51Թ

Msaada waliotupatia UNFPA umetusaidia kuendeleza huduma za wakunga -Wakunga Tanzania

Get monthly
e-newsletter

Msaada waliotupatia UNFPA umetusaidia kuendeleza huduma za wakunga -Wakunga Tanzania

UN News
6 May 2020
By: 
Mkunga Adelaide Raul kutoka Msumbiji akifurahi na mama baada ya kumzalisha watoto mapacha
UNFPA Mozambique
Mkunga Adelaide Raul kutoka Msumbiji akifurahi na mama baada ya kumzalisha watoto mapacha

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya wauguzi na wakunga , Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la afya WHO umesema mchango wa wahudumu hao wa afya hauna kipimo hasa wakati huu ambao janga la virusi vya corona aulinaitikisa dunia na wao wako msitari wa mbele kupambana nalo. Kaulimbiu ya mwaka huu ni "waunge mkono wauguzi na wakunga".

Nchini Tanzania Chama Cha wakunga TAMA, kimeushukuru Umoja wa Mataifa kupitia shirika la idadi ya watu duniani,kwa kuunga mkono harakati na juhudi za wakunga kuokoa maisha ya mama na mtoto wakati wa uzazi. Rais wa TAMA, Mkunga mbobevu wa miaka mingi, Bi Feddy Mwanga anaanza kwa kueleza kazi kubwa ya chama cha wakunga.

“Kazi kubwa ya Chama cha wakunga Tanzania (TAMA) ni kuelimisha wakunga ili kuwapa stadi stahiki za kuokoa mama na mtoto pale wanapopata matatizo wakati wa ujauzito, kujifungua, mara baada ya kujifungua na kumhudumia mtoto mchanga. Ili tuweze kufanya mafunzo haya tumepata msaada wa kifedha na vifaa kutoka kwa mashirika mbalimbali. Nitambue msaada mkubwa kabisa ambao tumeupata kutoka kwa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani, UNFPA ambao wamekuwa mstari wa mbele wa kutupa msaada wa kifedha na vifaa vya mafunzo lakini pia wametupa msaada mkubwa wa samani yaani furniture katika ofisi yetu ya makao makuu. Msaada huu umetupa utulivu wakati wa kufanya kazi hasa kwa wakati huu wa janga la virusi vya corona tunaweza kufanya kazi kwa nafasi inayotosheleza ya mtu hadi mtu.”

Bi Mwanga anasema kwa kuzingatia kuwa mkunga mtaalamu ana uwezo wa kutoa huduma hadi asilimia 87 ya kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi, wameendelea kutoa huduma hata wakati huu wa changamoto ya COVID-19

“Wakunga tumeendelea kutoa huduma yetu na tumeendelea kuhakikisha kwamba wakina mama wanajifungua salama na kama tunavyoona vifo vitokanazo na uzazi vinapungua japo sio sana lakini vinapungua. Tumefanya uhamasishaji mkubwa katika jamii kuhakikisha akina mama wanajifungulia katika vituo vya afya ambapo wanapata huduma ya matibabu ya kitaalum.Tunafurahia sana kwamba Idada ya akina mama wanaojifungulia katika vituo vya afya imeongezeka kwa kiwango cha kuridhisha kabisa.”