Janga la ugonjwa wa virusi vya Corona,COVID-19likiendelea, wanawake wanaendelea kupata ujauzito na watoto wanazaliwa huku wakunga wakiweka maisha yao hatarini kuokoa mama na mtoto.
Ni kauli ya Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu ,, Nathalie Kanem, aliyotoa leo siku ya wakunga duniani.
Amesema kuwa“majanga hayazuii watoto kuzaliwa, na pia hayazuii wakunga kufanya kazi zao. Wanafanya kazi bila kuchoka duniani kote, wakiwa mstari wa mbele katika wodi za wazazi, vituo vya afya, nyumbani kwa wajawazito ili kuokoa mama na mtoto.”
Bi.Kanem ameongeza kuwa katika mataifa mengi yaliyokumbwa na COVID-19, wakunga wengi wanafariki dunia kutokana na ukosefu wa vifaa vya kujikinga, PPE sambamba na ukosefu wa kuungwa mkono.
“Wakunga wengi katika vituo vya afya, wanatumwa kwenda kutoa huduma dhidi ya virusi vya Corona na hii huacha wanawake wajawazito bila huduma za kuokoa maisha yao wakati wanapokaribia kujifungua. Afya ya wajawazito na watoto wachanga lazima ipatiwe kipaumbele kama sehemu ya mpango mzima wa kushughulikia janga la COVID-19,”amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNFPA.
UNFPA hata hivyo imesema inapongeza kazi za wakunga na kuahidi kusimama nao kidete wakati huu wa janga la Corona kwa kushirikiana na serikali.
Shirika hilo pia limemulika umuhimu wa wakunga kama uti wa mgongo wa mifumo ya afya katika kuzalisha watoto na zaidi ya yote kusaidia kulinda haki ya kupata huduma ya afya ya uzazi na haki za wanawake popote ulimwenguni.
“Katika nchi ambazo haki za afya ya uzazi, kuchagua kuwa na mtoto au la bado ziko kwenye vitisho au zinahojiwa, wakunga wanazungumzia jinsi ya kuzuia vifo vya wajawazito vinavyoweza kuepukika na ukosefu wa huduma za uzazi wa mpango. Wao ndio wanafichua pindi kuna hatari ya ukatili wa kijinsia au vitendo hatarishi kama vile ukeketeji,”amesema Bi. Kanem.
Ni kwa mantiki hiyo amesema kuwa hivi sasa kuliko wakati wowote ni lazima kutambua wakunga kama mabingwa wa afya na haki za afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana.
Hata hivyo ametaja mambo matatu ya kufanikisha mwaka huu wa 2020 ambao umeteuliwa kuwa mwaka wa wakunga na wauguzi.
Mosi ni kuonesha kuunga mkono kwa kutambua na kuelimisha watu wengine khusu dhima yao katika kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga akisema kuwa, bila wakunga, watoto wengi na wanawake watakufa kutokana na magonjwa yanayozuilika wakati wa kujifungua au majanga.
Pili ni kusherehekea mafanikio ya wakunga yatokanayo na kuimarisha afya ya uzazi na tatu kuwapatia motisha kwa kupitisha sera za kuwezesha kuitambua fani yao na umuhimu wake kwenye jamii.