Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Nigeria Edward Kallon amelaani vikali shambulio la kikatili lililofanywa na makundi yenye silaha kwenye eneo la Monguno Nganzai nchini Nigeria siku ya Jumapili.
Kwa mujibu wa taarifa ya mratibu huyo wa Umoja wa Mataifa mashambulizi hayo yamekatili maisha ya takriban raia 40 akiwemo mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minne, kujeruhi watu wengine 37 na kufanya uharibifu mkubwa kwenye kituo cha masuala ya kibinadamu.
Kufuatia mashambulizi hayo Bwana. Kallon amesema“nimeshtushwa sana na taarifa za vifo vingi vya raia akiwemo mtoto katika mashambulizi haya kikatili, natuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika na kuwatakia ahuweni ya haraka majetuhi. Nasikitishwa sana na kuendelea kwa machafuko yanayoendeshwa na makundi yenye silaha kwenye jimbo la Borno.”
Tarehe 13 mwezi huu wa Juni kundi la watu wenye silaha likiwa na lori lililojaa silaha nzito nzito, lilivamia jamii ya Goni Usmanti katika eneo la Nganzai kabla ya kuingia kwenye mji wa Monguno na kusababisha mapambano na jeshi la serikali ya Nigeria,mapambano yaliyodumu kwa saa mbili.
Baada ya hapo wakaenda kuvamia kituo cha misaada ya kibinadamu ambako kulikuwa na wahudumu zaidi ya 50 ingawa kituo hicho likipata uharibifu tu, duru zinasema kuwa kililengwa makusudi.
Kallon amesema“ninashukuru kwamba wafanyakazi wote wako salama lakini nimeshtushwa sana na ukubwa wa shambulio lenyewe. Hili ni miongoni mwa mashambulio mengine mengi yanayoathiri raia na wahudumu wa misaada ya kibinadamu. Raia, wahudumu wa kibinadamu na miundombinu yao hawapaswi kushambuliwa na ni lazima walindwe.”
Ametoa wito kwa pande zote nchini Nigeria kuheshimu na kulinda hali za raia kila wakati.