Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema linatiwa wasiwasi mkubwa na ongezeko la machafuko katika ukanda wa Sahel ambayo yameshuhudia raia wasio na hatia wakilengwa na kusababisha maelfu kutawanywa katika wiki za hivi karibunilakini pia kuathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za misaada ya kibinadamu.
Kwa mujibu wa mashambulizi yanayofanywa na makundi yenye silaha na kuvuruga usalama wa kufanyika operesheni za kibinadamu yamesababisha watu wengi zaidi kufungasha virago na kukimbia nyumba zao kwenda kusaka usalama.
Lakini pia yameongeza shinikizo zaidi kwa jamii zinazowatunza ambazo tayari zinakabiliwa na hali ngumu ya kuhudumia watu waliotawanywa na machafuko ya siku za nyuma ambao mara nyingi ni ndugu.
Shirika hilo limesema mashambulizi ya karibuni kabisa yamefanyika Juni 5 na kukatili maisha ya raia 26 na kujeruhi wengine katika kijiji cha Binedama kwenye jimbo la Mopti katikati mwa Mali.
Makundi hayo yenye silaha pia Mei 31 yalilenga jamii zinazotunza wakimbizi katika eneo la Intikane Magharibi mwa Niger ambako duru zinasema viongozi wawili wa wakimbizi waliuawa na kiongozi mmoja kutoka jamii zilizopatia wakimbizi makazi.
Kwa mujibu wa Millicent Mutuli, Mkurugenzi wa kanda ya Afrika Magharibi na Kati wa UNHCR matokeo ya mashambulizi haya sasa watu zaidi ya 10,000 wanasaka makazi na hasa malazi kwenye eneo la Telemces ambako UNHCR na washirika wake wamewasaidia na makazi ya muda 1,800, hata hivyo limesema mazingira hapo ni mabaya kukiwa hakuna maji na suala la afya ndio hofu kubwa.
Pia ameongeza kuwa “Kuendelea kwa mashambulizi dhidi ya raia katika kanda ya Sahel ambayo yamesambaratisha Maisha ni jambo lisilokubalika na linahitaji ufumbuzi wa haraka.Watu wametawanya mara kadhaa na wanahitaji msaada wa haraka. Tunafanya kila tuwezalo kuwafikishia msaada licha ya changamoto ya sasa ya janga la COVID-19 ambalo limeongeza adha na vikwazo vingine vya usalama.”
UNHCR imejitahidi hadi sasa kuzisaidia familia zaidi ya 25,000 na linalenga kuzisaidia zingine 16,600 ifikapo mwisho wa mwezi huu wa Juni.
Hata hivyo mtihani mkubwa unaletwa na changamoto ya usalama, COVID-19 na ukata wa rasilimali fedha.
Tangu kuzuka kwa machafuko ya kwanza Sahel Kaskazini mwa Mali mwaka 2011, sasa vita hivyo vimesambaa katika maeneo ya Katikati mwa Mali, Niger hadi Burkina Faso.