Umoja wa Mataifa unashirikiana kwa karibu na serikali ya Kenya kusaidia kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona, auCOVID-19.
Na Siddharth Chatterjee, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya
Idadi ya wagonjwa wa virusi vya Corona nchini Kenya hadi tarehe 19 mwezi huu wa Machi ilikuwa ni watano baada ya wagonjwa hao kuthibitishwa na serikali. Rais Uhuru Kenyatta ametangaza hatua za kujikinga ili kuepusha kusambaa kwa virusi hivyo.
Miezi mitatu tangu mlipuko wa COVID-19, masoko ya fedha yameporomoka na mfumo wa usambazaji wa bidhaa duniani imevurugika. Duniani kote, wanunuzi wamepagawa na wamenunua kutoka madukani daw azote za kutakasa mikono, sabuni na vyakula vya kusindikwa,ikiwa ni maandalizi iwapo kutakuwepo na zuio la kutotoka nje ya nyumba.
Ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kuwa ‘tunapopambana na virusi hvi, katu tusikubali hofu isambae’ ni hoja ya ukweli kabisa. Na watu nchini Kenya wanaweza kutegemea timu ya Umoja wa Mataifa nchini humu kama mdau katika vita hivyo.
Majanga ya magonjwa duniani, ni tishio jipya la ubinadamu
Majanga ya magonjwa duniani ni tishio jipya kwa ubinadamu. Idadi ya magonjwa mapya kwa kila muongo imeongezeka mara nne katika kipindi cha miaka 60 iliyopita, na tangu mwaka 1980, idadi ya milipuko kila mwaka imeongezeka mara tatu.
Mambo kama vile mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la idadi ya watu na ongezeko la safari vimefanya binadamu kuwa hatarini zaidi hivi sasa kuliko ilivyokuwa miaka 100 iliyopita. Maambukizi katika kona moja ya dunia yanaweza kufika katika kona nyingine ya mbali ya dunia ndani ya siku moja.
Katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, kuna hofu Dhahiri kabisa iwapo mifumo ya afya inaweza kuhimili. Mifumo mingi ya afya bado haijajiandaa vya kutosha na haina vifaa vya kutosha kuchukua hatua sahihi kwa afya umma, ikiwemo usimamizi, ufuatiliaji, kuhakikisha hakuna mikaribiano baina ya watu, udhibiti wa safari na kuelimisha umma kuhusu usafi wa mikono na kujikinga wakati wa kupiga chafya au kukohoa.
Hizi ni hatua za msingi ambazo zinaweza kuchelewesha kuenea kwa maambukizi na kupunguza shinikizo kwa hospitali, na hata kama kunatafutwa suluhu nyingine kama vile vifaa vya kujikinga, vivuta hewa, oksijeni na vifaa vya kupima magonjwa.
Kwa nchi za Afrika na maeneo mengine ambako rasilimali ni finyu, ugonjwa wa Corona ambao haufahamiki vilivyo, ni changamoto inayohitaji hatua za jamii nzima. Wakati sayansi inatangeneza vifaa vya kupimia na italeta hatimaye chanjo, hatua fanisi zaidi na ya haraka ni kutegemea zaidi hatua rahisi tunazoweza kuchukua wenyewe badala ya kutegemea zile za kitabibu au dawa.
Kupunguza maambukizi ya COVID-19 kunaweza kusaidiwa pia na uwepo wa taarifa sahihi. Kuongeza hofu miongoni mwa jamii kunachochewa na kushindwa kuchuja ukweli kutoka kwenye uvumi na taarifa zisizo sahihi. Tatizo moja la zama za mitandao ya kijamii na uandisih wa kijamii ni kwamba vinapatia jukwaa kwa kila mtu na kuhatarisha kuwa kila mtu mwenye mawazo ni mtaalamu. Katika mazingira kama haya, simulizi ya ukweli na yenye misingi ya kisayansi ni vigumu sana kudumu.
UN inashirikiana na serikali ya Kenya
Kukabiliana na COVID-19 kwa kuhakikisha kuwa ni taarifa sahihi tu na miongozo ya kisayansi ndio inashika hatamu, ni jambo muhimu. Ni kwa sababu, Umoja wa Mataifa nchini Kenya inatoa msaada kwenye mawasiliano, ikiwa ni moja ya harakati kwa Wizara ya Afya katika hatua zake za kupongezwa za kudhibiti mlipuko. Kila mtu atanufaika iwapo atasikiliza ushauri kutoka Waziri wa Afya Mutahi Kagwe. Mathalani, amesisitiza umuhimu wa kunawa mikono mara kwa mara na kwa kina. Kunawa mikono kunaokoa Maisha na njia bora ya kujikinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza.
Ijapokuwa vijiumbemaradhi vinabadilika mara milioni kwa kasi kama binadamu, na binadamu wana kinga kidogo au hawana kabisa kinga dhidi ya virusi vipya, uelewa wetu wa wa kisayansi kuhusu hatari za zahma za magonjwa na uwezo wa kubashiri gonjwa lijalo iwapo litatokea ni bora kuliko wakati wowote ule.
Mathalani, inafahamika kuwa, magonjwa mengi mapya ya maambukizi chanzo chake ni wanyama, ikiwemo homa ya SARS kutoka kwa popo na baadhi ya homa ya mafua inatoka kwa ndege. Mambo kama vile kuishi karibu na wanyama hai, uchafu katika maandalizi ya nyama na wanyama wafugwao masokoni, mlundikano, ulaji wa nyama za porini vinaweza kuruhusu vijidudu kuvuka kikwazo cha kuishi kwa mnyama na kuingia kwa binadamu.
Maendeleo ya kisayansi sasa yanatumika kusaka suluhu bora zaidi kama vile chanjo. Kusambaa kwa chanjo kunasaidia kinga kwa binadamu na hata kujenga kinga kwa jamii. Chanjo zinafanya kazi na zimeokoa maisha ya wengi.
Nchi za Afrika zifanye nini?
Nchi za Afrika zinapaswa pia kukabiliana na janga la magonjwa kwa njia rahisi lakini fanisi kama vile kuabini, kupima, kutenga waliobainika wagonjwa na kuhamasisha wananchi kuepuka kusambaza magonjwa.
Kwa kutumia njia rahisi na zenye ukweli wa kisayansi, bara la Afrika linaweza kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi na kupunguza maambukizi. Na kwa familia ya Umoja wa Mataifa nchini Kenya, iko bega kwa began a serikali ya Kenya kukabili COVID-19 kwenye maeneo yote.