Nchini Niger, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linashirikiana na viongozi wa kijadi kusaidia kuelimisha jamii ijikinge dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona auCOVID-19, katika taifa hilo ambako tayari kuna wagonjwa 763 na kati yao hao, 38 wamefariki dunia.
Kwenye kitongoji cha Banizoumbou katika mji mkuu wa Niger, Niamey, ChifuYaye Modi Alzouma, anahamasisha wananchi juu ya virusi vya Corona, akisema kuwa hata machifu wamekiri kuwepo kwa gonjwa hilo.
Hatua hii ya Chifu Alzouma ni sehemu ya kampeni zinazoendeshwa kwa ushirikiano nazikijumuisha viongozi wa jadi na wapiga debe mjini Niamey.
Kampeni inalenga kuhamasisha jamii ielewa COVID-19, na izingatie kanuni za kutochangamana, na kuheshimu amri ya dharura ya kutotembea hovyo.
Chifu Alzouma anasema kuwa,
“Tangu kuingia kwa huu ugonjwa huu wa Corona, tumekuwa tukifanya kazi kuongeza uelewa. Tunatuma magari yenye vipaza sauti kwenye makazi ya watu. Niamey ni mji mkubwa, kwa hiyo hatuwezi kutembea mguu kwa mguu. Ni kwa kutumia magari yenye vifaa mahsusi tunaweza kuelimisha watu. Watu wanasikiliza machifu. Machifu ndio wanawaelezea jinsi ya kuchukua hatua. Watu bado wanajaribu kuelewa hali ilivyo. Wakati wa sherehe za ubatizo au harusi, hawakusanyiki kwa sababu ya huu ugonjwa.”
Matumizi ya vipaza sauti vilivyofungwa kwenye magari yanapigiwa chepuo na Harouna Bague ambaye ni mpiga debe.
“Watu wengi hawana televisheni wala radio na si kila mtu anaweza kufuatilia taarifa kupitia vyombo hivyo vya habari. Iwapo watu 5 watatusikiliza, wataweza kusambaza ujumbe huo kwa watu wengine 100 na kadhalika.”