Nchini Myanmar mradi wa shirika la kazi duniani, ILO wa kuelimisha kampuni binafsi kuhusu sheria za kazi umeanza kuzaa matunda ambapo sasa wafanyakazi ambao walikuwa wakifanya kazi kwa saa nyingi bila malipo ya ziada sasa wanatambua haki zao na kuna maelewano baina yao na mwajiri.
Mradi huo wa miaka mitatu wa kujenga mahusiano mazuri kazini kwa ajira yenye utu na maendeleo endelevu katika sekta ya ushonaji nguo nchini Myanmar,-GIP, unalenga kupunguza umaskini na kuwajengea uwezo wanawake waliojiriwa kwenye sekta hiyo katika taifa hilo ambalo sasa limefungua milango zaidi tofauti na awali.
Awali hali haikuwa shwari kama asemavyo Shwe Zin Tun ambaye alifika kazini saa 1 asubuhi hadi saa 4 usiku bila malipo ya ziada lakini sasa kuna muda maalum na muda ukizidi wanalipwa posho na kwamba,“awali hatukufahamu chochote kuhusu sheria za kazi na haki zetu kwa hiyo tulipata shida sana. Lakini sasa kiwanda hiki kinatambua sheria na haki za wafanyakazi. TUmefahamu kile tunachopaswa kufahamu na hili ni jambo jema.”
Mafunzo yakiendelea kwenye mji wa Yangon na wafanyakazi wanaulizwa iwapo wanafahamu aina za likizo? Na wanazitaja likizo hizo ikiwemo ile ya uzazi na matibabu..
Wanafundishwa pia kuhusu migogoro ya kazini ile ya maslahi nai le ya haki..
Mshauri wa kiufundi wa mradi huo Catherine Vaillancourt-Laflamme anasema kuwa wanajikita kwenye sheria za kazi ya Myanmar, hifadhi ya kijamii, haki za kujiunga kwenye vyama vya wafanyakazi na kudai maslahi kwa pamoja.
Ei Po Po Thu ni mnufaika wa mafunzo kutoka kiwanda cha mikoba ya wanawake cha Harvey na anasema,,“Nilichojifunza nitawaeleza rafiki zangu hasa wakati wa mapumziko ya chai au mlo wa mchana. Eneo langu la kazi kuna mjamzito ambaye alifikiria kuacha kazi kwa kutofahamu likizo ya uzazi. Leo nimemweleza nilichojifunza na imemsaidia sana.”
Bi.Vaillancourt-Laflamme anatamatisha akisema,"Kwa hiyo mafunzo ni muhimu sana kwa sababu sekta ya ushoni wa nguo ni mwajiri mkubwa wa wasichana nchini Myanmar. Inaeleweka kuwa kutokana na kuhama kwa wafanyakazi kutoka vijijini kwenda mijini, na mabadiliko makubwa ya mfumo wa sheria, kuna umuhimu wa kufundisha wafanyakazi na menejimenti kuhusu sheria ya kazi ya Myanmar, na jinsi ya kuitekeleza.»
Wafanyakazi wanaamini kuwa kuimarika kwa mahusiano kazini kati ya mwajiri na mwajiriwa sambamba na mazingira ya kazi kutaleta ufanisi na tija zaidi katika uzalishaji.