Volkan Bozkir kutoka Uturuki amechaguliwa kuwa Rais wa mkutano ujao wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kufuatia upigaji kura wa aina yake uliofanyika katika mazingira ya sasa ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 yanayozuia kuchangamana.
Wakiwa wamevalia barakoa na kuepuka kuchangamana, mabalozi wanaowakilisha nchi 192 wanachama wa Umoja wa Mataifa, walipanga mstari kuingia katika ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja huo uliokuwa mtupu ili kupiga kura katika muda uliopangwa.
Akizungumzia mfumo wa upigaji kura kabla ya kazi yenyewe, Rais wa sasa wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Tijjani Muhammad-Bande amesema kuwa “janga la COVID-19 lilipoanza, tulilazimika kufanya kazi katika mazingira ya kipekee ili kukabiliana na changamoto hizi zinazotukabili.”
Amesema kuwa “bila shaka zinawakilisha azma yetu ya kuhakikisha kuendelea kwa kazi muhimu ya Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa Katiba ya chombo hiki muhimu bila kutetereka.”
Sura mpya katika Baraza la Usalama na ECOSOC
Bwana Bozkir, mwanadiplomasia wa muda mrefu na pia mbunge, ataongoza mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambao utaanza mwezi Septemba mwaka huu. Yeye alikuwa mgombea pekee katika nafasi hiyo na katika upigaji kura alipata kura 178 kati ya kura halali 189 zilizopigwa. Kura 3 ziliharibika, ilhali nchi 11 hazikupiga kura kabisa.
Wawakilishi hao wa kudumu pia walipiga kura kuchagua wajumbe wapya 5 wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Baraza la Usalama kwa kawaida lina wajumbe 15 ambapo 5 kati yao , China Urusi, Marekani, Uingereza na Ufaransa ni wajumbe wa kudumu ilhali nchi 10 zinakuwa na ujumbe wa miaka miwili.
Kenya na Djibouti zakwaa kigingi, India kidedea, kura kupigwa tena Alhamisi
Kwa nchi za Afrika na Asia na Pasifiki kulikuwepo na viti viwili vikigombaniwa na India, Kenya na Djibouti ambapo mshindi lazima apate theluthi mbili za kura za wajumbe 192 waliopiga kura, ni India pekee ndio iliibuka kidedea kwa kupata kura 184.
Kenya imepata kura 113 ilhali Djibouti kura 78 hivyo kura zitapigwa tena kesho ili apatikanemshindi.
Canada nayo ilibwagwa katika uchaguzi wa kiti hicho kwa nchi za Ulaya Magharibi na makundi mengine, ambapo ilishindwa kupata theluthi mbili au kura 128 na badala yake washindi ni Norway na Ireland ambazo zitaanza ujumbe wao mwezi Januari mwakani zikiungana pia na Mexico ambayo ilikuwa inawania kundi la Amerika ya Kusini na Karibea.
Baraza la Uchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa, ECOSOC nalo pia limepata wajumbe wapya 18 katika chombo hicho ambacho in miongoni mwa vyombo sita vikuu vya UN.
Nchi hizo ni Argentina, Austria, Bolivia, Bulgaria, Ufaransa, Ujerumani, Indonesia, Japan, Liberia, Libya, Madagascar, Mexico, Nigeria, Ureno, Visiwa vya Solomon, Uingereza na Zimbabwe.
Kuelekea Mjadala Mkuu Septemba
Wakati Mkutano wa Baraza Kuu mwaka huu unaangukia katika maadhimisho ya miaka 75 ya Umoja wa Mataifa, janga la COVID-19 linaongezea katika historia ya kikao hicho na umuhimu wa kuchukua hatua za usalama zaidi.
Tayari mipango inaendelea kwa wiki ya vikao vya ngazi ya juu ambapo wakuu wa nchi na serikali watahutubia dunia kutoka katika jukwaa la ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Rais wa sasa wa Baraza Kuu, Bwana Bande amesema kuwa ameandika barua kwa nchi wanachama kuhusu mazingira ambamo kwayo Rais ajaye wa mkutano wa 75 na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres watakuwemo ndani ya ukumbi kwa ajili ya ufunguzi rasmi ilhali viongozi wan chi watatoa hotuba zao au zilizokwisharekodiwa kwa nchi ya video.
Wawakilishi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wanatakiwa hadi Ijumaa mchana wiki hii wawe wametoa mrejesho kuhusu mapendekezo hayo.