Wakati janga la mlipuko wa virusi vya Corona auCOVID-19likiendelea kuitikisa dunia na kusababisha athari kubwa ikiwemo kupoteza maisha ya maelfu ya watu, bara la Afrika ambalo japo halina wagonjwa wengi linahitaji msaada ili kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo.
Hayo yameelezwa na mkurugenzi wa shirika la afya dunianikanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti akizungumza na Umoja wa Mataifa na kuongeza kwamba pamoja na changamoto zinazolikabili bara hilo ambalo sasa limefikisha wagonjwa 10,000 wa COVID-19, nchi zinajitahidi kufanya ziwezalo
“Ninatiwa moyo sana na hatua ambazo zimepigwa kwa ujumla na nchi hadi sasa, lakini pia kuhusu uwezo wa upimaji kwa sababu ndio kitovu cha nini wanachotakiwa kufanya, mwezi mmoja na nusu uliopita kulikuwa na maabara mbili tu katika nchi mbili ambazo upimaji ulikuwepo lakini sasa nchi 41 katika kanda ya Afrika zinaweza kupima virusi hivi, hii ni hatua nzuri. “
Ameongeza kuwa nchi za Afrika zimepiga hatua pia katika uchunguzi kwenye maeneo ya kuingia na kutoka ikiwemo viwanja vya ndege na mipakani na pia baadhi ya viongozi na wakuu wa nchi wametambua umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti kudhibiti kuenea kwa mlipuko huo ikiwemo marufuku ya mikusanyiko, kutotembea hovyo , watu kusalia majumbani , kufunga mipaka na kuhakikisha usafi wa kunawa mikono kwa sabuni akitolea mfano Kenya, Afrika kusini na Rwanda.
Hata hivyo Dkt. Moet amesema pamoja na jitihada zinazofanyika bara hilo linahitaji msaada ili kupiga hatua katika baadhi ya maeneo
“Maeneo ambayo bado yanahitaji kupigwa hatua yanajumuisha kuhakikisha kwamba tuna vitu na vifaa katika nchi vya kwanza kuwalinda wahudumu wa afya , vifaa vya kujikinga, kuvipata vifaa hivi, na vifaa vya kupimia maabara ni muhimu sana. Tunakiri kwamba baadhi ya vitu hivi viko nje ya uwezo wa serikali, kimataifa pia kuna changamoto ya soko na baadhi ya vitu hivi ni vigumu kupatikana. Pia kuna haja ya kuimarisha ufuatiliaji kwa kina na uzoefu wetu katika kutoa huduma ni haba tutahitaji kutumia uwezo tulionao kwa njia bora zaidi.”