Kuelekea siku ya kimataifa ya mawasiliano na habari kesho Mei 17, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa ujumbe wake wa siku hii akisema kuwa teknolojia ya habari inaweza kuwa nguzo ya matumaini, kwa kuwezesha mabilioni ya watu duniani kote kuwasiliana.
Ametolea mfano kuwa katika zama za sasa za janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, auCOVID-19, mawasiliano ya aina hiyo baina ya wapendanao, shule, vyuo, ofisi, wataalamu wa afya na wasambazaji wa huduma muhimu ni kuliko wakati wowote ule.
“Shirika la mawasiliano la Umoja wa Mataifa, ITU, linaendelea kufanya kazi na jamii ya teknolojia ya mawasiliano, TEHAMA, na mashirika ya Umoja wa Mataifa kusaidia kushughulikia janga la sasa na kulimaliza na hatimaye kukwamuka tukiwa bora zaidi,”amesema Guterres.
Katibu Mkuu amesema teknolojia mpya kuanzia kizazi cha 5 cha masafa au 5G hadi uwekezaji wa takwimu kwenye vifaa visivyoshikika na akili bandia, zote ni mbinu thabiti za kushughulikia changamoto kubwa zinazokabili dunia ikiwemo janga la Corona.
“Kutomwacha mtu yeyote nyuma kuna maanisha kutomwengua mtu yeyote kwenye mtandao,” amefafanua Katbu Mkuu.
Amesema ni kwa mantiki hiyo, katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mawasiliano hii leo,“tunakumbushwa ushirikiano wa kimataifa katika teknolojia ya kidijitali na umuhimu wake katika kusaidia kutokomeza COVID-19 na kufanikisha ajenda 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu.”