51Թ

COVID-19 yadhihirisha umuhimu wa misitu kwa binadamu

Get monthly
e-newsletter

COVID-19 yadhihirisha umuhimu wa misitu kwa binadamu

UN News
27 May 2020
By: 
Mamilioni ya watu duniani kote wanategemea misitu kwa ajili ya kipato na chakula
UNEP/Barbara Schneider
Mamilioni ya watu duniani kote wanategemea misitu kwa ajili ya kipato na chakula

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya misitu inataka hatua za dharura zichukuliwe ili kulinda misitu na bayonuai. Wito huo kupitia ripoti hiyo iliyotolewa leo, inazingatia ukweli wa kuwepo kwa kasi kubwa ya ukataji holela wa miti misituni na ukataji miti hovyo.

Ikiwa imechapishwa hii leo ambayo ni siku ya kimataifa ya bayonuwai ya anuwai, ripoti inaonesha kwamba uhifadhi wa bayonuai inategemea zaidi jinsi ambavyo binadamu anatumia misitu duniani.

Ripoti hiyo imeandaliwa kwa pamoja na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa,kwa ushirikiano tena kwa mara ya kwanza na shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa,huku kitengo cha UNEP cha ufuatiliaji wa uhifadhi duniain, WCMC.

Kinachomulikwa kwenye irpoti hiyo ni ekari milioni 420 za misitu ambazo zimeteketea kutokana na ardhi kugeuzwa kwa matumizi mengine tangu mwaka 1990, ijapokuwa,“kiwango cha ukataji misitu kimepungua katika miongo mitatu iliyopita,”imesema taarifa ya FAO iliyotolewa leo katika miji ya Nairobi, Kenya na Roma, Italia.

Hata hivyo ripoti inasema kuwa,“janga la ugonjwa wa virusi vya Corona auCOVID-19, limeibua kwa kasi kubwa umuhimu wa kutunza na kutumia kwa uendelevu mazingira, kwa kutambua kuwa afya ya binadamu ina uhusiano na ustawi wa mfumo anuai.”

Bonde la mto Congo ni msitu wa kitropiki ambao ni wa pili kwa ukubwa duniani. Eneo hili pia ni muhimu katika kuweka utulivu wa bayonuai duniani.
Bonde la mto Congo ni msitu wa kitropiki ambao ni wa pili kwa ukubwa duniani. Eneo hili pia ni muhimu katika kuweka utulivu wa bayonuai duniani.
FAO/Giulio Napolitano

Ripoti inasema kuwa kulinda misitu ni jambo muhimu kwa sababu inahifadhi eneo la bayonuai la dunia mathalani,“aina 60,000 za miti, asilimia 80 ya aina za wanyama wanaohitaji mazingira oevu, asilimia 75 ya aina mbalimbali za ndege na asilimia 68 ya aina za wanyama.”

Ikinukuliwa katika ripoti hiyo, tathmini ya rasilimali za misitu duniani kwa mwaka huu wa 2020, inaonesha kuwa, licha ya kupungua kwa kasi ya ukataji misitu katika muongo uliopita,“takribani ekari milioni 10 za misitu hupotea kila mwaka kwa sababu ya shughuli za kilimo au matumizi mengine ya ardhi.”

Wakizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, QU Dongyu na Mkurugenzi Mtendaij wa UNEP, Inger Andersen, wamesema kuwa,“ukataji miti msituni na uharibifu wa misitu vinaendelea kufanyika katika kasi ya kutisha na hivyo kuchangia katika kutoweka kwa bayonuai.”

Ripoti hiyo ina tathmini ya hali ya juu ya bayonuai ya misitu ikiwemo ramani inayoonesha ni misitu ipi ambayo bado ina rasilimali kubwa ya wanyama na mimea kama vile maeneo ya kaskazini ya Andes na maeneo ya bonde la mto Congo, na pia maeneo ambako rasilimali hizo za wanyama na mimea zimetoweka.

Eneo la misitu linalohifadhiwa na jamii huko Dalaikoro, Fiji. FAO inasema misitu ni muhimu kwa uhai wa binadamu na viumbe wengine.
Eneo la misitu linalohifadhiwa na jamii huko Dalaikoro, Fiji. FAO inasema misitu ni muhimu kwa uhai wa binadamu na viumbe wengine.
FAO/Rudolf Hahn

Uhifadhi na matumizi endelevu

Kutokana na kasi kubwa ya uharibifu na matumizi holela ya misitu, FAO na UNEP ambayo yanajiandaa kuongoza muongo wa kurejesha misitu katika hali yake kuanzia mwakani, yameahidi kusimama kidete kuongeza ushirikiano duniani kulinda rasilimali hiyo adhimu.“Ili kubadili mwelekeo wa ukataji hovyo misitu na kupotea kwa bayonuai, tunahitaji mabadiliko ya jinsi ambavyo tunazalisha na kula chakula,” wamesema QU na Andersen, wakiongeza kuwa,“tunahitaji pia kuhifadhi na kusimamia vizuri misitu na miti katika mfumo unganifu na tunahitaji kurekebisha kile ambacho kimeharibiwa wakati wa harakati za kutunza misitu.”

Ajira na njia za kujipatia kipato

Ripoti inageukia pia suala uhusiano wa misitu na kipato ambapo inasema kuwa, “mamilioni ya watu duniani kote wanategemea misitu kwa ajili chakula na kujipatia kipato.”

Mathalani inasema kuwa zaidi ya fursa milioni 86 za ajira zisizoharibu mazingira zinatokana na misitu. Halikadhalika, kwa watu wale hohehahe, zaidi ya asilimia 90 wanategemea misitu kupata vyakula vya porini, kuni na njia nyingine za kipato. Idadi hiyo inahusisha watu milioni 8 hohehahe wanaotegemea misitu pekee ambao wanaishi Amerika ya Kusini.