Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO, leo limetoa ombi la dola milioni 100 zinazohitajika haraka ili kunusurua maisha ya wakulima, wafugaji ,wavuvi na familia zao nchini Yemen.
Akitoa ombi hilo mkurugenzi mkuu wa wa Qu Dongyyu aamesema Yemen hivi sasa ndio mgogoro mkubwa kabisa wa kibinamu duniani ambapo watu milioni 24 sawa na asilimia 80 ya watu wote wa taifa hilo wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi.
Amesema hata kabla ya janga la corona au COVID-19 Yemen ilikuwa kwenye zahma kubwa , karibu watu milioni 16 walikuwa wameathirika na njaa “ Mamilioni ya watu hawawezi kukidhi mahitaji ya msingi ya kila siku, wakulima, wavuvi na wafugaji wameathirika vibaya na vita na kuporomoka kwa uchumi.”
Hivyo bwana Qu amesema ombi hilo la dola milioni 100 ni msaada unaohitajika haraka Yemen ili “kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kuzalisha chakula kwa ajili yao, familia zao na jamii zao na hususan wakati huu wakikabiliana na mlipuko wa nzige wa jangwani na janga la COVID-19.
Amesisitiza kwamba fedha hizo zitasaidia kurejesha maisha ya watu, kuwajengea mnepo na kuhakikisha kwamba mahitaji ya chakula majumbani kwao yanatimizwa.“Ni lazima tuchukue hatua sasa, chondechonde wahisani tunahitaji msaada wenu , hakuna muda wa kusubiri” amesema mkuu huyo wa FAO na kuongeza kuwa lengo ni kuwafikia watu milioni 6 na kuwagawia msaada wa dharura , ikiwemo mbegu, nyenzo, zana, majokofu, maboya ya kuogelea na fedha taslim ili waweze kuendelea na uzalishajiwa chakula, mifugo na uvuvi.