Utafiti mpya uliofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya ukimwi UNAIDS, umeonyesha uwezekano wa athariza janga la corona au COVID-19 katika nchi za kipato cha chini na cha wastani kote duniani katika upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya ukimwi au ARV’s.
Matokeo ya utafiti huo yaliyotolewa leo na UNAIDS yamebaini kwamba hatua za watu kusalia majumbani na mipaka kufungwa kwa ajili ya kuzuia kuenea kwa COVID-19 zinaleta changamoto kubwa katika uzalishaji wa dawa hizo na usambazaji wake, na hatimaye kuweza kusababisha kuongezeka kwa gharama na matatizo ya upatikanaji wake ikiwemo kwisha kwa akiba ya dawa katika miezi miwili ijayo.
Akizungumzia changamoto hii mkurugenzi mtendaji wa UNAIDS Winnie Byanyima amesema “Ni muhimu sana kwa nchi kuweka mipango haraka hivi sasa ili kuzuia uwezekano wa hatari kuongezeka hasa bei na upatikanaji wa dawa hizo.Natoa wito kwa nchi zote na wanunuzi wa dawa za VVU kuchukua hatua muafaka ili kuhakikisha kwamba kila mtu ambaye yuko katika matibabu hivi sasa anaendelea kupata matibabu hayo kwa ajili yakuokoa maisha na kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya VVU.”
Ameongeza kuwa jumla ya watu milioni 24.5 wamekuwa katika dawa za VVU tangu mwisho wa mwezi Juni mwaka 2019, hivyo mamilioni ya watu watakuwa hatarini, kwanza kwao binafsi na kwa wengine pia kwa kuongeza hatari ya maambukizi ya HIV kama hawatoweza kuendelea kupata matibabu.
UNAIDS imesema utafiti huo wa hivi karibuni umekadiria kwamba usumbufu wa miezi sita tu katika utoaji wa dawa za ARVs katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara pekee unaweza kusababisha vifo 500,000 vya ziada vinavyohusiana na ukimwi.
Uzalishaji wa ARVs umepata changamoto kubwa ikiwemo usafiri wa anga na baharini ambao umeingilia kazi ya kusafirisha malighafi na vifaa vingine vya kuzalisha dawa hizo kwenye makampuni ya madawa kutokana na janga la COVID-19 na hivyo kupunguza uzalishaji na usambazaji wa ARVs.