51Թ

COVID-19 yakwamisha harakati za kulinda wanyamapori -WWF

Get monthly
e-newsletter

COVID-19 yakwamisha harakati za kulinda wanyamapori -WWF

UN News
11 June 2020
By: 
Tai akiwa kwenye tawi wakati wa dhoruba ya mvua ya masika huko Narrowsburg, New York.
UN Photo/Mark Garten
Tai akiwa kwenye tawi wakati wa dhoruba ya mvua ya masika huko Narrowsburg, New York.

Wakati dunia hii leo ikipaza sauti kuhusu utunzaji wa bayonuai ikiwemo viumbe vilivyomo duniani, nchini Tanzania harakati za kulinda wanyama walio hatarini kutoweka wakiwemo tembo na faru weusi ziko hatarini kutokana na ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19 uliokumba dunia tangu mwezi Machi mwaka huu.

Akihojiwa na Stella Vuzo ambaye ni Afisa Habari wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa, UNIC Dar es salaam nchini Tanzania, Dkt. Severin Kalonga kutoka mfuko wa wanyamapori duniani, WWF nchini humo amesema kuwa,

(Sauti ya Dkt. Severin Kalonga)

“Hatujafanya tathmini ya kutosha lakini athari ipo tukirejea nyuma kwamba kwa nini viumbe hawa wanatoweka. Viumbe hawa tembo, faru kwa sababu wanawindwa kwa ajili ya vipusa, kwa sababu wana thamani. Sasa COVID-19, wafanyakazi wanaokwenda kufanya doria humo ndani sana sana wanapata ruzuku kutokana na fedha za utalii. COVID-19 imesimamisha shughuli za utalii. Hakuna mapato katika taasisi ambazo zinaweza kuwalipa wataalamu wa doria, kwa hiyo imekuwa ni fursa kwa majangili kuweza kufanya uhalifu na kuzidi kuhatarisha maisha ya tembo na faru. Lakini vile vile nchi wahisani nao wamebadilisha pia namna ya kutoa uhifadhi. Kutokana na maradhi hayo, fedha nyingi wamepeleka kwenye afya na kuokoa uchumi wa jamii, siyo katika uhifadhi. Kwa hiyo hali hiyo inafanya juhudi za uhifadhi zishuke kidogo na hivyo majangili wanajinyanyua na kuharibu rasilimali iliyopo,” amesema Dkt. Kalonga

Alipoulizwa juu ya suala kwamba COVID-19 imetokana na wanyama, Dkt. Kalonga amesema kuwa,

(Sauti ya Dkt. Severin Kalonga)

“Ni ukweli usiopingika, na sayansi imehtibitisha hilo kwamba magonjwa ya mlipuko kama COVID-19 yanatokana na wanyama. Lakini watafiti wanafanya kazi usiku na mchana kubaini chanzo ni mnyama gani. Magonjwa mengine tunafahamu ni mnyama gani. Lakini ni wanyama ambao wanaleta maradhi hayo kwa binadamu. Na hii inakuja kwa sababu tunavunja uhusiano uliopo kati ya binadamu na mazingira na uvunjaji wenyewe ni pale tunapokwenda kuharibu makazi ya wanyamapori na pale tunapofanya biashara ya kuwasafirisha kutoka eneo moja kwenda lingine. Hata kufanya biashara ya nyamapori, yote hii inavuruga bayonuai katika ule mshikamano wake. Sasa katika kubadilisha na kuleta ule mchangamano unaweza kukuta kuna maradhi kutoka mnyama mmoja kwenda kwa mwingine, au kwa mnyama kwenda kwa binadamu na kutoka kwa binadamu kwenda kwa binadamu mwingine na hapo tunakuwa na magonjwa ya mlipuko kama COVID-19.”