Ikiwa leo ni siku ya kupinga matumizi ya madawa ya kulevya duniani, tunakwenda nchini Tanzania ambako kituo cha kusaidia waathirika kilichoko jijini Dar es salaam kimesaidia kuwabadili watumiaji wa madawa hayo kuwa wazalishaji katika jamii.
Kituo hicho cha kusaidia waathirika wa madawa ya kulevya au Sober House kilichopo wilaya ya Kigamboni jijini Dar es salaam nchini Tanzania kinaendeshwa na taasisi ya Pili Missana ambapo kimeshanusuru vijana zaidi ya 2,000.
Miongoni mwao ni Ismail Omari ambaye ndoto zake zilitwama baada ya kutumbukia kwenye madawa ya kulevya akisema kuwa, “nimepitia mambo mengi sana katika maharibiko, ikiwemo matatizo na jamii, matatizo na ndugu zangu ikafikia hadi wakanitenga. Niliamua kutafuta ushauri na msaada na nilifika hapa Sober House, nikagonga lango kuu na nikakutana na Pili Missana. Nilimwelezea shida yangu na nilikuwa naomba msaada kwa sababu kwa elimu yangu nilikuwa sifahamu chochote wakati natumia madawa ya kulevya. Vile vile hata haiba yangu haikuwa nzuri maana mtu akiniangalia tu alifahamu kuwa mimi ni muathirika wa madawa ya kulevya."
Ismail anaendelea akisema kuwa,"nilikuwa sifahamu chochote kuhusu madhara ya madawa ya kulevya, lakini baada ya kuingia hapa nilipata elimu, nikapata nafuu. Nilikaa hapa miezi sita, baada ya hapo nikaongezewa mwezi mmoja kwa ajili ya kusaidia waathirika wapya. Nilitakiwa sasa nirejee kwenye jamii kuendelea na maisha, lakini nilikuwa sina uwezo ndio nikaomba nibakie hapa, kwa bahati Bi. Missana anajishughulisha na uzalishaji wa chakula kama hivi na akanipa fursa.”
Kituo hiki kimembadili, kutoka mbomoaji wa jamii hadi mzalishaji akisema kuwa, “hivi sasa mimi ni afisa huduma za masoko na uuzaji wa bidhaa tofauti kama vile viungo vya chai na viungo vya pilau. Na nina uwezo wa kumshawishi mtu na kumpatia elimu kuhusu bidhaa zetu na akaelewa. Vituo vyote nimejifunza hapa kuanzia ujasiriamali hadi mauzo. Kabla ya kufika hapa tulikuwa wabomoaji na si wazalishaji, na sasa tumeweza basi jamii ituunge mkono. Huwa natoka na kwenda kuuza shuleni, vyuoni na kwenye halaiki, kwa siku naweza kupata shilingi Elfu 25, sawa na dola 10."
Kijana mwingine ni Diana Aristidas ambaye anasema kuwa “nilimaliza Chuo, lakini sikuwa na wazo lolote la kufanya biashara. Nilikuwa tu nachezea simu na kutafuta namba za wanaume na kuwauliza tukutane wapi. Lakini baadaye katika kutumia simu nikaona namba ya Bi.Missana, nilimtafuta na kumuomba nikutane naye. Alinipa ushauri na kunisaidia hapa nipo nafanya ujasiriamali. Namshukuru sana”.
Kwa mmiliki wa kituo hiki Pili Missana ambaye pia ana kituo cha ujasiriamali, shughuli za ujasiriamali zinasaidia kuimarisha Sober House akisema kuwa gharama za uendeshaji ni kubwa na iwapo mmiliki hana chanzo kingine cha kipato atakuwa ombaomba. Kwa hiyo anasema, “mimi huenda mitaani na kuangalia vijana wanaotumia madawa na hawana uwezo wa kumudu gharama za Sober house, nawachukua wakishapata nafuu nawapatia stadi za ujasiriamali ambapo baadaye wao wenyewe wanaingia mtaani kuuza bidhaa, na fedha zipatikanazo tunatumia kuendeshea kituo kwa wale wasio na uwezo wa kulipa gharama.”
Amesema kuwa, “kwa mfano kuna kijana mmoja hapa kwa siku anapata faida yake ya dola 5 au mwingine dola 4 kwa hiyo anaweza kutunza kwa mwezi mzima dola 133. Lakini pia kuna wengine wanaenda kuanzisha viwanda vyao, anatoka hapa amejifunza kutengeneza mfano dawa ya kuosha nywele, halafu familia inamuongezea mtaji, kwa hiyo unakuta ameanzisha kiwanda chake mwenyewe kwa kupitia sisi.”
Taasisi ya Missana ilikuwa na vituo vinne lakini sasa vimebakia vitatu kwa sababu idadi ya waathirika nchini Tanzania inapungua kutokana na udhibiti wa upatikanaji wa madawa kama vile afyuni na kokeni. Hata hivyo Bi. Missana ametoa ombi kwa walima bangi akisema kuwa, “dawa za kulevya kutoka nje zimepungua sana lakini hapa hapa nyumbani kuna watanzania wenzetu wasio waaminifu ambao wanalima bangi kwa kificho majumbani mwao. Wanajipatia kipato lakini wanaharibu watoto wa wenzao. Kwa nini wasilime mazao mengine ambayo japo watapata kipato kidogo lakini watakuwa na amani. Tuonee huruma kizazi chetu.”