuwashirikisha.

Kwa mfano, Nijeria imeimarisha uwezo wake wa kupima kwa kuanzisha maabara kadhaa. Mwanzoni, ilitubidi kupeleka sampuli katika maabara kuu kuzipima lakini sasa tuna maabara kadhaa na hatuhitaji sasa kusubiri kupata matokeo. Pia, kusambaza habari sahihi, kuwa na mipango ya uhamasishaji, kukuza tabia nzuri za afya, na kusaidiana.

Una ujumbe gani kwa vijana wenzako wa Nijeria na nchi zingine za Afrika?

Tunapaswa kuweka mtazamo mzuri, kudumisha matumaini! Vitu vingi vinaonekana kutokuwa na uhakika sasa na unaweza kuwa na wasiwasi ni jinsi gani vitaendelea. Ndoto na matamanio yoyote uliyo nayo, endelea kuyafanyia kazi. Tutashinda janga hili na tutakapolishinda, unafaa kuwa tayari kuchukua fursa itakayofuata. Sisi, vijana, ndio tutakaoendelea kujenga nchi zetu. Kwa hiyo, tuna urithi wa kulinda. Usikome, endelea na utafika hatimaye.

Je, ungependa kuwaambia nini wafanyakazi wa afya walio kwenye mstari wa mbele kupambana na COVID-19?

Kunaweza kuwa na giza sana na mambo yanatisha sasa na kazi yetu inahitaji kujitolea kwingi. Tunapaswa kuendelea kuweka mioyo yetu kwa kile tunachofanya - kuokoa maisha. Huu ndio wakati wetu wa kuchukua hatua na kusaidiana. Usisahau kujilinda kwa sababu maisha ya wengi yanategemea uhai wako.

Mojawapo ya masuala yanatojitokeza ni suala la unyanyapaa. Je, mawazo yako ni yapi kuhusu haya?

Nimeyashuhudia mwenyewe. Ili kupambana nayo, tunapaswa kuendelea kuelimisha na kuhamasisha watu kuhusu COVID-19. Watu wanapaswa pia kujaribu kuwahurumia wale waliopitia hali hii kwa sababu wamepigana vita vkubwa.

Afrika pia imeshiriki katika kutoa taarifa potofu, ghushi na uongo kuhusu virusi hivi. Je, kwa nini iwe hivyo?

Watu hueneza taarifa ghushi kwa sababu wanaamini kuwa ni ukweli. Kuna haja ya kukagua na kuchunguza ukweli wa taarifa kabla ya kuisambaza. Nenda kwenye wavuti inayofaa ya mamlaka ya afya na upate taarifa sahihi au uulize mfanyakazi wa afya.

Kwenye maeneo ya mbali, au kwa watu ambao hawawezi kutumia mtandao, ushiriki wa jamii ili kuwahamasisha katika lugha zao ni muhimu, ama kwa ushiriki wa moja kwa moja au redio.

Taja njia tatu tunazoweza kutumia kushinda vita hivi?

Kwanza, ulimwengu unapaswa kufanya kazi pamoja kama timu moja kwa sababu tuna lengo moja - kushinda vita dhidi ya COVID-19. Pili, kila mmoja wetu ana mchango wa kutoa kwa kuchukua tahadhari muhimu na kufuata miongozi ya afya na taratibu zilizowekwa. Tatu, kuwa mlinzi wa ndugu yako. Wajali watu wengine, haswa wasiojiweza, wazee, na walio hatarini zaidi. Unaweza kuwa usaidizi mdogo kama kusaidia kwa ununuzi wa mboga au kusambaza habari.

Ujumbe wako wa kuleta matumaini ni upi?

Kama binadamu, sisi ni jasiri kuliko tunavyojua. Tunaweza kufanya chochote tukiweka mawazo yetu kwacho. Kwa hivyo, usikate tamaa, hata hali iwe ngumu namna gani.