Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula la kilimo FAO limesema limepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya nzige wa jangwani katika eneo la Afrika Mashariki na Yemen lakini limeonya kwamba tishio la nzige hao katika uhakika wa chakula bado ni kubwa.
Katika ripoti ya hatua zilizopigwa nakuhusu vita dhidi ya nzige iliyotolewa leo mjini Roma Italia mkurugenzi mkuu wa FAO Qu Dongyu amesema pamoja na mafanikio hayo, hatua zaidi zinahitaji kufanyika ili kuzuia mgogoro wa uhakika wa chakula kwa sababu msimu wa mvua unaoendelea sio tu kwamba unatoa mazingira mazuri ya maisha kwa wakulima na wafugaji lakini pia ni mazingira muafaka kwa nzige hao kuendelea kuzaana.
Amesisitiza kwamba FAO inaendelea kufuatilia na kudhibiti operesheni za kutokomeza nzige hao licha ya changamoto kuwa iliyotokana na mlipuko wa virusi vya corona au COVID-19 pamoja na changamoto zingine.
Makadirio ya awali ya shirika la FAO yanaonyesha kwamba tani 720,000 za nafaka zinazotosheleza kulisha watu milioni 5 kwa mwaka mzima zimeokolewa katika nchi 10 kutokana na hatua za kuzuia kusambaa kwa nzige wa jangwani na uharibifu wa ekari nyingine nyingi na zaidi ya hapokaya 350,000 za wafugaji zimenusurika na zahma ya nzige hao.
Bwana Dongyu amesema,“mafanikio yetu ni makubwa lakini vita ni vya muda mrefu na havijaisha bado. Watu wengi zaidi wako katika hatari ya kupoteza kila kitu na kuwa katika hatari ya kutokuwa na uhakika wa chakula katika miezi ijayo”.
Pamoja na kwamba nzige hao wametokomezwa kwa kiasi kikubwa amesema wimbi lingine la watoto waliozaliwa wanakomaa na kuwa wakubwa ifikapo Juni wakati ambao ni muhimu sana kwa wakulima Afrika Mashariki wakijiandaa kuvuna mazao yao.
“Tunaweza na ni lazima tuwalinde watu walio katika hatari dhidi ya athari za majanga mbalimbali, vita, mabadiliko ya tabianchi, nzige wa jangwani na COVID-19 ambayo yanahatarisha zaidi uhakika wa chakula. Ili kutimiza lengo hili tunahitaji kuongeza juhudi zaidi na kujikita sio tu katika kudhibiti bali pia kuwasaidia wakulima na wafugaji ili wapitie kipindi hiki kigumu.”Amesema Dongyu.
Nzige wa jangwani wanachukuliwa ni wadudu waharibifu zaidi duniani ambapo wimbi moja kubwa linaweza kusafiri likiwa na jumla ya nzige milioni 80.
Ombi la FAO la fedha za kupambana na nzige lililotolewa mwezi Januari mwaka huu sasa zinasaidia vita dhidi ya wadudu hao Djibout, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania, Uganda na Yemen.