Ugonjwa wa virusi vya Corona auCOVID-19ukiendelea kusambaa barani Afrika, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amependekeza hatua za kisera zakusaidia bara hilo kukabiliana na changamoto zitokanazo na janga hilo ambalo hadi sasa limesababisha vifo vya watu 2500 barani humo.
Guterres ametoa mapendekezo hayo kupitia andiko lake la kisera huku akipongeza jinsi Afrika imechukua hatua haraka akisema kuwa ingawa idadi ya vifo hivi sasa ni ndogo kuliko ilivyodhaniwa , bado kuna mambo mengi yamesalia.
Amesema hatua za kisera anazopendekeza ni muhimu ili kuepusha kutoweka kwa mafanikio yaliyopatikana Affrika ikiweko kuimarisha ustawi wa watu wake, ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kidijitali bila kusahau makubaliano ya eneo la soko huru.
“Janga hili linatishia maendeleo ya Afrika. Litaongeza ukosefu wa usawa uliokuwa umedumu na pia njaa, utapiamlo na hatari ya kupata magonjwa. Tayari, mauzo ya bidhaa kutoka Afrika, utalii na utumaji wa fedha barani humo vinapungua. Ufunguzi wa ukanda wa biashara huru umesogezwa mbele na mamilioni wako hatarini kutumbukia kwenye umaskini,”amesema Guterres.
Katibu Mkuu amesema hatua mbali mbali zikiwemo uratibu wa kikanda zimechukuliwa ikiwemo kutuma wahudumu wa afya, kuimarisha karantini na kuzuia watu kukaa majumbani bila kusahau kufunga mipaka.
Umoja wa Mataifa nao, amesema unaonesha mshikamano kwenye vita dhidi ya COVID-19 kwa kusambaza mamilioni ya vikasha vya uchunguzi wa virusi, mashine za kusaidia wagonjwa kupumua na vifaa vingine kwenye maeneo mbali mbali barani Afrika.
Mapendekezo ya kisera
Hata hivyo amesema bado kuna changamoto na ndio msingi wa andiko lake lenye mapendekezo ya kisera akisema,“tunatoa wito wa hatua za kimataifa kuimarisha mifumo ya afya barani Afrika, kuendeleza usambazaji wa chakula, kuepuka janga la kifedha, kusaidia elimu, kulinda ajira, kuwezesha kaya na biashara kujimudu, kusaidia mapato yaliyopotea ikiwemo kutokana na mauzo ya bidhaa nje.”
Halikadhalika amesema Afrika inapaswa kuwa na uwezo sawa wa kupata chanjo na matibabu yatakayopatikana na kwamba chanjo hiyo inapaswa kuchukuliwa kuwa ni bidhaa ya maslahi ya umma.
Amegusia pia suala la msaada wa fedha akisema kuwa,“nimekuwa natoa wito fungu la kuchangia la kimataifa lenye thamani ya angalau asilimia 10 ya pato la ndani.Kwa Afrika ina maana zaidi ya dola milioni 200 za nyongeza za msaada kutoka jamii ya kimataifa.”
Kuhusumadeni, Katibu Mkuu amesema anaendelea kuchagiza mfumo mahsusi wa madeni, akisema kuwa mfumohuo lazima uangalie nchi zisizo na uwezo wa kulipa madeni, kisha unafuu wa malipo ya madeni na mwisho mfumo mahsusi kwenye masuala ya muundo wa ulipaji madeni ili kuzuia nchi kutumbukia kwenye kushindwa kabisa kulipa deni kwa wakati.
Mapigano yakome, chaguzi zitakuwa fursa ya amani ya kudumu
Amependekeza pia suala la nchi za Afrika kusitisha mapigano na kusisitiza kuwa michakato ya kisiasa na chaguzi katika miezi ijayo itatoa fursa za kipekee katika utulivu na amani.
Hata hivyo ametaka wanawake na vijana wasienguliwe wala kusahaulika kwenye michakato hiyo sambamba na hatua zoote za kujikwamua na madhara ya janga la Corona.
Ametamatisha pendekezo lake akikumbusha kuwa, kumaliza janga barani Afrika ni muhimu katika kulimaliza janga hilo duniani kote.