Umoja wa Mataifa umesihi nchi za Afrika ambazo zinatarajiwa kuwa na chaguzi zama hizi za janga la ugonjwa wavirusi vya Corona, zitekeleze hatua hiyo ya kidemokrasia ili kusongesha demokrasia na utulivu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema hayo katika ujumbe wake wa siku ya Afrika hii leo Mei 25, akiongeza kuwa, “nasihi wanasiasa kushiriki katika mazungumzi jumuishi na endelevu ya kisiasa na kuondoa mvutano kwenye masuala ya uchaguzi na watekeleza kanuni za kidemokrasia.”
Bwana Guterres ametoa wito huo kwa kutambua kuwa takribani nchi 20 za Afrika zimepanga kwa na uchaguzi mwaka huu, na baadhi yao zimepanga kuahirisha huku akisema kunaweza kuwa na athari katika utulivu na amani.
Katibu Mkuu katika ujumbe wake huo pia amekumbushia wito wake wa kutaka sitisho la mapigano ili kutoa fursa ya kukabili janga laCOVID-19, akipongeza mataifa ambayo tayari yameitikia wito huo.
Amesema vikundi vilivyojihami huko Cameron, Sudan Kusini na Sudan vimeitikia na kutangaza sitisho la mapigano ambapo amesema,“natoa wito kwa vikundi vingine Afrika kufanya hivyo. Naunga mkono pia wito wa nchi za Afrika wa kutaka amani iwepo majumbani na kutokomeza aina zote za ukatili majumbani, ikiwemo ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.”
Kuhusu COVID-19, Katibu Mkuu amesema kuwa ni masikitiko makubwa kuwa maadhimisho ya siku ya Afrika yamekuja wakati wa mapambano na janga la gonjwa hilo.
Hata hivyo amepongeza nchi za Afrika kwa kuonesha uongozi wa kipekee na uratibu dhidi ya Corona.
“Muungano wa Afrika uliunda kikosi kasi na kuandaa mkakati wa kibara na kuteua wajumbe maalum wa kuhamasisha usaidizi wa kimataifa. Baraza la amani na usalama la AU nalo limechukua hatua kukabili madhara ya COVID-19 katika utekelezaji wa makubaliano na hatua za maridhiano,”amesema Bwana Guterres.
Amekumbusha kuwa hivi karibuni amezindua tamko la kisera la jinsi ya kusaidia Afrika kukabili COVID-19, ikiwemo ujumuishaji wa wanawake, vijana na kuweka mundo wa kipekee wa urejeshaji madeni.
Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesema,“katika siku hii ya Afrika, narejelea mshikamano wangu na watu na serikali za Afrika dhidi yaCovid-19na kusongesha fursa kwa wale wauguao waweze kupona haraka.”