Hii leo dunia ikiwa inaadhimisha siku ya kupambana na ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana, shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana na Virusi Vya UKIMWI, VVU na UKIMWI, UNAIDS limesema mapambano dhidi ya UKIMWI hayatenganishwi na kupigania haki za wanawake na pia mapambano dhidi ya aina zote za ubaguzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Winnie Byanyima akiutangaza ujumbe wa shirika hilo kwa ulimwengu kupitia video, anaanza kwa kueleza namna tatizo la VVU na UKIMWI ambavyo limemgusa kila kila mtu ikiwemo familia yake mwenyewe na hata familia ya Umoja wa Mataifa na kwa hivyo kwa ujumla wao wamepata fundisho la kuwa mapambano dhidi ya UKIMWI hayawezi kutenganishwa na mapambano ya haki za wanawake na mapambano dhidi ya aina nyingine zote za ubaguzi,“UKIMWI unaweza kutokomezwa, lakini unaweza kutokomezwa iwapo tutapambana na ukosefu wa usawa wa kijamii na kiuchumi ambavyo vinaendeleza ugonjwa huo na ikiwa tutachochea zaidi uvumbuzi wa kisayansi kushughulikia mahitaji halisi ya wanawake na wasichana na watu wanaoishi na VVU.”
Akiendelea kufafanua kuhusu ukubwa wa tatizo hilo la UKIMWI na ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana, Bi Byanyima ameeleza kuwa UKIMWI umesalia kuwa ugonjwa unaoongoza kwa kuua wanawake wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 49 na kisha akatoa ushauri,“ili kutokomeza UKIMWI kufikia mwaka 2030, tunatakiwa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na kuhakikisha kuwa wanawake na wasichana wana nafasi sawa ya kupata elimu, afya na ajira.”