Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limejulishwa kuhusu dalili za matumaini nchini Yemen huku wajumbe wakionywa kuwa wasibweteke bali watumie fursa ya sasa kuhakikisha kuna amani ya kudumu kwenye taifa hilo.
Mjumbe maalum wa Umoja waMataifa kwa Yemen, Martin Griffiths akihutubia baraza hilo kwa njia ya video kutoka Amman nchini Jordan ametoa mfano wa maeneo ya kusini akisema,“maeneo ya kusini; lakini pia kupungua kwa ghasia hivi karibuni zaidi maeneo ya kaskazini; na kuongezeka kwa nia njema baina ya pande kinzani, mfano kuachilia huru wafungwa waliokuwa wanashikiliwa na kusaka njia bunifu za kuruhusu meli za mafuta yanayohitajika zaidi kutia nanga kwenye bandari ya Hudaydah.”
Bwana Griffiths amesema ingawa ni ishara ndogo lakini ni vyema kuzipalilia.
Mjumbe huyo maalum amesema ingawa wengi walitarajia kuwa makubaliano ya amani yangalitangazwa hii leo, bado kuna maendeleoyaliyopatikana kwenye mazungumzo yaliyofanyika huko Jeddah chini ya usimamizi wa Saudi Arabia.
“Nashukuru juhudi za kupindukia za Saudi Arabia zinazoonesha ishara kuwa hatimaye mkataba huo wenye lengo la kusaka suluhu kati ya serikali ya Yemen na Baraza la mamlaka ya mpito ya eneo la kusini uko mbioni kufikiwa,”amesema Bwana Griffiths.
Mapema mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na misaada ya dharura, OCHA, Mark Lowcock amejulisha wajumbe mwezi uliopita wa Septemba, ulikuwa mwezi mbaya zaidi kwa raia ambapo raia 388 waliuawa au walijeruhiwa kutokana na mzozo unaoendelea maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
“Hii ni wastani wa watu 13 kila siku. Kuna mifano ya kutisha. Wiki iliyopita mfano watoto wane huko Hudaydah waliuawa baada ya kilipukaji kilichotokana na bomu la awali kulipuka karibu na makazi yao. Watoto wote hao wanne walikuwa wanatoka kwenye familia moja.”Amesema Bwana Lowcock.
Hata hivyo amesema licha ya changamoto zinazoendelea nchini yemen, zaidi ya mashirika 250 ya kibinadamu, mengi yao yakiwa ni ya kiyemen, yanafanya kazi kwa kuzingatia mpango wa usaidizi wa umoja wa mataifa.“Kwa pamoja tunawafikia zaidi ya watu milioni 12 nchini kote Yemen kila mwezi. Lakini kadrioperesheni za usaidizi zinavyopanuka, vichochezi vya mzozo navyo vinakuwa vibaya zaidi,”amefafanua Bwana Lowcock ambaye anaongoza ofisi ya OCHA.
Ametoa wito kwa sitisho la mapigano ili angalau waweze kufikia wahitaji akisema kwa mafnao maeneo ya kaskazini,“mashirika ya kibinadamu yanalazimika kuvuka zaidi ya vizuizi 100 vilivyowekwa na mamlaka za wahouthi au Ansar Allah, kando mwa vitendo vya manyanyaso wanavyokumbana navyo kila wakati.”