51Թ

COVID-19 yaingia katika kambi ya Dadaab, Kenya na UNHCR zaimarisha huduma ya afya katika kambi za wakimbizi

Get monthly
e-newsletter

COVID-19 yaingia katika kambi ya Dadaab, Kenya na UNHCR zaimarisha huduma ya afya katika kambi za wakimbizi

UN News
21 May 2020
By: 
Kambini Dadaab
UNHCR
Kambini Dadaab

Baada ya wagonjwa wawili wa virusi vya corona kuthibitishwa katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab nchini Kenya, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR hii leo limetoa taarifa kuwa kwa kushirikiana na mashirika mengine ya kutoa msaada wa kibinadamu pamoja na serikali ya Kenya wanaimarisha mapambano yao dhidi yakatika kambi za wakimbizi nchini humo.

Taarifa hiyo iliyotolewa hii leo mjini Nairobi Kenya na Geneva Uswisi inaeleza kuwa kwa kufuata maelekezo ya serikali ya Kenya, wagonjwa hao wawili waliwekwa katika karantini na kisha kuhamishwa katika vituo vya kujitenga baada ya matokeo ya ugonjwa kupokelewa yakionesha kuwa walikuwa wameambukizwa ugonjwa huo. Timu ya kufuatilia na kushughulikia wagonjwa , inayotoka katika Wizara ya afya ya nchi hiyo imeanzisha ufuatiliaji wa watu wote waliokutana nawagonjwa hao.

inasema haliya msongamano wa watu katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab ambako tayari huduma za afya zimeelemewa, inaleta wasiwasi mkubwa kuhusu mazingira hatarishi kwa zaidi ya wakimbizi 217,000 na jamii wenyeji 320,000 wanaoishi wanaoishi katika kambi n maeneo yanayozunguka kambi.

UNHCR, wadau na mashirika mengine yamekuwa yakiisaidia mpango unaoongozwa na serikali kote nchini Kenya kupunguza hatari na kuzuia kusambaa zaidi kwa virusi katika kambi za wakimbizi.

Katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab, vituo vya afya vimeboreshwa kwa kujenga vituo vya kutenga na kuwaweka karantini wagonjwa na pia kuwapatia watu wengine 955 vitanda. Pia vituo 125 vya kusafishia mikono vimewekwa katika maeneo ya kusambazia vyakula, shule na masoko.

Vituo vya afya vimepatiwa vifaa vya kujikinga (PPE) 68 kwa ajili ya wafanyakazi walioko mstari wa mbele,vikijumuishaglavu 450, barakoa 45,000 na vifaa vinne vya hewa ya Oksijeni.

Makundi yanayoongozwa na wakimbizi yametengeneza barakoa za vitambaa zaidi ya 150,000 ambazo zitakuwa tayari kusambazwa katika siku zijazo. Wahudumu wote wa afya wamepewa mafunzo kuhusu kupambana na COVID-19.

Hivi sasa kuna daktari 18, nesi 150, wahudumu wa kilniki 52, wataalamu wa maabara 11 na wahudumu 336 wa kijamii wa kujitolea wanaofanya kazi katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab.

“Kampeni ya uelewa kuhusu kuzuia COVID-19 umewafikia wakimbizi 200,000 ikiwemo kupitia njia ya redio za kijamii, mabango, vipeperushi, ujumbe wa mtandao wa WhatsApp, mitandao ya kijamii na wavuti ambazo zinaandikwa katika lugha ya Kisomali, Kioromo, Kidinka, Kiswahili, Nuer, Kifaransa, na Kiingereza.”Imeeleza taarifa hiyo ya UNHCR.

UNHCR na shirika la mpango wa chakula duniani, WFP pamoja na wadau wametoa mgao wa chakula na vifaa vya kujisafi kama vile sabuni, vidumu vya kutunzia maji ili kupunguza misongamano mikubwa ya watu.