Miezi miwili kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Burundi, kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya uchunguzi dhidi ya Burundi, COIB, imetoa ombi kwa jamii ya kimataifa likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na taasisi za kikanda ziungane kulisihi taifa hilo la Maziwa Makuu liache kubinya fursa za kiraia, kisiasa na kidemokrasia.
Kauli hiyo imo kwenye taarifa ya kamisheni hiyo iliyotolewa leo huko mjini Geneva, Uswisi wakati huu ambapo uchaguzi wa rais, wabunge na manispaa unatarajiwa kufanyika mwezi Mei mwaka huu wa 2020.
Kamisheni hiyo imesema fursa hizo za kidemokrasia, kisiasa na kiraia ni haki za msingi za kibinadamu na pia ni vigezo muhimu katika kuhakikisha chaguzi hizo zinakuwa halali, huru na zinafanyika katika mazingira yenye amani.
Wito huo wa Kamisheni hiyo unazingatia ripoti yake kwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa tarehe 9 mwezi huu wa Machi huko Geneva, Uswisi, ya kwamba vigezo 8 hatarishi vya kuweza kusabaisha ukatili Burundi ambavyo vilibainiwa mwaka 2014 na washauri maalum wa Umoja wa Mataifa, bado vipo wakati huu ambapo chaguzi za rais na manispaa zinakaribia.
Mathalani kwa kigezo cha ukosefu wa utulivu kisiasa, kiuchumi na kiusalama, COIB imesema kuwa bado kipo."Wafuasi wa tawi la vijana la chama cha CNDD-FDD liitwalo, Imbonerakure, wanaendelea kufanya mauaji, kutowesha watu,kukamata watu kiholela na kuwasweka rumande, pamoja na kuwatesa, kuwabaka wapinzani wa kisiasa au watu wanaodaiwa kuwa wapinzani wa kisiasa. Wanafamilia wa waathirika hao nao wamekumbwa na ukatili ikiwemo ule wa kingono,"imesema kamisheni hiyo.
Kamisheni imeongeza kuwa hali ya haki za binadamu inazidi kuzorota kutokana na kudoroa kwa uchumi, kigezo kingine hatarishi ambacho kimeathiri Burundi tangu mwaka 2015.
"Hali ya kibinadamu imesalia kuwa ya kutia shaka ambapo warundi 336,000 wamesaka hifadhi nchi jirani na baadhi yao wanarejeshwa katika mazingira ambamo urejeaji wa kihiari bado ni tata,"imeongeza taarifa hiyo.
Vigezo vingine hatarishi vinahusiana na kusambaa kwa mazingira ya ukwepaji sheria dhidi ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na udhaifu wa taasisi za dola katika kuwa na uwezo wa kuzuia ukiukwaji huo.
Ni kwa kuzingatia hali kama hiyo wajumbe wa Kamisheni hiyo wana hofu na wamesisitiza kuwa kufanyika kwa uchaguzi huru na wa haki ni muhimu kuondolewa kwa ubinyaji wa fursa za kiraia, kidemorkasia ya kisiasa.
"Baada ya miaka ya machungu, warundi wana haki ya kuishi kwenye jamii yenye maridhiano na yenye mazingira ya kidemokrasia,"imetamatisha taarifa hiyo.