51Թ

Tunapowakumbuka waathirika wa Holocaust tuhakikishe uhalifu huo haturejeiGuterres

Get monthly
e-newsletter

Tunapowakumbuka waathirika wa Holocaust tuhakikishe uhalifu huo haturejeiGuterres

UN News
28 January 2020
By: 
Auschwitz-Birkenau, Poland.
Unsplash/Jean Carlo Emer
Auschwitz-Birkenau, Poland.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameikumbusha dunia kwamba mauaji ya maangamizi makuu au Holocaust ni uhalifu mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani na tunapowakumbuka waathirika ni jukumu la dunia kuhakikisha kwamba uhalifu huu asilani haurejei tena

Katika ujumbe wake maalum wa siku hii ambayo kila mwaka huadhimishwa Januari 27 , Guterres amesema dunia inakuja pamoja kukumbuka moja ya uhalifu mbaya zaidi katika wakati wetu,mauaji ya kupanga yaloyotekelezwa na manazi na washirika wao ya maangamizi makuu (Holocaust) .

Wayahudi milioni sita wanaume, wanawake na watoto na mamilioni wengine waliuawa kikatili.Amesisitiza kwamba

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES)

“Tunaahidi kwamba asilani hatutosahau.Tunaapa kueleza hadithi zao na kuwaenzi kwa kutetea haki ya kila mtu ya kuishi kwa utu katika ulimwengu wenye haki na amani.Miaka sabini na tano iliyopita, ukombozi wa kambi za kifo ulimaliza mauaji lakini uliushtua ulimwengu, kwani wigo kamili wa uhalifu wa Manazi umeonekana bayana.”

Katibu Mkuu amesema kutokana na matendo haya ya kutisha, Umoja wa Mataifa uliundwa ili kuleta mataifa pamoja kwa amani na ubinadamu wetu wa pamoja, na kuzuia kurudia kwa uhalifu kama huu dhidi ya ubinadamu.

Hata hivyo ameonya kwamba

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES )

“Kuibuka tena kwa chuki katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na machafuko ya itikadi kali kushambulia kwenye maeneo ya ibada, inaonyesha kwamba chuki dhidi ya Wayahudi, aina zingine za ubaguzi wa kidini, ubaguzi wa rangi na ubaguzi mwingine bado upo pamoja nasi.”

Amesema hivi sasa ikiwa ni miaka sabini na tano baadaye, Unazi-mamboleo na fikra za kudhani wazungu ni bora zaidi zinaibuka tena, na kuna juhudi zinazoendelea kupunguza ukubwa wa mauaji ya maangamizi makuu na kuyakana au kudunisha jukumu la wahusika.

Lakini amehimiza kwamba kama vile chuki inavyoendelea, vivyo hivyo linapaswa kuwa azimio letu la kupigana nayo.

Ametoa wito kwamba leo na kila siku, tunawakumbuka waathirika wa mauaji haya ya maangamizi makuu kwa kufuata ukweli, ukumbusho na elimu, na kwa kujenga amani na haki kote ulimwenguni.

Lazima tuchagize amani

Rais wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Balozi Tijjani Muhammad-Bande akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani, Septemba 2019
Rais wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Balozi Tijjani Muhammad-Bande akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani, Septemba 2019
UN /Mark Garten

Kwa upande wake Rais wa Baraza Kuu, Tijjani Muhammad-Bande, ameyaita mauaji ya maangamizi makuu kama ni “mauaji mabaya zaidi ya kimbari katika historia ya binadamu.”

Akikumbusha maelezo ya kusikitisha ya manusura amesisitiza kwamba kuna haja ya kuongeza juhudi kuhakikisha kwamba kuna ujumuishwaji, amani na jamii ya kimataifa inayoishi kwa amani na utulivu ambayo inachagiza umoja na kukumbatia tofauti.

“Wanatukumbusha kwamba kila wakati haja ya kuwa makini kwa kuwa na juhudi za pamoja ambazo zinapinga chuki, kauli za chuki ikiwemo mifumo mingine ya kutovumiliana ambayo inachochea ubaguzi, chuki dhidi ya wageni na mifumo mingine ya kibaguzi.”

Bwana. Bande ameongeza kuwa vijana wa leo watakuwa watu viongozi wa kesho akisistiza kwamba kuna haja ya kuwafundisha kuhusu suala hili na uhalifu mwingine mbayá ili kuhakikisha kwamba unyama na ukatili wa mauaji ya maangamizi makuu asilani hautokei tena.

“Tunapaswa kukumbuka siku zote waathirika wa mauaji ya maangamizi makuu na kuhakikisha kwamba waliyopitia yanatumuka kutukumbusha kila wakati haja ya kuchagiza amani, utulivu, kuvumiliana, ushirikiano na ujumuishwaji wa matakwa yetu ya pamoja kwa ajili ya kuwa na dunia ya amani na mafanikio.”

Simama kidete kwa ajili ya amani na haki za binadamu

Naye Kamishina Mkuu wa haki za binadamu Michelle Bachelet katika ujumbe wake maalum kuhusu siku hii amekumbusha kwamba Umoja wa Mataifa uliundwa kukabiliana na mauaji, unyama na chuki zilizopsambazwa na utawala wa kinazi wakati wa vita ya pili ya dunia ili kujenga upya dunia ya haki na amani.

Amesema “Lakini leo hii watu ambao wanaonekana kuwa ni tofauti wanakabiliwa na mifumo mbalimbali ya chuki, ambapo hata viongozi wanachochea ubaguzi au machafuko dhidi ya Wayahudi, waislam, wahamiaji au watu wengine kutoka makundi ya jamii za walio wachache.”

Bi. Bachelet amesisitiza kwamba ubinadamu asilani usiruhusiwe kurejea katika fikra hizo za kutokuwa na haki na unyama wa hali ya juu.

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet
Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet
UN Photo/Laura Jarriel

Kamishina Mkuu amewapongeza wanawake, wanaume na vijana kote duniani ambao wameonyesha ujasiri , huruma na kusimamia misingi ya kuvumiliana na haki za binadamu katika wakati huu ambapo dunia inajaribu kuuharamisha utu wa watu.

Amesisitiza kwamba “Suluhu ya kudumu dhidi ya ongezeko la chuki ni elimu ya msingi ya mtazamo ba mioyo ya watu ili isibadilike. Elimu ya haki za binadamu sio tu inahakikisha misingi ya haki kwa kila mtu na kutambua historia lakini pia inawawezesha watu kuziwajibisha serikali zao.”

Inahakikisha utu wa pamoja huku pia ikisaidia watu kuafanya maamuzi ya busara wakiwa na ufahamu , kutatua migogoro kwa njia ya amani na kushiriki kwa uangalifu katika jamii zao.