Miongo miwili na nusu tangu mkutano wa kihistoria wa wanawake mjini Beijing, China bado ghasia dhidi ya wanawake na wasichana zimeshamiri na cha ajabu zinakubalika.
Tathmini hiyo imo kwenye ripoti mpya iliyotolewa leo jijini New York, Marekani kabla ya kufanyika kwa mkutano wa 64 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani, CSW64 jijini humo.
Ripoti iliyoandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,, lile la masuala ya wanawake, UN-Women na shirika la Plan International, inaonesha kuwa ingawa idadi ya wasichana wanaoandikishwa shule na kumaliza masomo ni kubwa kuliko wakati wowote, mafanikio hayo hayajaweza kuunda jamii yenye usawa na yenye mazingira yasiyo na katili kwa wasichana.
“Idadi ya wasichana watoro shuleni tangu mwaka 1995 imepungua kwa wasichana milioni 79, yaani wasichana wana fursa zaidi ya kuingia shule ya sekondari kuliko wavulana,”imetanabaisha ripoti hiyo.
Hata hivyo ukatili dhidi ya wanawake na wasichana umeshamiri.“Mathalani mwaka 2016, asilimia 70 ya watu waliosafirishwa kiharamu duniani walikuwa ni wanawake na wasichana, wengi wao wakisafirishwa kwa ajili ya kulazimishwa vitendo vya ngono. Cha kustaajabisha zaidi, msichana mmoja kati ya wasichana 20 wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 19, sawa na wasichana milioni 13 wamebakwa kwenye familia zao, moja ya ukatili mbaya zaidi wa kingono ambao wanawake na wasichana wanakabiliwa nao.”
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore akizungumzia ripoti hiyo amesema kuwa, “miaka 25 iliyopita, serikali duniani zilitoa ahadi kwa ajili ya wanawake na wasichana, lakini zimetekeleza ahadi kidogo tu. Wakati dunia ilizingatia utashi wa kisiasa wa kupeleka wasichana wengi zaidi shuleni, bado ni aibu kuwa imeshindwa kuwapatia stadi na msaada wanaohitaji ili kuunda siyo tu mustakabali wao bali pia kuishi maisha salama na yenye utu.”
Bi. Fore amesema kuwa kupata elimu pekee haitoshi bali lazima kubadili tabia na mitazamo ya watu kwa wasichana.“Usawa wa ukweli utakuwepo pindi wasichana watakuwa salama dhidi ya ukatili na waweze kufurahia haki zao na fursa sawa maishani,”amesema Mkurugenzi Mkuu huyo wa UNICEF.
Ni kwa kuzingatia changamoto hizo wanazokabili wasichana hivi sasa, ripoti hiyo inataka hatua zaidi kwenye maeneo matatu ambapo mosi, kufurahia na kupanua fursa za wasichana wa makabila, vipato na hadhi tofauti kwenye jamii ili wawe waleta mabadiliko na wabunifu wa suluhu za changamoto kwenye jamii zao. Halikadhalika kujumuisha sauti zao, maoni na mawazo kwenye mijadala, majukwaa kuhakikisha kuna michakato ambayo inazingatia jamii, elimu na mustakabali wao.
Pili ni kuongeza uwekezaji kwenye sera na mipango na kuchagiza miundo ambamo kwayo maendeleo yanasongeshwa na wasichana barubaru kwa ajili yao wenyewe ikiwemo kusongesha stadi zao na kutokomeza ghasia kama vile ndoa za umri mdogo na ukeketeji.
Eneo la tatu ni kuongeza uwekezaji kwenye usakaji, uchambuzi na matumizi ya takwimu zilizonyambuliwa kutokana na tafiti kwenye maeneo ambayo hivi sasa hayana taarifa za kutosha. Maeneo hayo ni kama vile ukatili wa kijinsia, stadi zihitajikazo karne hii ya 21 na lishe na afya ya akili kwa barubaru.