51Թ

WHO yaunda mfuko kukabili COVID-19; Ulaya sasa ndio kitovu kipya cha virusi hivyo hatari

Get monthly
e-newsletter

WHO yaunda mfuko kukabili COVID-19; Ulaya sasa ndio kitovu kipya cha virusi hivyo hatari

UN News
17 March 2020
By: 
Kuosha mikono kwa sekunde 20 kunahamasishwa kama hatua za kukabiliana na virusi vya corona COVID-2019
UN Photo/Loey Felipe
Kuosha mikono kwa sekunde 20 kunahamasishwa kama hatua za kukabiliana na virusi vya corona COVID-2019

Ulaya sasa ndio kitovu kipya cha zahma ya mlipuko wa virusi vya Corona, amesema leo Ijumaa mkurugenzi mkuu wa shirika la afya ulimwenguni WHO Dkt. Tedros Adhamon Ghebreyesus.

“Ulaya hivi sasa ndio kitovu cha zahma ya COVID-19 kukiwa na visa vingi na vifo vilivyoripotiwa kuliko sehemu zingine zote kwa pamoja duniani ukiacha China.”

Dkt. Tedross ameyasema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi na kusisitiza kwamba idadi ya visa vipya vinavyoripotiwa kila siku ni kubwa kuliko ile iliyoripotiwa na China wakati wa kiwango cha juu kabisa cha maambukizi.

Tangu Desemba zaidi ya visa 132,536 vimeripotiwa katika nchi 123 kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa nahii leo“watu 5000 wamepoteza maisha kutokana na virusi hivyo, na 3173 kati yao wamekuwa nchini China ambako visa hivi sasa ni 80,981 na watu wengine zaidi ya 500 wamekufa nchini Iran.”

Idadi ya visa

Dkt. Tedros ameongeza kuwa lakini miongoni mwa nchi kumi zilizoathirika zaidi na virusi hivyo nusu yake ziko Ulaya na katika bara hilo Italia ndio inayoongoza kwa visa vingi, hadi sasa imeripoti visa 15,000 na vifo 1,016.

Inafuatiwa na Ufaransa yenye visa 2,860 na Ujerumani visa 2369. Na Uswisi inahitimisha orodha ya nchi 10 zilizathirika Zaidi ikiwa na jumla ya visa 858.

WHO imezitaka nchi kuchukua mtazamo wa kimataifa katika kukabiliana na janga hili, sio upimaji peke yake, sio kutafuta tu watu waliokutana na waathirika, sio tu kuweka karantini, na kujitenga katija jamii, badala yake fanya kila kitu amesema Dkt. Tedros, “uzoefu wa China, Korea Kusini, Singapore miongoni mwa nchi nyingine unaonyesha bayana kwamba upimaji wa kina, kufuatilia watu waliokutana na waathirika pamoja na watu kujitenga katika jamii, ikiwemo kuzihamasisha jamii kuchukua tahadhari kwa pamoja hatua hizi zinaweza kuzuia maambukizi na kuokoa maisha.”

Ni kosa la jinai kwa nchi kudhani iko salama

Mkuu huyo wa WHO amezionya nchi kutofikiri kwamba “janga hili haliwezi kuwakumba” akisema “kila nchi ambayo inafikiria zahma inayowakabili nchi zingine kutokana na virusi vya Corona ni kwa ajili ya nchi hizo tu na janga hilo haliwezi kuwakumba wao basi wanafanya kosa kubwa la jinai, kwani virusi hivi vinaweza kumpata yeyote na katika nchi yoyote.”

Ameongeza kuwa kila mtu anapaswa kujua dalili za COVID-19 na jinsi ya kujilinda na kuwalinda wengine . “Kuna hatua rahisi za kuchukua ambazo wote tunaweza kuzifanya ili kupunguza hatari ya maambukizi kwetu na kwa wenzetu wanaotuzunguka mfano “nawa mikono kila wakati kwa kutumia dawa za kutakasa mikono, au sabuni na maji.”

Vita hivi dhidi ya COVID-19 ameongeza vinahusisha kuvibaini, kulinda na kutibu, kwani huwezi kupambana na virusi hivyo kama hujui viliko hivyo ni muhimu “kuvibaini, kutenga, kupima na kutibu kila kisa ili kuvunja mzunguko wa maambukizi kwani kila kisa kinachobainika na kutibiwa kinasaidia kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo.”