Mtaalamumaalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu, Catalina Devandas, hii leo mjini Geneva ameonya kwamba juhudi kidogo sana zimefanywa kuwapa maelekezo na usaidizi unaohitajika, watu wenye ulemavu ili kuwalinda wakati wa mlipuko huu wa ugonjwa waCOVID-19ingawa wengi wao wako katika kundi la wale walioko hatarini zaidi.
“Watu wenye ulemavu wanajihisi kuwa wameachwa nyuma. Hatua kama kujitenga au kukaa umbali kati ya mt una mtu kunaweza kusiwezekane kwa wale ambao wanaishi kwa kutegemea msaada wa watu wengine kula, kuvaa na kuoga. Msaada huu ni wa msingi kwa maisha yao na mataifa yanapaswa kuchukua hatua zaidi za ulinzi wa jamii ili kuhakikisha msaada endelevu katika hali salama hadi mwisho wa janga.”Amesema Bi Devandas.
Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa hatua za makusudi ni muhimu kuwafanya watu wenye ulemavu waweze kupunguza kukutana na watu na hatari ya kuambukizwa. Wanatakiwa kuruhusiwa kufanya kazi kutokea nyumba au kupatiwa likizo za malipo ili kuwahakikishia uhakika wa kipato. Pia ewana familia na wasaidizi wanaweza kutakiwa kuangaliwa ili waweze kuendelea kutoa msaada kwa watu wenye ulemavu katika kipindi hiki chaCOVID-19.
“Uwezekano wa kupata msaada wa kifedha ni muhimu pia ili kupunguza uwezekano wa watu wenye ulemavu na familia zao kuangukia katika hatari zaidi au umaskini. Watu wengi wenye ulemavu wanategemea huduma ambazo zimeahirishwa na wanaweza wasiwe na fedha ya kutosha kuhifadhi vyakula na dawa au kumudu gharama za ziada za kuletewa huduma nyumbani.”Amefafanua.
Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza pia kuwa ni muhimu kampeni kwa umma na taarifa kutoka katika mamlaka za kiafya za nchi, ni lazima zitolewe kwa umma kwa njia ya lugha ya alama na namna ambayo zinaweza kupatikana kwa kila mtu ikiwemo teknolojia ya kidijitali, sauti kuwekewa maandishi, ujumbe mfupi wa simu, lugha rahisi na inayosomeka kirahisi.
“Mashirika ya watu wenye ulemavu yanapaswa kuhusishwa na kuombwa ushauri katika hatua zote za kupambana na COVID-19.”Amehitimisha Bi Devandas.