Serikali ya Kenya imeombwa kuwa wakati huu wa janga laisiwafurushe wakazi wa maeneo yasiyo rasmi ya Kariobangi na Ruai na ilinde usalama wa watetezi wa haki za binadamu ambao wanatishiwa usalama wao kutokana na kutetea haki za wakazi hao.
Wataalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za makazi na haki za watetezi wa haki za binadamu wamesema hayo leo kupitia taarifa yao iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.
Balakrishnan Rajagopal, na Mary Lawlor wamesema wito wao unafuatia ripoti ya matumizi ya nguvu ya kuwatoa watu hao kutoka makazi hayo yasiyo rasmi huko kwenye mji mkuu wa Kenya, Nairobi huku watetezi wa haki wakikabiliwa na vitisho vya kutoweshwa.
Wamesema kuwa siyo tu kuharibu nyumba za wakazi hao wa Kariobangi na Ruai bila kuwapatia makazi mbadala ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, bali pia kufanya hivyo wakati huu wa janga la virusi vya Corona auCOVID-19, kunaongeza makali ya madhara ya kiafya na uhai wa maelfu ya wakenya.
Wataalamu hao maalum wamesema pia wana wasiwasi kwa kuwa wameendelea kupokea ripoti mpya za kuendelea kufurushwa kwa wakazi katika siku chache zilizopita licha ya tangazo la serikali kuwa itasitisha ufurushaji huo wakati huu wa janga la Corona.
“Asubuhi ya tarehe 4 mwezi huu wa Mei, licha ya amri ya mahakama iliyotolewa siku iliyotangulia ya kuzuia mamlaka kuendelea na kazi ya kufukuza watu, takribani watu 8,000 walifuruswa kutoka eneo la Kariobangi na nyumba zao kubomolewa,” wamenukuliwa wataalamu hao.
Cha kusikitisha ni kwamba,“serikali ya Kenya ilikuwa imewapatia notisi ya kati ya saa 24 na 48 tena kwa maneno, na haikuwa imechukua hatua zozote kuwapatia chakula, makazi ya muda, huduma za maji na kujisafi na hata fidia yoyote. Maelfu ya watu hivi sasa hawana makazi na wanahitaji msaada wa dharura,” wamesema Bwana Rajagopal na Bi. Lawlor.
Huko Ruai hali ilikuwa vivyo hivyo tarehe 15 mwezi huu ambako zaidi ya watu 1,500 walifurushwa usiku wakati wa amri ya kutotembea hovyo na mvua kubwa.
Wamekumbusha kuwa serikali ya Kenya ina wajibu wa kuzuia mipango zaidi ya kufurusha wakazihao na iwapatie haraka msaada wale ambao tayari wamefukuzwa makao na iweke mpango wa muda mrefu wa kuwapatia mahitaji ya malazi.
Kuhusu watetezi wa haki, wataalamu hao wamemtaja Ruth Mumbi ambaye baada ya kukusanya maoni ya wakazi wa Kariobangi na kutaka wanahabari wapaze vilio vyao, tarehe 12 mwezi huu mtu anayedaiwa kuwa ni afisa wa polisi alimpigia simu na kumtishia kuwa atatowesha asipoacha kutetea haki za waliofurushwa.
Wataalamu hao wameeleza wasiwasi wao kuhusu usalama wa Bi. Mumbi na kuitaka serikali ya Kenya ichunguze vitisho hivyo na hatua zichukuliwe.