51Թ

Pande kinzani Sudan wekeni silaha chini tokomezeni COVID-19

Get monthly
e-newsletter

Pande kinzani Sudan wekeni silaha chini tokomezeni COVID-19

UN News
27 March 2020
By: 
Tarehe 3 Januari 2020 Jeremiah Mamabolo alipofika katika eneo la kambi iliyotelekezwa mjini El Geneina huko Darfur Magharibi kufuatia mapigano ya kijamii
UNAMID/Hamid Abdulsalam
Tarehe 3 Januari 2020 Jeremiah Mamabolo alipofika katika eneo la kambi iliyotelekezwa mjini El Geneina huko Darfur Magharibi kufuatia mapigano ya kijamii

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika, AU, huko Darfur, Sudan, Jeremiah Mamabolo amekazia kauli ya Katibu Mkuu wa umoja huo ya kutaka sitisho la mapigano kwenye maeneo ya mizozo wakati huu ambapo virusi vya Corona,COVID-19, vimeshasambaa katika mataifa 194.

Kupitia taarifa iliyotolewa na ujumbe wa pamoja wa UN na AU huko Darfur, UNAMID, Bwana Mamabolo amesema, anatambua huku akitiwa moyo na makubaliano ya sitisho la uhasama kati ya serikali ya mpito ya Sudan na kikundi cha upinzani cha SRF, makubaliano yaliyotiwa saini tangu tarehe 21 mwezi Oktoba mwaka jana.

“Narejelea kauli ya Katibu Mkuu na kusihi pande kinzani Sudan zitambue ugumu wa mazingira ya sasa ambayo Katibu Mkuu wa UN ameelezea kuwa ni vita halisi vya maisha yet una zifikie makubaliano ya kina haraka iwezekanavyo,”amesema Bwana Mamabolo ambaye pia ni mkuu wa UNAMID.

Ukurasa kuhusu virusivyacorona & taarifa mpya
Wasomaji wanaweza kupata taarifa na muongozo kuhusu mlipuko wa virusi vya corona (2019-nCoV) kutoka Umoja wa Mataifa, Shirika la afya duniani na mashirika mengine ya UN hapa.
Kwa habari mpya kila siku kutoka UN News, bofya hapa.

Ni kwa mantiki hiyo amesema anatumia fursa ya sasa katika kipindi muhimu cha kihistoria cha Sudan kumsihi“Abdul Wahid Al-Nur, kiongozi wa kikundi cha Sudan Liberation Army upande wa upinzani au (SLA/AW), aungane na mchakato wa amani wakati huu ambapo janga la Corona linataka umoja ili kuokoa maisha. Nashikamana na wananchi wa Sudan katika kipindi hiki muhimu na nawahakikishia msaada kutoka UNAMID.”

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, alitoa ombi la sitisho la haraka la mapigano kwenye maeneo ya mizozo duniani, akitoa wito kwa pande kinzani kuweka silaha nchini ili kushiriki kwenye mazungumzo na kuwezesha uingizaji wa misaada ya kibinadamu huku juhudi zote zikielekezwa kwenye vita dhidi ya virusi vya Corona.