Nchini Kenya ambako tayari mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona, auCOVID-19, umesababisha vifo huku wagonjwa wapya wakiendelea kuripotiwa, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaunga mkono harakati za kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo ambavyo hadi sasa havina tiba wala chanjo.
Wilson Langat, Naibu Mkurugenzi wa Idara ya afya ya umma katika kaunti ya Nairobi nchini Kenya, anasema jiji la Nairobi limechukua hatua kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya Corona hususan kwenye eneo la mabanda la Kibera, ambako hatua za kutochangamana bado ni changamoto kutokana na msongamano.
Hatua hizo zinatakelezwa kwa ubia pia na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,ambalo hivi karibuni lilipatia kaunti ya Nairobi, vifaa vya kujisafi zikiwemo sabuni na maji ambapo Bwana Langat anasema kuwa,"tunahakikisha kwamba unawaji mikono kwa maji tiririka kutasaidia vita dhidi ya COVID-19. Pia tunapuliza dawa kutakasa maeneo na huduma, pengine kuna ambao hawanawi mikono tunataka kuhakikisha huduma ziko safi.”
Kila mfanyakazi wa kijamii wa kujitolea katika eneo la Kibera anapatiwa miche miwili ya sabuni ambayo ataiweka kwenye kituo cha kunawa mikono.
Mamlaka za Kaunti ya Nairobi zinasema kuwa wakazi wa Kibera wameelimishwa jinsi ya kunawa mikono kwa ukamilifu sambamba na kutochangamana.
Kwa upande wake, Agnes Makanyi ambaye ni afisa wa huduma za kujisafi, au WASH, UNICEF anasema, kwamba“UNICEF ina msisitizo wa kipekee kwa makazi yasiyo rasmi, na kwa Nairobi tunalenga kaya elfu 20, ambazo zitakuwa zinapokea sababu kwa kipindi cha miezi 3 ijayo kuhakikisha wanajikinga dhidi ya maambukizi. Na tutafika katika maeneo mengine yasiyo rasmi katika kaunti 14 za kipaumbele.”
Pamoja na hii, UNICEF imesambaza vifaa vya kujisafi kwa kaunti 11, vifaa kama vile miche 40,000 ya sabuni, zaidi ya ndoo elfu 20 za lita 10, madumu ya kupulizia dawa na vifaa vya kunawia mikono ili kila mtu aweze kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka