51Թ

Hatua ya Malta kuzirejesha boti za wahamiaji baharini inatutia hofu -UN

Get monthly
e-newsletter

Hatua ya Malta kuzirejesha boti za wahamiaji baharini inatutia hofu -UN

UN News
8 May 2020
By: 
Picha ya maktaba inaonesha waokoaji wa kikosi cha wanamaji cha Italia wakiokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediterania
Italian Coastguard/Massimo Sestini
Picha ya maktaba inaonesha waokoaji wa kikosi cha wanamaji cha Italia wakiokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediterania

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa leo imesema inatiwa hofu kubwa na taarifa za serikali ya Malta kuzitaka meli zote za biashara kuzirejesha baharini boti zote zilizofurika wahamiaji na wakimbizi.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa ofisi hiyo Rupert Colville imesema taarifa hizo ni za kusikitisha za kushindwa kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji na badala yake kuratibu hatua za kurejesha boti zao kwenye bahari ya Mediterranea safari ambazo zinaendelea kuwa moja ya zinazokatili maisha ya wahamiaji wengi duniani.

Ameongeza kuwa“pia tunatiwa hofu kwamba boti za uokozi ambazo mara nyingi hufanya doria katika eneo la katikati mwa Mediterranea sasa zimekatazwa kuwasaidia wahamiaji walio katika dhoruba wakati huu ambapo idadi ya wanaojaribu kufanya safari hizo za hatari kutoka Libya kuingia Ulaya umeongezeka sana.”

Amesema kutokana na katazo hilo hivi sasa hakuna boti zozote za uokozi katikati mwa Mediterranea , na pia imedaiwa kwamba sheria na hatua zinatumika ili kuzuia kazi za mashirika ya kibinadamu yasiyo ya kiserikali au NGOs.

Hivyo Rupert Coville amesema“tunatoa wito kwa vikwazo vyote dhidi ya kazi za waokoaji hawa kuondolewa mara moja. Hatua hizo kwa hakika zinayaweka maisha hatarini.”

Ofisi ya haki za binadamu inasema katika miezi mitatu ya kwanzaya mwaka huu tayari kumekuwa na ongezeko mara nne la zafari za wahamiaji kuondoka Libya ukilinganisha na kipindi kama hiki makwa 2019.

Limeongeza kuwa wahamamiaji hawa wanaofanya safari wanamahitaji mbalimbali ya ulinzi chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kimataifa za wakimbizi ikiwemo , kanuni ya kutochukuliwa kama ni wahalifu kanuni ambayo inawalinda wahamiaji wote bila kujali hali yao ya uhamiaji au uomba hifadhi dhidi ya kufukuzwa au kurejeshwa katika mazingira ya hatari. Aprili 9 mwaka huu Italia na Malta wametangaza kwamba bandari zao si salama kwa watu kuingia kutokana na janga la virsi vya corona au COVID-19.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya ofisi ya haki za binadamu hivi sasaa kuna angalau boti 3 zikiwa zimejaa wahamiaji wanaosubiri kushuka nchi kavu. Na tarehe 7 Mei vyombo vya Habari vimeripoti kuwa kundi dogo la watu wazima wahamiaji akiwemo mama mjamzito na Watoto walituhusiwa kutoka katika boti hiyo baada ya serikali ya Malta kufikiria misingi ya kibinadamu.

Wakati huohuo mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL umethibitisha kwamba Aprili 15 mwaka huu boti iliyokuwa na wahamiaji na waomba hifadhi 51 wakiwemo wanawake 8 na watoto watatu ilirejeshwa Libya kutoka Malta.

Hivyo ofisi ya haki za binadamu“inatoa wito wa kusitsha kuzuia na kurejesha boti hizo za wahamiaji Libya, ikisema licha ya janga la COVID-19 operesheni za kuwatafuta na kuokoa watu lazima ziendelee na pia kuwahakikishia usalama wao huku tahadhari ikichukuliwa kuzingatia hatua za kiafya.”