51Թ

'Wanawake wanafanya vyema katika kujenga amani na umoja’

Get monthly
e-newsletter

'Wanawake wanafanya vyema katika kujenga amani na umoja’

-Okwa Morphy kutoka Nijeria, nahudumu Sudan Kusini
19 May 2020
Jackline Urujeni from Rwanda
-Okwa Morphy kutoka Nijeria, nahudumu Sudan Kusini

Tarehe 29 Mei ndiyo Siku ya Kimataifa ya Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa - siku ya kuwaenzi wafanyakazi wetu wanaovalia sare na wale raia. Tunapoadhimisha miaka 20 ya Azimio 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama, tutawaangazia walinda amani wa kike na kuwasikia wakisimulia hadithi zao kwa maneno yao wenyewe. Mlinda amani wa leo anatoka Rwanda

Tufahamishe kidogo kukuhusu?

Jina langu ni Jackline Urujeni kutoka Rwanda. Umri wangu ni miaka 39, nimeolewa na nina watoto watatu. Nimekuwa afisa wa polisi kwa miaka 19 na niko katika kiwango cha Msimamizi Mkuu.

Unafanyia kazi wapi?

Mimi ni Afisa Kamanda wa Kitengo cha Polisi kilichoundwa na nchi ya Rwanda jijini Juba, Sudan Kusini.

Je, majukumu yako katika misheni ni yapi na siku yako ya kawaida huwa vipi?

Majukumu yangu ni mengi. Kitengo chetu kinajumuisha maafisa wa polisi 160, nusu yao wakiwa wanawake. Napanga na kusimamia kazi yao kila siku. Ninaratibu na kupanga doria ya kujenga ustawi katika mji na katika vituo vya kuwalinda wakimbizi wa ndani. Katika vituo hivi nasimamia malango, usidikizaji wa wahudumu wa kibinadamu, wageni, na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, na kutekeleza shughuli za utafutaji kukamata silaha, dawa za kulevya na vitu vingine vilivyopigwa marufuku katika majengo hayo. Tunashiriki pia katika vikao tofauti vya kuwajenga uwezo na kuongeza uelewa na watu wanaoishi katika vituo vya ulinzi, haswa wanawake.

Je, siku yako ya kawaida huwa namna gani?

Naanza kazi yangu saa 11 asubuhi kwa mazoezi ya kukimbia kilomita 4 angalau mara tatu kwa wiki. Ofisini huwa naongoza kikao saa 1.30 asubuhi ambapo tunakagua yaliyofanyika katika saa 24 zilizopita, kujadili na kusuluhisha shida ambazo zinaweza kutatiza kazi yetu, kupitia majukumu ya siku na kugawa majukumu.

Natenga saa moja kila siku, kawaida kati ya saa 4 na 5 asubuhi, ili kushughulikia kila afisa anayetaka kukutana nami kibinafsi kujadili masuala ya kila aina, kuanzia yale ya kitaalamu hadi ya kibinafsi.

Natumia muda mwingi katika dawati langu, nikifuatilia redio yangu ya kazi na nikisikiliza jinsi shughuli zetu zinavyoendelea na kufanya maamuzi kama ikihitajika.

Je, unatumiaje muda wako wa kibinafsi?

Ninapokuwa na wakati wa kupumzika, napenda kwenda kwenye mazoezi au kuwasiliana na familia yangu nyumbani. Mimi pia hutangamana na wenzangu na kushiriki katika michezo, hafla za kijamii, na michezo mingine ya burudani iliyopangwa kutuchangamsha, kukuza hali ya maadili na ustawi wa akili.

Je, umekuwa mfanyakazi wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa kuanzia lini na ilikuwaje ukawa mmoja?

Nimekuwa hapa Juba tangu mwezi wa Juni 2019, lakini kabla ya kuja Sudan Kusini nilifanya safari yangu ya kwanza kama mlinda amani wa Umoja wa Mataifa jijini Darfur mnano 2016-2017. Nilikuwa nimeshuhudia mateso mengi katika nchi yangu na pia nilitazama na kuvutiwa na jinsi watu binafsi, hususani uongozi wetu wa kitaifa, walifanya kuleta tofauti kubwa, waliibadilisha nchi na kuboresha maisha ya watu wengi. Nilitiwa moyo na vitendo hivyo na nikaamua kuwa nilitaka kutoa mchango wangu kwa kufanya jambo lenye maana kwa wengine. Nikizungumza kama mwanamke, pia nataka kuonyesha jinsi tunaweza kuwa na nguvu na ufanisi katika kujenga amani na umoja.

Je, familia yako na marafiki nyumbani walifikiria nini kuhusu uamuzi wako wa kuondoka nchini mwako na kufanya kazi ya misheni ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani?

Nilipoiambia familia yangu, hawakuweza kuamini. Walishtuka, walichanganyikiwa na hawakufurahia kabisa uamuzi wangu. Ilibidi niwashawishi ili wakubali. Ilinibidi niwaambie "tazama, watu wengi wamefanya kitu kama hiki na kila kitu kimekuwa sawa." Niliwaelezea kuwa naitazama [kwenda kwa misheni ya kulinda amani] kama sehemu ya kazi yangu, na baada ya muda fulani walianza kunielewa. Sasa wanafurahi na wanajivunia kile ninachofanya.

Je, kwa muhtasari, ni mambo gani muhimu yametokea katika misheni yako ya sasa ya kulinda amani:

Ninapenda kuwa naweza kufanya mabadiliko dhahiri katika maisha ya watu, nitakupa mfano. Muda mfupi baada ya kuwasili mnamo Juni 2019, tulipelekwa katika kimoja kati ya vituo vya ulinzi na nikatambua kwamba hakukuwa na vyumba vya kuogea, haswa kwa wasichana na wanawake. Kwa hivyo, mimi na wenzangu tuliamua kuwajengea choo cha shimo. Bado kinatumika hadi leo.

Je, ni vitu gani vitatu unavyopenda zaidi kuhusu misheni hii na nchi unayoitumikia?

Ninafurahia uvumilivu na moyo wa ukaribishaji wa watu wa Sudan Kusini. Licha ya kupitia kipindi kirefu cha migogoro na vurugu, bado wana urafiki na wana uwezo wa kukaa na matumaini. Ninapenda maingiliano yetu na wanawake wakimbizi wa ndani. Kuhisi imani walio nayo kwetu wanawake hawa ni jambo la kipekee sana. Mara nyingi, hawatufikirii kama maafisa wa polisi - sisi ni kama marafiki au dada. Kwa kweli, wengi wao hutuita "dada", na mvulana mmoja huko anasisitiza kuniita 'Mama'.

Je, ni sehemu gani ya kazi yako ambayo ina changamoto zaidi?

Changamoto kubwa ni wakati mlinda-amani mwenza akishambuliwa au kujeruhiwa. Tuko hapa kufanya mema, kwa hivyo mtu anaposhambuliwa hutuweka katika hali ngumu, na hunisikitisha. Unyanyasaji dhidi ya wahudumu wenza ni moja ya sababu (sisi walinda amani), na labda wanawake hasa, lazima tuwe na ujasiri na kuwashirikisha watu tunaowahudumia katika shughuli za ushirika wa jamii. Tukiweza kuingiliana, tunaweza kuteka mioyo yao na akili zao na kufanya kila mtu aelewe kwa nini tuko Sudan Kusini kwa jumla na kwenye sehemu za ulinzi haswa.

Je, unafikiri walinda amani wa kike hutumika kama vielelezo bora kwa watu wa eneo hilo?

Tunachukua jukumu kubwa katika kuhamasisha wasichana na wanawake hapa. Nchi nyingi na tamaduni nyingi za Afrika zinaongozwa na wanaume, na watu wengi, wanaume na wanawake, wakidhani kuwa mwanamke hawezi kuwa afisa wa polisi, hawezi kubeba bidhaa nzito au kutumia bunduki. Wanawake hapa wameniuliza maswali mengi, haswa wanapogundua kuwa mimi ndiye afisa kamanda wa jeshi kubwa la polisi. Wananiuliza: "Unawezaje kuwa kamanda? Je, hakuna wanaume katika nchi yako?" Ninagundua kuwa wasichana na wanawake hapa wanaanza hatua kwa hatua kufahamu haki zao za kuwa kile watakacho. Wanaelewa kuwa wasichana hawapo tu kuolewa na kupata watoto. Tunafungua macho yao kwa uwezekano mpya, kwa chaguzi mpya ambazo wanapaswa kuruhusiwa kufanya.

Je, ungesema nini kwa wanawake wanaowazia kufanya kazi ya kulinda amani?

Ninawahimiza wanawake kila wakati kuwa walinda amani kwa sababu naona kwa macho yangu mwenyewe kuwa tunahitajika na tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli. Kuna vitu katika hali kama hizi ambazo tunaweza kushughulikia ambazo wenzetu wa kiume hawawezi, au watapata shida kufanya, kwa mfano, kupata uaminifu wa wasichana na wanawake walio katika mazingira magumu. Uaminifu huo hutoa habari muhimu, ambayo inatuwezesha kufanya kazi nzuri ya kuwalinda na kuboresha maisha yao.